September 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mhagama :Baraza la Madaktari jipangeni kuendana na kasi ya mabadiliko ya Sekta ya Afya

Na Mwandishi wetu ,Timesmajira

Waziri wa Afya Jenister Mhagama amelitaka Baraza la Madaktari Tanganyika kujipanga zaidi ili kuendana na kasi ya mabadiliko makubwa ndani ya Sekta ya Afya yanayotokea na uongozi mahiri wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Waziri Mhagama ametoa wito huo jana Septemba 05, 2024 kwenye kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI ikiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Elibariki Kingu kwenye kumbi za Bunge Jijini Dodoma.

“Sekta ya Afya imekuwa sana, na hivi sasa kuna Ultrasound ya Jicho kitu ambazo zamani hakikuwepo na ukipata tatizo unatakiwa uende India, hivyo wanataaluma wanatakiwa waendele kujifunza hususani kwenye matumizi ya vifaa na kukakikisha huduma hizi zinawafikia wananchi wote hasa wa vijijini”amesema Waziri Mhagama

Kwa upande wake Msajili wa Baraza la Madaktari Tanganyika Dkt. David Mnzava, amesema mpaka sasa baraza limefanikiwa kuwasajili wanataaluma Zaidi ya 9,983 kwa kipindi cha mwaka Mmoja pekee.

“Hadi Juni 30,2024 Jumla ya wanataalamu 9,983 wamesajiliwa kufikia idadi ya wataalamu 41,937 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 31,”amesema Dkt. Mnzava

Dkt. Mnzava amesema ongezeko hilo litakwenda kuongeza utoaji wa huduma bora kwa wananchi.