📌 Awataka watumishi kufanya kazi kwa Bidii, Uadilifu na Maarifa
Na Mwandishi wetu,Timesmajira
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi, Hassan Saidy amesema Wananchi hususan wanaoishi vijijini wana matumaini na Serikali kupitia REA katika kuwaboreshea hali ya maisha na amewataka Watumishi wa Wakala kuhakikisha wanafanya kazi kwa bidii, uadilifu na maarifa ili kutimiza malengo ya Serikali kuhudumia wananchi wake.
Ametoa rai hiyo Machi 12, 2026 mkoani Morogoro wakati wa kufungua Kikao cha Tatu cha Baraza la Pili la Wafanyakazi wa REA lenye ajenda kuu ya Kupitia na Kujadili Mapato na Matumizi kwa Mwaka 2026/2027.
“Watumishi wenzangu mnafanya kazi nzuri, tuendelee kuhakikisha tunawatumikia wananchi, matumaini yao kwetu ni makubwa na leo hii tupo hapa kujadili Mapato na Matumizi katika kutekeleza na kukamilisha miradi na kwa bajeti ya REA imezingatia vipaumbele vya Serikali ikiwemo kuharakisha kupeleka umeme vitongojini, kuongeza idadi ya wateja na kutanua wigo upatikanaji wa Nishati Safi ya Kupikia,” amesema Mhandisi Saidy.

Amesema makadirio ya Mapato na Matumizi ya Bajeti kwa Mwaka 2026/2027 yanayojadiliwa katika Baraza hilo yamelenga kuboresha mazingira ya kazi na uwezo wa Taasisi katika kutekeleza majukumu yake sambamba na maslahi ya Watumishi.
Akizungumzia mafanikio yaliyofikiwa ndani ya kipindi cha miezi 12 (kutoka kikao cha Baraza kilichopita cha Mwezi Machi, 2025 hadi kikao cha sasa Machi, 2026), Mha. Saidy amesema REA imefanikiwa kusambaza umeme kwenye vitongoji 3,532 ambayo ni sawa na wastani wa vitongoji 10 kwa siku.

“Ndani ya kipindi cha miezi 12 tumefanikiwa kusambaza mitungi 400,000, majiko banifu 300,000, kujenga mifumo ya kisasa ya kupikia kwa Taasisi 452 zinazohudumia zaidi ya Watu 100, tumeanza kutekeleza Mradi wa kupeleka Umeme – Jua kwa kaya takriban 20,000 katika visiwa 143 na ndani ya kipindi hiki miradi takriban mitatu ya kusambaza ùmeme imekamilika,” amesema Mkurugenzi Mkuu wa REA.
Akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE), Hery Mkunda ameipongeza REA kwa kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi na uzalendo.

“REA mnafanya kazi kubwa sana, mmefanikisha azma ya Serikali ya kubadilisha na kuboresha maisha ya wananchi wa maeneo ya vijijini, kwa hili kila mwananchi anaetoka kijijini ni shahidi,” amepongeza Mkunda.
Kikao cha Tatu cha Baraza la Pili la Wafanyakazi wa REA kilihudhuriwa na Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Wilson Nyamanga, Mwakilishi wa Msajili wa HAZINA, Gerald Nzalalila pamoja na Katibu Mkuu wa TUGHE mkoa wa Dodoma, Samwel Nyangwa ambao walipata fursa ya kuzungumza na Watumishi.

More Stories
Rais Samia na Afisa Mtendaji Mkuu ABF Sugar kuendeleza uwekezaji sekta ya sukari
Tafiti nne NBS kuboresha mazingira ya biashara,uwekezaji
Msichana Initiative yazindua mradi wa Renewed Women Voices and Leadership Tanzania