November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mifugo 303 ikisafirishwa nje ya nchi kimagendo

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia doria ya pamoja wamefanikiwa kukamata watuhumiwa wawili wakiwa na jumla ya mifugo 303 ambayo walikua wanaisafirisha kwenda Nje ya Nchi kwa njia za magendo bila kuwa na vibali.

Akitoa taarifa hiyo huko maeneo ya Mnada wa Longido, Kamanda wa Polisi Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo Nchini Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Simon Pasua leo Novemba 19, 2023 amebainisha kuwa mifugo hiyo pamoja na watuhumiwa hao wamekamatwa maeneo ya Buguruni C Wilaya ya Longido Mkoani Arusha.

Kamanda Pasua amefafanua kuwa bado wanaendelea na upelelezi, na pindi utakapokamilika watuhumiwa hao watafikishwa Mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.

Aidha ametoa wito kwa wafugaji wote nchini kuacha tabia ya kutorosha mifugo kwenda Nje ya Nchi bila ya kufuata utaratibu wa kupata vibali toka serikalini, kwani Jeshi hilo litachukua hatua za kisheria dhidi yao ikiwa ni pamoja na kukamata mifugo hiyo na kuwafikisha mahakamani.

Sambamba na hilo pia ametoa rai kwa wafugaji kote Nchini kutumia vizuri msimu huu wa mvua ambao kuna malisho ya kutosha, kwa kutenga maeneo ya malisho ambayo watayatumia katika msimu wa kiangazi ambapo itasaidia kuepukana na migogoro baina ya wafugaji na wakulima.

Kwa upande wake Daktari wa Mnada wa Longido Dkt. Ally Hamka amesema changamoto kubwa wanayokabiliana nayo ni baadhi ya wafanyabaishara wa mifugo kutokuwa waaminifu kwa kukwepa kupeleka mifugo yao katika mnada huo kwa ajili ya kupewa vibali.

Aidha amebainisha kupitia doria hiyo ambayo ni endelevu itasaidia kwa kiasi kikubwa kuwabaini na kuwakamata baadhi ya wafanyabishara wachache wanaotorosha mifugo na kuwachukulia hatua za kisheria.

Naye Bwana Joseph Lengashe ambaye ni mfugaji lakini pia mfanyabiashara amewaasa wafanyabishara wenzake kufuata utaratibu ambao umewekwa na Seririkali wa kupata vibali vya kusafirisha mifugo yao ili kuepuka hasara ambazo wanaweza kukutana nazo pindi mifugo yao itakapokamatwa na kutaifishwa.