January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mikakati thabiti ya kuimarisha mifumo ya kukabiliana na maafa yawekwa

Na Mwandishi wetu

Serikali kupitia Idara ya Menejimenti ya maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu imeendelea kuimarisha mifumo ya usimamizi wa masuala ya maafa nchini ili kuendelea kuwa na mikakati thabiti ya kukabiliana na maafa nchini.

Akizungumza wakati wa semina kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) Naibu Katibu Mkuu wa ofisi hiyo Bw. Anderson Mutatembwa amesema kuwa tayari ofisi yake imeendelea kuratibu Mfumo Shirikishi wa kidigitali wa usimamizi wa taarifa za masuala ya maafa, uwepo wa Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura, uwepo wa vifaa vya misaada ya kibinadamu vinavyohifadhiwa kwenye maghala, utoaji wa elimu kwa umma pamoja na ujenzi wa kituo cha Usimamizi wa Maafa katika eneo la Nzuguni Dodoma.

Akizungumzia maandalizi katika kuelekea mvua za el nino amesema kuwa, ofisi imeendela kuziwezesha kamati za maafa katika mikoa 14 iliyotabiriwa kupata athari za mvua hizo zilizotabiriwa na Mamlaka ya hali ya hewa nchini na kuzikumbusha kuendelea kujiimarisha katika maeneo yao ili kukabiliana na madhara yanayoweza kutokea wakati wa mvua hizo.

“Tumeshaifikia mikoa iliyotajwa kuathiriwa na mvua za el nino kwa kutoa elimu kwa kamati za maafa ngazi ya Mkoa hadi Vijiji lengo ni kuwajengea uelewa zaidi na kukumbusha jamii kuchukua hatua za mapema kabla ya kupata madhara ya uwepo wa mvua hizo,” alisema Mutatembwa.

Aidha akiwasilisha taarifa kuhusu dhana ya menejimenti ya Maafa na Mfuko wa Taifa wa usimamizi wa maafa nchini Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Menejimenti ya maafa Bw. Charles Msangi ameeleza kuwa, Ofisi imeendelea kuimarisha mfumo wa mawasilino kupitia kituo cha operesheni na mawasiliano ya dharura ambacho kipo chini ya Ofisi hiyo kinachopokea taarifa za majanga kwa kupiga namba 190 au kuandika ujumbe kwenda namba *190# ok ambapo ofisi inapokea taarifa hizo na kuzifanyia kazi katika maeneo yote nchini.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe.Japhet Hasunga ameipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuendelea kuratibu masuala ya maafa nchini huku akiwakumbusha kuongeza nguvu katika utoaji wa elimu kwa umma na kuwa na mifumo rahisi ya kuyafikia makundi yote nchini kuanzia ngazi ya Kijiji ili kuwa na uelewa wa pamoja juu ya masuala hayo.

“Endeleeni kutoa elimu kwa umma na kuikumbusha jamii kuchukua hatua hususan katika kipindi hichi kilichotabiriwa kuwepo na mvua za el nino nchini, pia ni wakati sasa wa serikali kuimarisha mawasiliano wakati wa maafa ili kuwa na jamii salama na stahimilivu dhidi ya madhara ya maafa,” alisisitiza Mhe. Hasunga.