November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Miaka miwili ya Samia, Shida ya maji Handeni kuwa historia HTM yajenga miradi mipya, upo wa Miji 28

Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online, Korogwe

MRADI mkubwa wa maji wa kitaifa wa Handeni Trunk Main (HTM) uliopo Wilaya ya Handeni mkoani Tanga ulianzishwa mwaka 1974 kwa madhumuni ya kutoa huduma kwa wananchi wa wilaya za Handeni na Korogwe.

Wananchi wa Kata ya Kwamagome, Halmashauri ya Mji Handeni wakinufaika na Mradi wa Maji Kwamagome.

Mradi huo ambao ulijengwa kwa ufadhili wa nchi ya Ujerumani kupitia Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GTZ na sasa GIZ), ulikusudia kutoa huduma ya maji kwa wananchi 180,000 waliopo kwenye vijiji 60 kwa wakati huo, huku ukiwa na mtandao wa bomba kuu la kilomita 316, na mabomba ya usambazaji yenye mtandao wa kilomita 100.

Mradi huo ulikuwa utoe huduma kwa ukamilifu kwa miaka 20 tu halafu ufanyiwe upembuzi yakinifu upya halafu ukarabati mkubwa ili kuweza kutoa huduma kwa kukidhi mahitaji ya wananchi ikiwemo kuangalia ongezeko la watu.

Lakini mradi huo ulishindikana kufanyiwa ukarabati mkubwa, hivyo kujikuta unafanyiwa ukarabati mdogo ikiwemo kuongeza miundombinu ya maji kwa kuangalia upatikanaji wa fedha na mahitaji yaliyopo, hivyo kushindwa kukidhi mahitaji ya wananchi kwa sasa.

Mwandishi wa makala haya ameweza kuzungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi Mradi wa HTM Mhandisi Yohana Mgaza, na kueleza mafanikio ya miaka miwili ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kumaliza changamoto ya maji Wilaya ya Handeni.

Mgaza anasema kwa miaka miwili ya Dkt. Samia, wameweza kupata fedha ya kujenga miradi ya maji itayowasaidia wananchi kwa muda mfupi na mrefu ili kuona tatizo la maji linakuwa historia katika Wilaya ya Handeni.

Mfumo wa Solar uliofungwa kwenye Mradi wa Maji Mabanda kwa ajili ya kuvuta maji kutoka kwenye kisima kirefu kwenda kwenye tenki na kusambazwa katika mabomba.

“Katika Mradi wa Maji Mabanda uliopo Kata ya Mabanda, Halmashauri ya Mji Handeni tumejenga mradi kwa gharama ya sh. 671,349,822 kupitia fedha za Mfuko wa Maji wa Taifa (NWF). Mradi huo ulioanza Septemba 15, 2021, ulikamilika Machi 31, 2022 kwa asilimia 100. Mradi huo umejengwa tenki lenye ujazo wa lita 100,000, laini ya bomba kuu la inchi nne (4) na urefu wa kilomita tatu.

“Bomba la kusambaza maji ni kilomita 13, vituo vya kuchotea maji (vilula) 20, ambapo Kata ya Mabanda vilula 16, na Konje vilula vinne (4). Wananchi 6,500 wa mitaa mitano ya Komoza, Bagamoyo, Kwedigongo, Mabanda na Kwenguto, pamoja na Mtaa wa Konje watafaidika na maji hayo” anasema Mgaza.

Pia kwenye eneo la Mankinda kumechimbwa kisima kirefu, kujengwa nyumba ya mitambo (pamp house), kulaza mabomba yenye urefu wa kilomita mbili na kufunga solar, ambapo maji hayo pia yataingizwa kwenye tenki la Mradi wa Maji Mabanda na kusambazwa kwa wananchi.

Mradi wa Maji Kwediamba uliopo Kata ya Kwediamba Halmashauri ya Mji Handeni. Mradi huo hadi kukamilika kwake utagharimu sh. 875,921,494, na unajengwa na Serikali kupitia fedha za Mfuko wa NWF. Hadi sasa mradi umetekelezwa kwa asilimia 60, na kazi zilizofanyika ni kuchimba kisima kirefu, kujenga tenki la lita 150,000 kulaza bomba kuu la nchi nne (4) la kilomita sita na chemba tano.

Kazi zilizobaki ni kulaza bomba za kusambaza maji kilomita 17.92, kujenga vilula 29, na kujenga chemba 20. Idadi ya wanufaika ni wananchi 5,746 kwenye mitaa mitano ya Mpakani, Kwenkambala, Tuliani, Kwediamba na Kwedizando.

Mradi wa Maji Kwamagome uliopo Kata ya Kwamagome, Halmashauri ya Mji Handeni. Gharama ya Mradi ni sh. 344,754,062, huku kati ya fedha hizo, sh. 244,754,062 ni fedha za UVIKO 19, na umekamilika kwa asilimia 100.

Mradi huo ulianza ujenzi Aprili 15, 2022 na kukamilika Septemba 30, 2022. Kazi zilizofanyika ilikuwa ni kuchimba kisima kirefu na kufunga pampu, kujenga tenki la ujazo wa lita 100,000, kujenga nyumba ya mitambo (pamp house), kulaza bomba kuu la inchi 2.5 la urefu wa kilomita 2.07, bomba la kusambaza maji la kilomita 15.281, na vilula 13.

Wananchi 4,664 watanufaika na mradi huo waliopo kwenye mitaa ya Kwamagome, Hedi, Mji Mpya, Sasioni, Lusanga na Lolopi.

Mradi wa Maji Majani Mapana uliopo Kata ya Kabuku Ndani, umejengwa kwa sh. 352,463,382, na umekamilika kwa asilimia 100, na umejengwa kwa fedha za UVIKO 19. Wanufaika wa mradi ni 2,521 kwenye Kijiji cha Majani Mapana, ambapo kuna vitongoji vya mikoroshini, mkulima, Ujamaa, Kwamaluli, Kibongo na Shuleni.

Mradi huo ulioanza Novemba 17, 2021 na kukamilika Juni 30, 2022, ulihusisha kuchimba kisima, kujenga nyumba ya mitambo, kujenga tenki lenye ujazo wa lita 100,000, kujenga bomba kuu kwa kilomita 2.6, kujenga bomba la kusambaza maji kwa kilomita 7.85, na kufunga solar, na kujenga vilula tisa.

Kazi nyingine zilizofanywa na HTM ni kufunga pampu ya akiba kituo cha kusukuma maji Kwamatuku kwa sh. milioni 244.

Mradi wa Maji Kabuku Nje. Gharama ya mradi ni sh. 303,048,000, na mradi upo asilimia 90, na kilichobaki ni kuunganisha umeme na kufunga pampu.

Wanufaika ni 2,000 katika vijiji vya Kabuku Kaskazini, Kabuku Nje na Kabuku Mjini, ambapo mradi huo upo kwenye kata mbili za Kabuku. Mradi huo umehusisha kuchimba kisima, pamp house, kulaza bomba kuu la kilomita nne (4) na kuweka mnara wa tenki, na kununua matenki mawili yenye ujazo wa lita 10,000 kila moja.

MRADI WA UCHIMBAJI VISIMA

Zoezi la uchimbaji visima lilikamilka kwa uchimbaji wa visima saba maeneo tofauti ya Wilaya ya Handeni ili kukabiliana na changamoto ya uhaba wa maji.

Visima saba vimechimbwa ili kukabiliana na hali ya ukame, lakini pia maji yatakayozalishwa kwenye visima hivyo yataweza kuingizwa kwenye mtandao wa maji ya bomba kwa kuwekwa kwenye matenki.

Visima hivyo vimejengwa Kabuku Nje, Komkonga, Kwachaga, Bwawani, Ndelema, Malezi na Mankinda. Visima hivyo vyote vimechimbwa na kukamilika, na gharama ya mradi huo ni sh. 175,028,220.

MRADI WA MAJI SEGERA- KABUKU

Mradi wa Maji Segera- Kabuku utakuwa mkombozi kwa wananchi wanaoishi pembezoni mwa barabara kuu ya Dar es Salaam kwenda Arusha kuanzia Segera- Kabuku- Mkata hadi Manga.

Mradi huo ambao utatekelezwa kwa gharama ya sh. 25,546,028,652, na wananchi 120,000 watanufaika kutoka kwenye vijiji 19 katika kata tisa za Segera, Kwamgwe, Kwedizinga, Mgambo, Kabuku, Kabuku Ndani, Komkonga, Kitumbi na Ndolwa.

Mradi huo ambao bado haujaanza, lakini tayari mkataba wa ujenzi umesainiwa, na Mkandarasi ni Chichi Engineering Company Ltd wa jijini Dar es Salaam, na ataanza ujenzi wakati wowote Aprili, mwaka huu, na kukamilisha ujenzi Aprili, 2025.

Kazi zitakazofanyika ni kujenga banio ama dakio (Intake) kwenye eneo la Segera kutoka Mto Pangani, na banio hilo litakuwa na uwezo wa kupitisha lita za maji milioni 6.2 kwa siku. Kutajengwa tenki kubwa la lita milioni mbili kwenye Kijiji cha Chanika Kofi, ujenzi wa chujio eneo la Segera, nyumba ya mitambo na maabara.

Pia kutajengwa bomba kuu la inchi 12 lenye urefu wa kilomita 26 kutoka kwenye chujio hadi tenki, na kutakuwa na mtandao wa mabomba ya kusambaza maji yenye kipenyo cha inchi mbili hadi 16 kwa urefu wa kilomita 80.

MRADI WA MAJI MIJI 28

Mradi wa Maji wa Miji 28 nchini, ni mradi utakaomaliza changamoto za maji katika Wilaya ya Handeni, lakini pia mradi huo utafikisha maji kwenye miji ya Korogwe, Muheza na Pangani.

Na mradi huo ambao kwa Mkoa wa Tanga utakuwa chini ya HTM, utaanza Aprili, 2023, na utahusisha chanzo kipya cha ujenzi wa banio ama dakio (Intake) kutoka Mto Pangani, na kwa siku lita milioni 52 za maji zitazalishwa.

Lakini pia kutajengwa chujio jipya, mtambo wa kutibu maji, kulaza bomba kuu la kutoka kwenye banio hadi kwenye chujio lenye urefu wa kilomita saba. Kutoka kwenye chujio hadi Mji wa Korogwe kutajengwa bomba lenye urefu wa kilomita 24, na bomba kuu la kutoka kwenye chujio kwenda Kwamatuku litakuwa la kilomita 16.

Mradi huo ukikamilika, utaondoa tatizo la maji kwa asilimia 100 kwenye Wilaya ya Handeni, miji ya Korogwe, Muheza na Pangani.