November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mhandisi Mahundi wazazi na walezi tengeni muda kuwakagua watoto wa kiume

Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya

WAZAZI na walezi wametakiwa kuwakagua watoto wa kiume badala ya kuelekeza nguvu kwa watoto wa kike pekee ili kuzuia vitendo vya ukatili dhidi yao ikiwemo ubakaji na ulawiti ambavyo vimekuwa vikifanyika katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Kauli hiyo imetolewa Septemba 20,2024 na Naibu Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mbeya na Mkurugenzi wa Taasisi ya Maryprisca Women Empowerment Foundation(MWEF) Mhandisi Maryprisca Mahundi wakati wa mahafali ya shule ya msingi Ilemi iliyopo Kata ya Iganzo Jijini Mbeya .

Mhandisi Mahundi amesema kuwa katika malezi ya watoto wazazi wanatakiwa kutenga muda maalum wa kuwakagua watoto wa kiume na sio kuelekeza nguvu kwa watoto wa kike pekee hivi sasa hali ni mbaya kwa watoto wetu tusiwaache tu bila kuwachunguza kwa kudhani wapo Salama.

“Watoto wote wanahitaji uangalizi wa karibu. Vitendo vya ukatili vimekuwa vingi kwa watoto wetu tutoe muda wetu kukagua usalama wa watoto wa kiume ndugu zangu”amesema Mhandisi Mahundi.

Aidha Naibu Waziri huyo katika mahafali hayo ametoa msaada wa computer mbili na magodoro matatu kwa watoto wenye uhitaji katika Shule hiyo.

Amesema computer hiyo itakuwa msaada kwa shule katika kuandaa ripoti ripoti mbalimbali za Shule na utunzaji kumbukumbu sambasamba na magodoro hayo kwa watoto wenye uhitaji maalum waliopo shuleni hapo pamoja na kuahidi kutoa vitimwendo saba kwa watoto wenye ulemavu.

Awali watoto hao wameelezea dhima nzima ya ukatili wanaofanyiwa watoto wa kiume kwa njia ya shairi.

Diwani wa Kata ya Iganzo Daniel Mwanjoka amemshukuru Naibu Waziri kwa msaada huo mkubwa ambao utakuwa mkombozi kwa shule huku akiomba wadau wengine kujitokeza kusaidia vitu mbali mbali hususani kwa watoto wenye uhitaji.

Sophia Malingumu ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Ilemi anaeleza changamoto mbalimbali zinazowakabili wanafunzi katika shule hiyo ikiwemo watoto wenye uhitaji kukosa mahitaji muhimu ya kujifunzia vikiwemo vitu mwendo ambavyo ni nyezo muhimu kwa watoto hao.

Mwalimu Scolah Daud na Justin Mwamba Mwenyekiti wa Mtaa wa Nkuyu Kata ya Iganzo wametoa neno la shukurani na kuhaidi kutunza vifaa vilivyotolewa na Naibu Waziri .

Hata hivyo wameomba wadau kujitokeza kusaidia shule hiyo ili iweze kupiga hatua zaidi kitaaluma.