November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

MIAKA 10 YA LSF:

Watu milioni 6.4 wapata msaada, elimu ya kisheria kutoka kwa Wasaidizi wa kisheria, RMOs

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online

SHIRIKA la Huduma za Sheria (LSF) linatimiza miaka 10 tangu kuanzishwa kwake.

Ni muongo mmoja ambao umewanufaisha mamilioni ya Watanzania hususani wanawake kwa kuwaongeza uelewa kuhusu masuala ya kisheria na kupata haki zao za kijamii na kiuchumi.

Katika kuhakikisha kuwa lengo kuu la LSF la upatikanaji wa haki kwa wote nchini linafikiwa, LSF ilianzisha mpango maalumu ambao kila raia ambaye alikuwa hapati huduma za msaada wa kisheria kwa urahisi, sasa anapata huduma hiyo na kufurahia haki yake ya msingi.

Ni dhahiri kwamba kimsingi wanawake na wasichana wako katika hali mbaya zaidi katika kupata haki zao ikilinganishwa na wanaume, lakini katika kushughulikia hilo na kuleta usawa, LSF ilianzisha mpango wake wa Upataji Haki ambao unawaweka wanawake na wasichana katika msingi imara wa kupata haki.

Ili kufikia malengo ya mpango huo wa haki kwa urahisi, LSF imewekeza kwa wasaidizi wa kisheria ambao wapo ndani ya jamii ili kuwawezesha wanawake na wasichana kupata huduma za msaada wa kisheria kwa bei nafuu na kwa urahisi zaidi.

Ili kuhakikisha utekelezaji wa mpango huo unafanyika kwa usahihi, LSF kwa kushirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria, Chama cha Wanasheria ya Tanganyika (TLS) na Shule ya Sheria ya Tanzania iliratibu mafunzo ya kuwandaa wasaidizi wa sheria zaidi ya 4,500 kwa Tanzania Bara na Zanzibar.

Katika kila wilaya, watu 25 ambao wanakidhi vigezo vya kiwango, pamoja na wananchi wengine waliandaliwa na kufundishwa kwa madhumuni ya kutoa huduma za msaada wa kisheria kwa hiari.

Wahitimu wa mafunzo hayo, walitakiwa kujipanga na kuanzisha shirika lisilokuwa na kiserikali wala la kibiashara ambalo limesajiliwa kikamilifu litakalofanya kazi katika ngazi ya wilaya.

Pia LSF ilianzisha mashirika yasiyo ya kiserikali yanayotoa ushauri wa kitaalam (RMOs), ambayo kazi yake kuu ilikuwa kusimamia na kuongoza kazi ya wasaidizi wa kisheria katika kila wilaya.

Kupitia usimamizi huo wa RMOs, LSF iliimarisha uwezo wa wasaidizi wa kisheria kupitia mafunzo kazini katika vipengele mbalimbali ikiwamo usimamizi wa fedha, utekelezaji wa programu, ufuatiliaji na tathmini, uhamasishaji na mawasiliano kwa madhumuni ili kuboresha utoaji wa huduma.

Umakini zaidi uliwekwa juu ya uimarishaji wa taasisi kuhakikisha miundo na mifumo iko sambamba na mashirika yote 183 ya kisheria ambayo yamesajiliwa kikamilifu na kufuata sheria na kanuni za NGOs.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa LSF, Lulu Ng’wanakilala

Kupitia ujuzi wa kisheria walioupata, wasaidizi hao wa kisheria wameendelea kutoa huduma za msaada wa kisheria chini ya udhamini wa mashirika yaliyosajiliwa kutoa huduma kwa watu wengi nchini ambao huduma za msaada wa kisheria hazikuwafikia.

Mashirika hayo ya RMOs yamefuatilia uhusiano wa wasaidizi wa kisheria na LSF katika miaka ya mwanzo tangu kuanzishwa kwake wakati wakitekeleza miradi ambayo ilichangia kwa ufanisi kutimiza malengo mapana ya LSF.
Malengo hayo yanalenga kuwepo kwa mazingira upatikanaji wa haki kwa kila mtu bila ubaguzi.

Uhusiano huu wa awali ulikuwa muhimu katika awamu ya pili ya Mpango wa Upataji Haki ambao ulianza mwaka 2016 na kumalizika mwaka 2020.

Pamoja na mambo mengine LSF ilishuhudia njia nyingi za ubunifu zilizoundwa na RMOs na kutekelezwa kwa ushirikiano na mashirika ya kisheria ili kupanua utoaji wa huduma za msaada wa kisheria.

“Jukumu letu linamaanisha kwamba lazima tufanye bidii zaidi kufikia malengo tunayoweka kwa shirika letu na mashirika ya kisheria yaliyo chini ya uangalizi wetu.

Katika mkoa mkubwa kama Shinyanga lazima kuzingatia viwango ambavyo LSF inatarajia kuvipata kutoka kwetu lakini pia tuna malengo yetu kama shirika ambayo tunahitaji kufanya kazi kwa bidii ili kutimiza.

“Kwa kifupi ni kwamba sehemu ya Mpango wa Upataji Haki ni fursa muhimu ya kutumia uwezo wetu”, anasema John Shija ambaye ni Meneja wa Programu katika Kituo cha Paralegal Shinyanga (PACESHI), RMO wa eneo hilo.

Jambo la kipekee zaidi la Mpango wa Upataji Haki ni kwamba huduma hizi muhimu zinapatikana bure na kwa zaidi ya miaka hii 10 wamefaidika wanawake, wanaume, wasichana na wavulana kwa sawa.

Kwa kuwa walengwa hawalipii huduma hizi za msaada wa kisheria, LSF imepanua mzunguko wake na kuruhusu Watanzania wengi haswa wale walio katika ngazi za chini za jamii zilizopo vijijini kuzipata huduma hizo kwa urahisi.

Takwimu za ripoti za 2016 hadi 2020 zinaonyesha kuwa ya watu waliofikiwa na msaada wa kisheria asilimi 56 walikuwa wanawake na asilimia 44 wanaume, wakati wale waliofikiwa kupitia msaada wa kisheria 55% walikuwa wanawake na asilimia 45 walikuwa wanaume.

Takwimu hizo zinaonyesha kuwa mpango huo unalenga zaidi kufikia wanawake pia wanaume hufikiwa na kufaidika nao.

Siri Liwawa ambaye ni Msaidizi wa Sheria na Paza Sauti Foundation (PASAFO) huko Rufiji, Pwani anasema; “Watu tunaowahudumia wale wa hali ya chini kabisa, ni wale ambao wamekosa fursa ya kufikiwa kwa urahisi na huduma hizo, hivyo tunawasaidia kupata haki zao bila kuwa na wasiwasi wowote kuhusu suala la upatikanaji wa pesa ili kupata huduma hizo za msaada wa kisheria.

“Tunafanya kazi katika jamii zetu kwa kujitolea licha ya changamoto nyingi tunafanya kila tuwezalo kuendelea kutoa huduma hizi muhimu”.

Ukweli huu unamaanisha kuwa wasaidizi wa kisheria ni miongoni mwa Watanzania waliojitolea zaidi haswa kwa kuzingatia hali zao moja kwa moja wanazokutana nazo katika kazi zao za kila siku.

Hutembea umbali mrefu kutoa huduma za msaada wa kisheria kwa walengwa walio katika mazingira magumu kwani jamii nyingine huona haki ya kupata huduma za kisheria ni hatari kwao ndio maana hujenga uhasama na hata kutoa vitisho kwa wasaidizi hawa wa kisheria.

Kama kaulimbiu ya LSF inavyosema kwa ufupi; “Haki kila siku kwa changamoto za kila siku.” Hii inaendana na malengo ya kila mshauri wa sheria anapoamka asubuhi na kuanza kutimiza majukumu yake.

Ukweli kwamba idadi kubwa ya Watanzania ambao hupatikana katika jamii za vijijini hawana fursa ya kupata haki ikilinganishwa na wenzao wa mijini ambao wanao uwanja wa kutosha wa kupata haki.

Changamoto kama vile migogoro ya ardhi, mivutano kuhusu urithi, unyanyasaji wa kijinsia, kutelekezwa kwa watoto, mimba za utotoni na ukeketaji wa wanawake ni sehemu kubwa ya kesi ambazo wasaidizi wa kisheria hushughulikia mara kwa mara.

Ripoti ya mwaka 2020 ya LSF inaonyesha kuwa zaidi ya watu milioni 6.4 walifikiwa kupitia elimu ya kisheria iliyotolewa na wasaidizi wa kisheria, wakati asilimia 68 ya kesi ambazo wasaidizi wa kisheria walihudhuria walisuluhishwa kwa mafanikio.

Meneja Mradi wa Kuboresha Huduma za Msaada wa Sheria Kupitia Wasaidizi wa Kisheria wa PACESHI, John Shija

“Tunashughulikia kila aina ya masuala ambayo jamii zetu zinakabiliana nayo ni sawa kusema kwamba huduma za kisheria tunazotoa zinawawezesha hata wale ambao mwanzoni waliamini kuwa hawana tumaini.

“Sisi ni sehemu ya jamii zetu na tuna jukumu la kuhakikisha haki inafurahiwa na kila mtu.

Ni muhimu kusema kwamba stadi nyingi tulizonazo na tunazotumia kila siku ni matokeo ya uboreshaji wa uwezo wa kawaida tunayopokea kutoka kwa shirika letu la washauri ambalo linajumuisha utekelezaji wa mradi, kuripoti, ufuatiliaji wa miradi na matokeo pamoja na usimamizi wa fedha ”, anaelezea Japhet Lazaro wa Kibondo Paralegal Foundation (KIPAFO) huko Kigoma.

Ili kusaidia na kuwezesha ufikiaji wa huduma za msaada wa kisheria, wasaidizi wa kisheria pia hutumia njia zilizopo za kuungana na watu katika wilaya zao na hii ni pamoja na mikutano ya hadhara, vikao vya shule na wanafunzi, hafla za umma kama bonanza, ziara za vituo vya afya ambapo idadi kubwa ya wanawake wanaweza kufikiwa ikiwa ni pamoja na vipindi vya redio vinavyoonyesha uelewa wa jumla wa sheria na vipindi vya maswali na majibu.

Programu ya Haki Yangu inayopatikana kwenye Smart phone, ilizinduliwa mwaka huu pia imetoa jukwaa la msaada wa kisheria kwa mtu yeyote mahali popote anapoweza kupata wasaidizi wa kisheria na kufaidika na elimu ya sheria au msaada wa kisheria.

Ni ukweli kwamba wakati mwingine wasaidizi wa kisheria hawawezi kutekeleza kazi za kisheria kama wanasheria au mawakili lakini RMOs kwa upande mwingine wanaweza kuwa na mawakili katika ofisi zao. Jambo hili limekuwa muhimu katika kuhakikisha kesi ambazo zinahitaji utatuzi wa kisheria zaidi ya wigo wa wasaidizi wa sheria zinarejeshwa kwa ofisi ya RMO.

Mpangilio huu kimsingi umeongeza imani ya wasaidizi wa sheria katika kushughulikia migogoro wakijua kwamba kwa vyovyote vile mnufaika atasaidiwa kwa urahisi katika kiwango cha juu wakati wowote atakapohitaji msaada wa kisheria.

Kwa kutambua michango ya RMOs na wasaidizi wa kisheria katika safari hii nzuri ya miaka 10, sio vibaya kusema kwa ujasiri kwamba Mpango wa Upataji Haki wa LSF unakuwa muhimu kila siku kwani watanzania wengi wamepata haki zao na kuzitumia kuboresha maisha yao.

Xxxxx