Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
MIFUKO ya Hifadhi ya Jamii nchini kupitia Shirikisho la Mifuko hiyo (TSSA) imetakiwa kufanya uwekezaji wenye tija kupitia uchumi wa Kijani, Blue, Njano na TEHAMA kwa kuhakikisha wanaanzisha viwanda vitakavyotumia malighafi za ndani.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu) Jenista Mhagama wakati akifunga mkutano wa wajumbe wa Bodi ya Shirikisho la Mifuko hiyo, TSSA linaloundwa na NSSF,PSSSF, NHIF, WCF, ZSSF uliofanyika jijijni Mwanza.
Mhagama amesema, ilani ya Chama cha Mapinduzi(CCM) ya mwaka 2020 hadi 2025 inaelekeza kufanya uwekezaji makini katika viwanda vyenye uwezo wa kutengeneza ajira nyingi (rasmi na zisizo rasmi) kwa misingi ya kuzalisha ajira, na kuongeza wigo wa wanachama wa kujiunga na Mifuko ya hifadhi ya jamii.
Amesema, wajibu wa Wenyeviti wa Bodi ya Mifuko hiyo kushauri ni mifuko hiyo kuwekeza katika viwanda vitakavyotumia malighafi zipatikanazo hapa nchini ili kukuza soko la mazao ya wakulima ingawa anatambua kuna baadhi ya viwanda waliishaanza kama vile viwanda vya Vifaa Tiba, viwanda vinavyotumia Pamba, viwanda vya vya viatu kama kile cha Karanga Moshi, kiwanda cha Tangawizi kilichopo Same kinacholenga kuwainua akina mama.
Katika kusimamia mifuko hiyo, Bodi hiyo ina jukumu la kushauri na kuona kuwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii inawekeza katika aina ya viwanda vinavyotumia malighafi zinazopatikana kwa wingi hapa nchini na si kuagiza kutoka nje ya nchi.
“Nchi yetu ina uchumi wa kijani, njano,tehama na bluu,hivyo lazima kama mifuko tushughulike na uchumi huo, nashangaa watanzania tuna mito ,tuna maji lakini tunashindwa kutengeneza hata dripu ambapo tumekuwa tukitumia mamilioni kuagiza dripu nchini Uganda ni jambo la kusikitisha,hivyo hakikisheni mnaanzisha
viwanda ambavyo vitatumia malighafi za hapa nchini vinavyotegemea soko la ndani ikizingatiwa kuwa nchi yetu ina watu zaidi milioni 50 hivyo soko zuri tunalo kwa ajili ya bidhaa zetu,” amesema Mhagama.
Amesema, aina ya viwanda viwe ni vile vitakavyotoa ajira kwa wingi ili kuongeza idadi ya wanachama na hivyo kupanua wigo wa sekta ya Hifadhi ya Jamii mfano kiwanda cha Karanga ambacho kitatoa ajira zaidi ya 4000, kiwanda cha vifaa vya Hospitali Simiyu(WCF na NHIF),kama wyaziri mwenye dhamana ya ajira, atafarijika zaidi kusikia kwamba malengo hayo yanatimizwa na viwanda hivi vinaongeza ajira nyingi kwa vijana.
Mhagama amesema jukumu lingine linalopaswa kufanywa na bodi hizo ni kushauri na kusimamia uwekezaji unaofanywa na mifuko ya hifadhi ya jamii kwa lengo la kulinda pesa za wanachama,sera ya Serikali ya awamu ya tano ni uchumi wa viwanda kama dira ya miaka mitano iliyopita na miaka mitano ya sasa.
Pia alitumia fursa hiyo kumuhimiza Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mifuko ya Hifadhi ya Jamii Nchini(TSSA),Meshack Bandawe kwa jitihada na umaarufu aliotumia katika kuhakisha na kujenga mji wa Serikali mkoani Dodoma huo huo atumie katika kuhakikisha mifuko hiyo inawekeza katika viwanda ikiwa ni njia ya ushiriki wa sekta ya Hifadhi ya Jamii katika kukuza uchumi na kuinua maisha ya Mwanachama mmoja mmoja na wanachama wote kwa ujumla na kuchangia katika kuinua uchumi wa taifa.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mifuko ya Hifadhi ya Jamii Nchini(TSSA),Meshack Bandawe, amesema jumla ya wajumbe 40 wa wameshiriki mafunzo ya wajumbe wa bodi za mifuko ya Hifadhi ya Jamii yenye lengo la kuboresha utendaji katika bodi zao na kuongeza uelewa juu ya majukumu ya bodi kulingana na mabadiliko yanayoendelea kutokea katika sekta ya hifadhi ya jamii nchini ikiwemo masuala ya uwekezaji na ushiriki wa mifuko hiyo katika uchumi wa taifa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TSSA William Erio amesema,mafunzo hayo yanawapa fursa ya kujikumbusha mambo mbalimbali ambapo mara ya mwisho kufanya mkutano huo ilikuwa mwaka 2016,wameamua kufanya hivyo ili kuongeza elimu na mafunzo ikiwa ni njia moja wapo ya kuongeza mapato na taasisi yao iweze kujiendeleza bila kutegemea michango kutoka kwa taasisi zingine.
Erio amesema katika mafunzo hayo wameondoka na changamoto ambayo wanaenda kuangalia ni kwa namna gani mifuko hiyo inaweza kushiriki katika mikakati ya Serikali ya kuweza kuwekeza katika sekta ya kilimo,mifugo na uvuvi pia katika kuanzisha viwanda waangalie na vile vilivyokuwepo kwa kuvirudisha katika uzalisha kwa kutumia vitengo vyao vya uwekezaji wataenda kuangalia ni wapi wataweza na kuanza kufanyia kazi.
Amesema shirikisho lao lipo katika mipango ya kuvifufua viwanda vyote nchini ambavyo havifanyi kazi viweze kurejea tena ambavyo itasaidia sana katika kutimiza lengo la awamu ya tano katika kuelekea Tanzania ya Viwanda.
“Nchi yetu inaupatikanaji mkubwa sana wa malighafi na asilimia kubwa ya watanzania wanashiriki sana katika shughuli za kilimo,ufugaji na uvuvi,hivyo mifuko yetu itasaidia katika kushiriki kwenye miradi ya Kimkakati,”amesema Erio
More Stories
Rais Samia kuzindua mfuko wa kuendeleza kazi za wabunifu
Makalla ampongeza Lissu kukiri CHADEMA haina wagombea Serikali za Mitaa
Chande azindua misheni ya uangalizi uchaguzi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika