Na Hamisi Miraji, Timesmajira Online
UNAPOZUNGUMZIA Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC), ni taasisi maalum ya Serikali inayohusika na masuala yote ya nishati ya atomiki katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Tume hiyo ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Na.7 yamwaka 2003 (The Atomic Energy Act. No.7 of 2003).
Awali ilikuwa ikijulikana kama Tume ya Taifa ya Mionzi (National Radiation Commission) iliyoanzishwa kwa Sheria ya Bunge Na.5 ya mwaka 1983 (The Protection from Radiation Act. No.5 of 1983).
TAEC ina majukumu mbalimbali miongoni mwa majukumu yake ni; Kudhibiti matumizi salama ya mionzi nchini, kuhamasisha na kuendeleza matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia.
Kufanya utafiti na kutoa ushauri na taarifa mbalimbali juu ya sayansi na teknolojia ya nyuklia
Hata hivyo TAEC ina kazi nyingi, baadhi ya kazi zake ni kukagua vituo vyote vyenye vyanzo vya mionzi ili kusimamia utekelezaji wa sheria ya Nguvu za Atomiki na kanuni zake.
Kutoa vibali vya uingizaji, umiliki, usafirishaji na utumiaji wa vyanzo vya mionzi.
Kupima sampuli za vyakula, mbolea, vyakula vya wanyama, tumbaku na mazao yake vinavyoingizwa na kusafirishwa nje ya nchi.
Kupima sampuli za mazingira ili kubaini uchafuzi wa mionzi kwenye mazingira. Kupima kiwango cha mionzi kwenye minara ya simu na rada za mawasiliano.
Kutoa huduma ya upimaji wa mionzi kwa wafanyakazi wanaofanyakazi kwenye maeneo yenye vifaa vya mionzi. Kuendesha kituo cha kupima uchafuzi wa anga (air pollution) unaotokana na majaribio ya silaha za nyuklia (Radionuclides Monitoring Station- RN64) nk.
Katika kipindi cha awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, TAEC imepata mafanikio mbalimbali ikiwemo ukusanyaji wa maduhuli ya serikali.
Akizungumzia mafanikio hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC), Prof. Lazaro Busagala amesema ukusanyaji wa maduhuli umeongezeka kutoka shilingi bilioni 8.7 kwa mwaka wa fedha 2020/2021 hadi kufikia shilingi bilioni 10.9 mwaka wa fedha 2022/2023.
Amesema, Mafanikio hayo yametokana na juhudi za Serikali ya awamu ya Sita kufungua ofisi za kanda, mipakani na kutumia mifumo ya TEHAMA kama vile TANCIS, TeSWS na EDMS katika kutoa
huduma.
Prof. Busagala amesema mafanikio mengine ni, Serikali imeendelea kusogeza huduma kwa wananchi kwa kujenga miundo mbinu inayoipa TAEC uwezo wa kutoa huduma kwa tija na ufanisi.
Amesema, Serikali imejenga majengo 6 ya maaabara na ofisi katika kanda 5 yenye thamani ya takribani Bilion 28.11 ambapo majengo 4 kati ya hayo yamekamilika.
Ameitaja Miradi hiyo ambayo ipo Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Mbeya, Mwanza na Zanzibar.
Amesema, Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea na jitihada za kuwasogezea wananchi huduma karibu na maeneo yao kwa kufungua ofisi. Katika miaka mitatu ofisi 14 zimefunguliwa na kuwekewa vitendea kazi, hivyo kuzifanya kuwa 63 mipakani, mikoani.
Lengo la kufanya hivyo ni kusogeza huduma kwa wananchi pamoja na kuinua shughuli za kiuchumi za wananchi.
Vilevile amesema, TAEC imeboresha mazingira ya kufanya biashara kwa ajili ya kupunguza siku za utoaji wa cheti cha uchunguzi wa mionzi (RAC) kutoka zaidi ya siku 7 hadi kufikia kwa wastani wa masaa 3 hadi siku moja kwa asilimia 98.
Awali utaratibu wa RAC ulikuwa una mlolongo mrefu ambao ulisababisha malalamiko mengi kutoka kwa wadau mbalimbali.
Lakini pia, amesema Serikali ya awamu ya sita imeondoa tozo na kupunguza tozo kwa kuamua kubeba gharama za upimaji (subsidy.
Hiyo kwa wale wanaosafirisha bidhaa nje ya nchi kwa kupunguza kutoka asilimia 0.2 ya malipwani kuwa asilimia 0.1 ya malipwani, sawa na punguzo la asilimia 50.
Aidha, amesema kwa wafanyabiashara wadogo hupatiwa huduma ya upimaji wa sampuli bure sawa na punguzo la asilimia 100.
Mafanikio mengine ambayo TAEC imefanikiwa katika kipindi cha awamu ya sita ni, Serikali imeboresha matumizi ya TEHAMA ambayo yamesaidia sana katika kufanikisha mambo mengi.
“Kuunganisha mifumo ya TAEC (EDMS), ifanye kazi kwa pamoja na ile mingine ya serikali mfano GePG, TANCIS, TeSWS yamekuza mawasiliano ndani na nje ya TAEC na kuleta matokeo chanya katika maeneo mbalimbali.
“Kuongeza idadi ya watumishi wa kudumu kutoka 89 hadi kufikia 142. Kwa kufanya hivyo, TAEC imeweza kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuwahudumia wananchi kwa uharaka zaidi.
“Kutatua matatizo ya watumishi wa TAEC kupandishwa vyeo baadhi ya watumishi lililodumu kwa muda mrefu. Watumishi 57 wa TAEC walikuwa na matatizo yaliyodumu kwa muda mrefu lakini Serikali ya awamu ya sita imeyatatua.
“Serikali ya Awamu Sita kupitia TAEC ipo katika hatua za mwisho kukamalisha mpango wa ufadhili kwa vijana wa kitanzania kusoma vyuo vya nje ya nchi masomo ya teknolojia na sayansi ya nyuklia katika ngazi ya shahada za uzamili.
“Lengo la ufadhili huu ni kuongeza idadi ya wataalam nchini katika nyanja ya teknolojia na sayansi ya nyuklia ili kuhakikisha kwamba nchi inanufaika ipasavyo na fursa za sayansi ya nyuklia.” amesema Prof. Busagala.
Mbali na hivyo, pia amesema Serikali ya Awamu ya Sita kupitia TAEC imewajengea uwezo wa kitaalam watumishi ili kujenga taifa lenye uwezo katika teknolojia ya nyuklia.
Amesema, kwa kufuata mpango wa mafunzo uliowekwa na kuanza kutekelezwa, TAEC imeshasomesha 29 na na inaendelea kusomesha wengine 32 ndani ya miaka mitatu. Jumla itakuwa watumishi 61.
“Hili ni muhimu sana kwa ustawi wa taifa letu katika sekta ya sayansi na teknolojia ya nyuklia,” amesema.
TRELA LA KUBEBA VYANZO VYA MIONZI
Serikali ya awamu ya sita kupitia TAEC, imebuni na kutengeneza trela maalum la kubebea vyanzo vya mionzi.
Akizungumzia hilo Prof. Busagala amesema, awali, watumishi na vyanzo vya mionzi walikuwa
wanakaa kwenye gari moja linalotenganishwa na vifaa ambavyo havizuii sawasawa mionzi.
Amesema, oambo hilo lilikuwa linahatarisha usalama wa watumishi wanao safirisha vyanzo vya mionzi, wananchi pamoja na mazingira kwa ujumla.
“Trela hili limesheheni vizuizi vya mionzi ili wanasafirishaji na wanchi wasiathirike na mionzi,” amesema Prof. Busagala.
Aidha, amesema Serikali ya Awamu ya Sita kupitia TAEC imeendelea na juhudi za kuhamasisha matumizi salama ya teknolojia ya nyukilia nchini.
Vilevile, amesema TAEC imefanya juhudi kubwa kuhakikisha wananchi wanaelewa fursa zilizopo katika matumizi salama ya sayansi ya nyuklia kwa ajili ya kujilitea maendeleo.
Lakini pia, imeongeza program za kujitangaza kutoka 12 hadi 60 kwenye TV, Redio, magazeti, mitandao ya kijamii na kushiriki katika maonesho mbalimbali.
KUBORESHA TAFITI ZA TEKNOLOJIA YA NYUKLIA
Serikali ya Awamu ya Sita imefanikiwa kuongeza tengeo la bajeti ya utafiti kwa TAEC hadi kufikia Tsh 450M katika mwaka wa fedha 2023/2024.
“Juhudi hizi zimefanyika ili kupata fursa zaidi za sayansi na teknolojia ya nyukilia na pia kuwalinda wananchi na mazingira dhidi ya madhara ya mionzi.
“Katika miaka mitatu machapisho 25 yakitafiti
yamepatikana katika juhudi hizi,” amesema Prof. Busagala.
AKkiendelea kuzungumzia mafaniko ya TAEC katika kipindi cha awamu ya sita, Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo amesema, Vifaa vya kisayansi ni nguzo muhimu katika kudhibiti athari za mionzi, tafiti, usimamizi na uendelezaji wa Teknolojia ya Nyuklia.
Hivyo Serikali ya Awamu ya Sita, inaendelea kuweka bajeti na kununua vifaa. Vifaa vya jumla ya TSh. 2.9 Billion vinaendelea kununuliwa.
Amesema, Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea na juhudi za kusimamia udhibiti wa matumizi salama ya mionzi ili kuepuka madhara yake.
Ameongeza, Hadi mwaka 2022/2023 jumla kaguzi 971 kwa mwaka zilifanyika ukilinganisha na kaguzi 244 kwa mwaka 2016/2017. Hilo ni ongezeko la asilimia 298. Kaguzi hizo ni nyingi kuliko viwango vya kimataifa.
Hata hivyo amesema, katika kudhibiti matumizi salama ya mionzi, Serikali ilifanikiwa kuongeza idadi ya wale wanaopewa lesseni kwa asilimia 102 yaani kutoka lesseni 297 kwa 2016/2017 hadi wastani wa 767 kwa mwaka.
Amesema, sababu kubwa ya matokeo hayo ni ongezeko la juhudi za udhibiti ikiwemo kufanya kaguzi za mara kwa mara, kufungua ofisi mbalimbali na kutumia mifumo ya TEHAMA.
Aidha amesema, katika utekelezaji wa Sheria ya Nguvu za Atomu Na. 7 ya 2003, Serikali imefanikiwa kusajili wataalam wa mionzi 788 wenye sifa za kutoa huduma ya mionzi kwa watu.
“Ndani ya miaka mitatu, Serikali imesajili wataalum 1,289 wa kutoa huduma ya mionzi kwa wagonjwa, kutengeneza, kukarabati na kuendesha vifaa vya nyuklia. Jambo hili lilikuwa halifanyiki kwa kipindi cha nyuma,” amesema.
MIPANGO YA TAEC ILIYOPO KWA SASA
Akizungumzia mipango iliyopo kwa sasa, Prof. Busagala amesema Kuendelea Kuwasogezea Wananchi Huduma kwa Kuimarisha Maabara za Kanda na maeneo mengine.
“Serikali itaendelea na juhudu za kujenga uwezo wa watumishi na kusimika vifaa na mitambo husika. Hii ni pamoja na kuendelea kumalizia ujenzi wa maabara na ofisi za kanda zilizo kwenye hatua mbalimbali.
“Ujenzi wa miundombinu unaiwezesha Serikali kusogeza huduma kwa wananchi hivyo kuwa kichocheo kwenye biashara, uchumi, shughuli za wananchi pamoja afya za wananchi na mazingira.
“Kukamilisha Mradi Kinunurisho Jumuishi ambacho kitatumika katika kuhifadhi mazao mbali mbali ikiwemo matunda, bidhaa za viwandani na mahospitalini (multipurpose irradiator) ili kuyapa thamani na kuongeza usafirishaji nje ya nchi.
“Hivi sasa upotevu wa mazao ya kilimo (post harvest loss) unakadiriwa kufikia hadi asilimia 60%. Pia mboga mboga na matunda huharibika kirahisi.
“Lakini pia, kukamilisha Mradi Kinunurisho Jumuishi. Kinunurishi Jumuishi kina faida zingine zikiwemo utafiti na utoaji wa elimu kwenye sayansi na teknolojia ya nyuklia,” amesema Prof. Busagala.
Aidha, amesema vifaa tiba na viwandani mbalimbali zinaweza kuvifanya salama (sterilization). Ujenzi wa miundo mbinu umekwisha kuanza.
Amesema Nchi yetu inakuwa ya 66 kati zile ambazo zinatumia teknolojia hii duniani.
Mipango mingine Prof. Busagala amesema ni, Kusimika Kinu cha Utafiti cha Nyuklia.
Amesema, kinu cha utafiti cha nyuklia (Nuclear Research Reactor) ni muhimu sana kwa ajili ya utafiti, kufundishia na kuweka mazingira ya kuwa na viwanda vya madawa ya kutibu saratani (radio-pharmaceautical industries).
“Vinu vingi vya nyuklia duniani vya namna hii hutumika kwa utafiti na mafunzo, majaribio ya ubora wa vifaa, au utengenezaji wa isotopu za dawa.
“Kwa sasa, vyuo vikuu hazina aina hii ya vinu na baadhi ya tafiti haziwezi kufanyika kwa sababu ya kutokuwa na kinu cha utafiti cha nyuklia,” amesema. kuendelea Kuboreshsa Udhibiti wa Matumizi Salama ya Mionzi na Miundombinu ya Teknolojia ya Nyuklia.
“Kuendelea kuweka na kuboresha kanuni na sheria ili kuwaweka watanzania salama zaidi dhidi ya madhara ya mionzi na teknolojia ya nyuklia.
“Kuongeza matumizi ya amani na salama kwenye
kilimo kama vile uboreshaji wa mbegu mbalimbali kwa kutumia teknolojia ya nyukilia (plant breeding).
Prof. Busagala ameipongeza sana Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mafaniko makubwa iliyopata katika Nyanja ya Teknolojia na Sayansi ya Nyuklia.
Maono na maelekezo ya Rais pamoja na Usimamizi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ya Nyukilia na Bodi ya TAEC yameiwezesha TAEC kutekeleza Sera ya Taifa ya Sayansi ya Nyuklia kikamilifu.
More Stories
Siri ya Rais Samia kutembea kifua mbelea kijivunia Mapinduzi Matukufu ya Z,bar
Rais Samia anavyotimiza ahadi yake ya kumtua ndoo ya maji mwanamke
Rais Samia anavyozidi kusogeza karibu watoto wa kike na kasi ukuaji teknolojia