December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mha.Kundo:Miradi ya maji itatekelezwa kwa asilimia 100

Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Tanga

NAIBU Waziri wa Maji Mhandisi Kundo Mathew amekihakikishia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa Ilani ya CCM 2020-2025 itatekelezwa kwa asilimia 100 kwa wananchi wa vijijini kupata maji kwa asilimia 85 na wa mijini kwa asilimia 95.

Akizungumza Juni 22, 2024 mbele ya viongozi wa CCM akiwemo Katibu wa CCM Mkoa wa Tanga Selemani Sankwa ambapo alifika kwenye Ofisi za CCM za mkoa ikiwa ni kujitambulisha ili kuanza ziara ya siku mbili mkoani humo amesema hadi sasa upatikanaji wa maji kwa vijijini ni asilimia 79.6, huku kwa mijini ni asilimia 91.

Mhandisi Mathew amesema Rais wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan akiwa Makamu wa Rais alitoa kauli ya kuitaka Wizara ya Maji kumtua mwanamke ndoo kichwani na kauli hiyo ameirudia alipokuwa Rais, hivyo wao kama Wizara ya Maji hawana budi kutimiza ndoto ya Rais Dkt.Samia.

“Kitabu chetu cha kurasa 303 (Ilani ya Uchaguzi 2020- 2025) kimetuelekeza nini cha kufanya,nini tukifanye ndani ya miji yetu mikubwa kufikisha huduma ya maji kwa asilimia 95 lakini vile vile vijijini tufikie asilimia 85,hii dhana ya kumtua mama ndoo kichwani iliasisiwa na Makamu wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na sasa yeye ni Rais, na dhana hii bado tunaendelea nayo.

“Msukumo wake wa kumtua mama ndoo kichwani ni kuhakikisha badala ya mama kutembea kilomita nyingi kutafuta maji, basi tunamsogezea karibu na nyumbani kwake na hiyo ndiyo maana halisi ya kumtua mama ndoo kichwani.

“Lakini msukumo wake wa kuhakikisha mama anatuliwa ndoo kichwani, ulifanya kubadilishwa kwa sheria na kuanzisha Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijiji, RUWASA,”amesema Mhandisi Mathew.

Mhandisi Mathew amesema kabla ya RUWASA, kulikuwa na Idara ya Maji chini ya Mkurugenzi wa Halmashauri ambapo utendaji wake ulikuwa hauna ufanisi kwani fedha za miradi zilikuwa hazijulikani zilikokwenda hata Jumaa Aweso akiwa Naibu Waziri wa Maji (sasa Waziri wa Maji), alizunguka nchi nzima na kukutana na ‘madudu’ kwenye miradi ya maji huku miradi mingi ikiwa imesimama lakini fedha zimetumika na kumalizika.

“Mnakumbuka tulikuwa na Idara ya Maji chini ya Mkurugenzi wa Halmashauri, Miradi ilikuwa inaingilia huku inatokea huku, fedha ilikuwa inaingilia huku inatokea huku,Sote tunakumbuka, ukitambulishwa unatoka Idara ya Maji ulikuwa unaonekana ni kichefuchefu, Ulikuwa unaonekana ni wale wale watafunaji wa pesa za Watanzania.

“Lakini katika kipindi hicho hicho Rais Dkt. Samia akiwa ni Makamu wa Rais,Jumaa Aweso Mbunge wa Pangani akiwa Naibu Waziri wa Maji, alitembea nchi nzima na kujionea miradi 177 ikiwa imekwama kabisa,huku wizarani fedha zikionekana zimetoka zimekwenda halmashauri lakini ukienda halmashauri fedha hizo hazipo, Unaoneshwa tenki lile pale limejengwa lakini maji hayatoki,Siku ya kuzindua mnakwenda na mbwembwe zote, mkitoka pale, maji hakuna ilikuwa ni kichefuchefu” amesema Mhandisi Mathew.

Mhandisi Mathew amesema ili kuonesha namna Serikali ilivyojisahihisha na kuanzisha RUWASA ambayo imeleta mageuzi makubwa katika kuwapatia maji wananchi wa mijini na vijijini.

“Kwa nini nayasema hayo, miradi 77 iliyokuwa imekwama ambayo Jumaa Aweso aliigundua huko, na miradi mingine ambayo ilikuwa haitoi maji, sasa miradi 164 kati ya ile miradi 177, yote imekwamuliwa na inatoa maji safi na salama,haya yote ni maelekezo ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi.

“Lakini vile vile tangu kuanzishwa kwa RUWASA (2019) tulikuwa na vijiji 4,326 vyenye maji,leo naongea hapa na kuna uwezekano vimeongezeka lakini kwa taarifa niliyonayo hadi naamka asubuhi ya leo vijiji 9,737 kati ya vijiji 12,318 nchini tayari vina maji safi na salama sawa sawa na asilimia 79.6 kuelekea kwenye 85 tuna sogea sogea.

“Mtu anaweza kujiuliza tutafikaje kwenye asilimia 85, tuna miradi mingi inayoendelea ambayo haijakamilka, na Serikali inataka tukamilishe iliyopo badala ya kuanzisha mipya” amesema Mhandisi Mathew.

Naye Katibu wa CCM Mkoa wa Tanga, Sankwa, amesema ukiacha changamoto ndogo ndogo zilizopo kwenye Sekta ya Maji kwenye mkoa huo bado miradi iliyopo inakwenda vizuri na wananchi wengi wanapata maji na kukitokea jambo hawana haja ya kuueleza uongozi wa juu bali wanaitana wenyewe kwa wenyewe ndani ya mkoa na kurekebisha.

“Naibu Waziri nikuthibitishie sisi pamoja na watendaji wa Idara ya Maji kwenye mkoa huu tunafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na wenzetu kukiwa na changamoto tunaitana tunaelezana,tunashauriana, tunaelekezana, na tunahakikisha wananchi wetu wa Mkoa wa Tanga wanapata huduma ya maji” amesema Sankwa.

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya kikao cha Naibu Waziri na watendaji wa Sekta ya Maji Mkoa wa Tanga, Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo, amesema kuna miradi 75 inaendelea kwenye mkoa huo kati ya hiyo miradi 35 itakamilika Desemba mwaka huu na huduma ya maji kwenye mkoa huo inatarajia kupanda kutoka asilimia 65 hadi 75 ifikapo Desemba mwaka huu.

“Mkakati mkubwa wa Serikali ni kutekeleza Mradi wa Maji wa Miji 28 ambao unapita kwenye miji ya Korogwe, Handeni, Muheza na Pangani,lakini pia kuna mradi wa Wilaya ya Kilindi na ule wa Horohoro, Wilaya ya Mkinga,leo tunakaa kikao na Naibu Waziri pamoja na Wakandarasi ili kuweka mikakati ya pamoja na tunamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi” amesema Mhandisi Lugongo.