Na Ashura Kazinja, TimesMajira Online,Morogoro
MHITIMU wa shahada ya kwanza ya Uhandisi Umwangiliaji na Rasilimali Maji katika Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) mkoani Morogoro, Musa Dotto (23) amebuni gari shamba lenye uwezo wa kufanya kazi mbalimbali shambani ikiwemo usafiri.
Lengo la hatua yake hiyo ni kuwakomboa wakulima wadogo. Akizungumza na Majira mwishoni mwa wiki mkoani Morogoro, Musa amesema gari shamba hilo limetokana na wazo ambalo lilimjia kama suluhisho la ndani kwa wakulima wadogo.
Amesema gari shamba hilo lina uwezo wa kupukuchua mahindi kwa kutumia kinu chenye uwezo wa kupukuchua magunia 50 ya mahindi yenye magunzi kwa saa moja.
Amesema ameshaanza kubuni majembe ambayo ni rahisi kuvutwa na gari shamba hilo ili kuleta kuwapa urahisi wakulima na hatimate kutumia muda mfupi kwenye shughuli zao.
Ameongeza kuwa gari shamba hilo lina uwezo wa kutumika kupandia mazao kutokana na kuwa na mifumo ya upandaji yenye uwezo wa kupanda mistari minne kwa mazao ya punje kama vile mahindi, uwele, mtama.
“Gari hili lina uwezo wa kutumika kufyekea majani shambani, kuwekea mbolea ikiwemo ya maji na yabisi na kupuliza dawa kabla ya kuanza kupanda,” amesema Musa na kuongeza;
“Vitu ambavyo bado vinanikwamisha ni vifaa kwa ajili ya kutengenezea hii mashine yangu, nahitaji fedha kwa ajili ya kununua vifaa na malipo kwa wale nitakaoshirikiana nao, kwani hii ni ajira kama ajira nyingine,” amesema Musa.
“Kwa hapa ilipofikia hii trekta ndogo inafanya kazi kadhaa kama usafiri na kuvuta mizigo. Vifaa vingine bado havijakamilika tumekuwa tukijaribu tunavitoa, kwa kutumia gari shamba hili wakulima hadi wanne wanaweza kusafiri umbali hadi kilomita 50 kwa siku kwenda na kurudi kwa kutumia lita mbili za petroli sawa na sh. 4,000,” amesema Dotto.
Amesema kwa sasa wakulima wengi wanajikuta wakitumia nyenzo duni za kilimo kama vile jembe la mkono na wanyama kazi (mfano punda) kutokana na gharama kuwa kubwa za kumiliki na kuendesha mitambo mikubwa ya kilimo kama vile trekta, mashine za kupandia, kupulizia dawa, mashine za kupalilia na kuwekea mbolea shambani.
Alipoulizwa wazo la kutengeneza gari shamba hilo lilianzia wapi? Musa amesema; “Nilipoenda nyumbani nikakuta baba anatumia trekta ya zamani sana ambayo ilikuwa inamsumbua na inatumia gharama nyingi na kumsababishia hasara.
Nilijiuliza ni kwa nini hatuwezi kutumia mashine ambayo ni ndogo inayotumia vifaa ambavyo tunavyo ndani, ambavyo vikiharibika hata shambani tunaweza kuvitengeza, ndipo baba alinipa injini ya pikipiki mbovu, hapo ndio wazo likaanza, nikaanza kununua tairi na vifaa vingine.
Wazo hili liliniijia mwaka 2017 nilipokuwa kwenye mafunzo ya vitendo.”
Musa amesema pamoja na jitihada zake hizo za kufanikisha mradi huo, lakini pia anaiomba Serikali na sekta binafsi kumsaidia ili aweze kutimiza ndoto yake ya kumalizia gari shamba hilo, ambalo gharama za manunuzi litakapokamilika linaweza kufikia sh. milioni 12.
Kufuatia ubunifu huo uliofanywa na mhitimu huyo wa SUA, baadhi ya wanafunzi wenzake akiwemo Anna Sanga, Clementina Dismas na Madila Mkunda wamemuunga mkono na kuiomba Serikali na jamii kwa ujumla kumsaidia ili kuweza kufanikisha ndoto zake.
More Stories
CCM hakuna kulala, Nchimbi atua Tabora kwa ziara ya siku mbili
Kongamano la Uwekezaji na Biashara lafunguliwa Pwani
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi