November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Miili ya watu 14 wa ajali Singida waanza kuzikwa

Na Damiano Mkumbo,TimesMajira Online,Singida

JUMLA ya miili 14 ya marehemu waliofariki kutokana na ajali iliyotokea Desemba 13, mwaka huu eneo la Mkiwa Wilayani Ikungi barabara ya Singida Dodoma walitambuliwa na kuanza kusafirishwa kwenda Mkoa ya Mwanza na Mbeya.

Viongozi wa dini wakisalia miili ya marehemu 14 waliofariki kwa ajali eneo la Mkiwa wilayani Ikungi ambao wamesafirishwa kwenda Mkoa wa Mwanza na Mbeya. Picha na Damiano Mkumbo

Miili hiyo ilitambuliwa kuanzia juzi hadi jana asubuhi baada ya ujumbe wa watu watano kutoka familia za marehemu Kata ya Mabatini Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza kuwasili mjini hapa na kushirikiana na uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida uliofanyika kwenye chumba cha maiti.

Marehemu hao,ambao wapata ajali hiyo ilitokana na gari lao la aina ya hiace kugongana uso kwa uso na lori la mizigo ni pamoja na Ustaadhi Mrisho Swed (33), Ibrahimu (25) aliyekuwa anakwenda huko kufungisha ndoa, Zakia Ibrahimu (13) mwanafunzi wa shule ya sekondari mojawapo Mkoani Mwanza wa kidato cha tatu.

Wengine waliofariki papo hapo katika ajali hiyo wakati wakisafiri kwenda kwenye sherehe za harusi Mjini Itigi ni Lamrati Mkama (22),Rehema Husseini (42), Abdul Milambo (28), Halima Rashidi (20), Luhunani Ibrahimu mtoto mchanga wa kiume wa mwaka mmoja na miezi mitatu, Majaliwa Rashidi (40) dereva wa hiace na aliyejulikana kwa jina la Mama mdogo (60) wote wakiwa wakazi wa Wilaya ya Nyamagana.

Katika ajali hiyo ambayo ilielezwa na Kamanda wa Polisi Sixbert Njewike kuwa ilisababishwa na uzembe wa Dereva wa Hiace, wengine waliyotambuliwa ni Chiristian Richard (24) rafiki wa harusi mtarajiwa mkazi wa Mbeya na wakazi watatu wa Kijiji cha Damankia Wilayani ya Ikungi Mkoani Singida,walipandia gari hilo kituoni hapo kwenda Itigi msibani.

Watu hao wametajwa kuwa ni Joseph Lodvick,mzee Wiliam na Anna Gabriel ambao mili yao yainaendelea kuifadhiwa katika chumba cha maiti hospitalini hapo,ambao itachukuliwa kwenda kuzikwa baada ya maandalizi kukamilika.

Akizungumza wakati wa kuaga miili hiyo nje ya chumba cha maiti juzi,Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Rehema Nchimbi, amesema Serikali imepokea msiba huo ambao unahusu Taifa kwa huzuni kubwa wa kuwa marehemu na majeruhi walikuwa wakienda kwenye furaha lakini ilibadilika kuwa huzuni ghafla.

“Ninatoa pole kwa familia,jukumu la Serikali kutambua heshima ya binadamu na kuwatumikia watu wake wote ndiyo maana imechukua wajibu wake wa kushirikiana na wanafamilia na wadau wote, ikagharamikia shughuli zote za msiba ikiwa pamoja na kutengeneza majeneza na kusafirisha miili hiyo kwenda sehemu husika za mazishi,” amesema.

Akitoa salamu za Rais Dkt.John Magufuli alizopokea amesema alitoa salamu za pole kwa wote waliyoguswa na majonzi hayo pamoja na majeruhi wawili wakiendelea kutibiwa Hospitali ya Mtakatifu Gaspari Itigi kupona upesi na kurudi katika shughuli zao.