Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoani Tabora inajivunia kupata mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka 3 ya uongozi wa Rais wa awamu ya 6 wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan.
Akiongea na Mwandishi wa gazeti hili Ofisini kwake jana Meneja wa Mamlaka hiyo Mkoani hapa Fredrick Kanyilili alisema kuwa kasi na weledi wa Rais Samia vimekuwa kichocheo cha utendaji mzuri kwa Watumishi wa taasisi hiyo.
Alisema kuwa katika kipindi cha miaka 3 tangu aingie madarakani, Mamlaka hiyo imefanikiwa kuwa na Ofisi katika Wilaya zote 7 za Mkoa huo huku Wilaya ya Uyui ikihudumiwa na Ofisi ya Tabora Manispaa.
Alifafanua kuwa mbali na kuwa na Ofisi katika Wilaya hizo jengo la Ofisi za TRA Mkoa nalo linafanyiwa ukarabati mkubwa ili kuwa na mwonekano bora zaidi, jengo hili litakuwa kichocheo kikubwa cha kasi ya utendaji wa Mamlaka hiyo.
Mbali na mafanikio hayo, Kanyilili alibainisha kuwa kasi ya ukusanyaji mapato imekuwa ikiongezeka kila mwaka hivyo kuwezesha Mamlaka hiyo kuvuka lengo kila mwaka.
Aidha alieleza kuwa TRA Mkoa imefanikiwa kusajili walipa kodi wapya wapatao 12,512 katika kipindi hicho ambapo walipa kodi 4,813 walisajiliwa kwa mwaka 2020/2021, walipa kodi 3,726 mwaka 2021/2022 na 3,973 kwa mwaka 2022/2023.
Kuhusu mapato, Meneja alieleza kuwa katika kipindi cha miaka 3 Mamlaka hiyo ilipangiwa kukusanya kiasi cha sh bil 76.9 ambapo kwa mwaka 2020/2021 ilipaswa kukusanywa sh bil 24.82, mwaka 2021/2022 sh bil 26.45 na mwaka 2022/2023 sh bil 25.70.
Alifafanua kuwa kwa mwaka 2020/2021 lengo lao ilikuwa kukusanya sh bil 24.8 lakini wakakusanya bil 24.7 sawa na ufanisi wa asilimia 99.7 na mwaka 2021/2022 walipanga kukusanya bil 26.5 lakini wakakusanya bil 22.2 sawa na asilimia 83.8.
Aidha kwa mwaka 2022/2023 lengo ilikuwa kukusanya sh bil 25.7 lakini wakakusanya bil 24.6 sawa na ufanisi wa asilimia 95.9 na kuanzia Julai 2023 hadi Februari 2024 walipanga kukusanya sh bil 12.3 kwa wateja wa kati pekee lakini wakakusanya bil 12.9 sawa na ufanisi wa asilimia 105.
Kanyilili alidokeza kuwa miaka 3 ya Rais Samia Suluhu Hassan kuanzia 2021/2022 hadi 2023/2024 imekuwa na ukuaji mzuri wa makusanyo ukilinganisha mwaka wa mbele na nyuma ambapo kiwango cha ukuaji kimeendelea kuongezeka.
More Stories
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari