December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mgumba aahidi barabara ya Handeni- Turiani kujengwa

Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online, Kilindi

MKUU wa Mkoa wa Tanga Omar Mgumba amewahakikishia wananchi wa Kata ya Negero katika Wilaya ya Kilindi kuwa barabara ya kutoka Handeni- Negero- Mziha- Turiani mkoani Morogoro yenye urefu wa kilomita 128, itajengwa kwa kiwango cha lami.

Akizungumza na wananchi mwishoni mwa wiki Oktoba 28, 2022 kwenye Kata ya Negero, ambapo alikuwa anajibu hoja za wananchi waliouliza maswali, Mgumba alisema barabara hiyo ya kuunganisha mkoa na mkoa, ipo kwenye mipango ya Serikali, na imeanza kujengwa kwa vipande vipande.

Mgumba alisema Serikali inajenga barabara kwa viwango vya lami kwa vipaumbele kulingana na rasilimali fedha, na miradi iliyopo wakati huo, hivyo Serikali kwa sasa inajenga miradi ya kitaifa kama Mradi wa kufua umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) na Daraja la Kigongo- Busisi kule Mwanza.

“Wananchi, napenda kuwahakikishia, barabara ya Handeni- Negero- Mziha hadi Turiani, itajengwa. Barabara hii tayari ujenzi wake umeshaanza kwa kujengwa vipande vipande. Barabara hii inaanzia Korogwe- Handeni- Degero- Mziha- Dumila- Kilosa hadi Mikumi. Na tayari kipande cha kutoka Korogwe- Handeni (kilomita 65), kipande cha Dumila- Kilosa (kilomita 65), na kile cha Turiani hadi Dumila vimeshajengwa.”

“Serikali inajenga miundombinu mbalimbali kutoka na vipaumbele na rasilimali fedha. Kwa sasa Serikali inajenga miradi ya kitaifa ya Mradi wa Umeme wa Mwalimu Nyerere na Reli ya SGR.

Ikimaliza itarudi kujenga barabara za kuunganisha Taifa, na barabara za kuunganisha mkoa kwa mkoa kama hii ya kutoka Handeni mkoani Tanga, hadi Turiani mkoani Morogoro” alisema Mgumba.

Awali, mwananchi wa Kijiji cha Negero, Hezron Kinasa alitaka kujua, ni vipi kipande cha barabara cha kutoka Handeni- Negero- Turiani ujenzi wake haujaanza, wakati kutoka Turiani- Dumila- Kilosa tayari ujenzi wake umekamilka, huku akidai kwa kutopata barabara ya kiwango cha lami, mazao yao wanauza kwa bei ya chini.Katika ziara hiyo, Mgumba alitembelea Shule ya Sekondari Vyadigwa.

Shule hiyo ambayo ni ya pili kwenye Kata ya Kimbe, hadi kufikia kupauliwa, imejengwa kwa nguvu za wananchi, hivyo baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kupata taarifa ya juhudi za wananchi wa Kijiji cha Vyadigwa, Kata ya Kimbe kujenga shule nyingine ya sekondari, kama Mama, amewapa sh. milioni mbili ili kuwaongezea nguvu.

“Napenda kuwapongeza wananchi wa Kata ya Kimbe kwa kujenga shule ya pili ya sekondari kwa nguvu zao wenyewe. Wananchi mmeweza kujenga vyumba vinne (4) vya madarasa, ambapo kama Serikali ingeamua kutoa fedha, basi ingekuwa ni sh. milioni 80. Kwa kuona juhudi zetu, Rais Samia Suluhu, kama Mama, ameamua kutoa sh. milioni mbili ili kuwaunga mkono” alisema Mgumba.

Mgumba alisema, kuna haja ya viongozi wengine kwenye halmashauri za Mkoa wa Tanga kwenda Kilindi kujifunza matumizi sahihi ya fedha, hasa kwenye ujenzi wa miradi ya maendeleo, kwani pia, Kata ya Bokwa imeweza kujenga vyumba sita vya madarasa Shule ya Msingi Nkama kwa sh. milioni 60.

Kwani vyumba vitatu ilikuwa ni vipya, na vyumba vingine vitatu walikuwa wanakamilisha baada ya wananchi kujenga maboma.

“Napenda kutoa wito kwa halmashauri nyingine kwenye Mkoa wa Tanga (Tanga ina halmashauri 11) na Taifa kwa ujumla kuja kujifunza Kata ya Bokwa namna walivyoweza kujenga vyumba vipya vitatu vya madarasa, na vingine vitatu kukamilisha ujenzi wake kwa sh. milioni 60, na kubaki sh. milioni tatu. Haya ni maajabu ya dunia.”

“Kuna baadhi ya halmashauri huwa wanasema sh. milioni 20 hazitoshi kujenga darasa, wanataka wapewe sh. milioni 30 mpaka sh. milioni 35, lakini kwenye Kata ya Bokwa wameweza kukamilisha ujenzi huo, tena na kuweka mpaka madawati” alisema Mgumba.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Diwani wa Kata ya Bokwa, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi Idrissa Mgaza, alisema ni kweli, wananchi wa Kijiji cha Nkama walijitolea kwa nguvu zao kuona wanachangia ujenzi wa shule yao.”Awali, wananchi wa Kijiji cha Nkama walijenga vyumba vitatu vya madarasa na kufikia hatua ya maboma.

Serikali ilipotoa sh. milioni 60, wananchi wakachangia tena nguvu zao, hivyo kuweza kupata vyumba sita vya madarasa, na kununua madawati 70, sh. milioni tatu zilizobaki tumepeleka kwenye ujenzi wa vyoo.” alisema Mgaza.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Omar Mgumba (katikati) akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kwaluguru, Kata ya Negero, Wilaya ya Kilindi mara baada ya kuwasili wilayani humo Oktoba 28, 2022 kufanya ziara ya siku mbili. (Picha na Yusuph Mussa).
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Omar Mgumba (kulia) akipata maelezo kutoka kwa Mkuu wa Idara ya Ujenzi, Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi, Mhandisi Frank Miala (kushoto). Ni baada ya kutembelea boma la Zahanati ya Kijiji cha Kwaluguru, Kata ya Negero Oktoba 28, 2022, ambapo wananchi walijenga kwa nguvu zao hadi usawa wa boma miaka zaidi ya 10 iliyopita, lakini mpaka sasa haijakamilika. Mgumba ameahidi kuitafutia fedha ili kukamilisha. (Picha na Yusuph Mussa).
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Omar Mgumba (kushoto) akipata maelezo kutoka kwa Diwani wa Kata ya Kimbe, Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi Shaaban Nkelemy (kulia), mara baada ya kufika Oktoba 28, 2022 kuangalia ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari Vyadigwa ambapo hadi hatua hiyo ya upauaji wa vyumba vinne (4) vya madarasa, zimetumika nguvu za wananchi pekee, hivyo Rais Samia Suluhu Hassan, kama Mama, amewapa sh. milioni mbili kuongeza nguvu. Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Kilindi Abel Busalama. (Picha na Yusuph Mussa).
Wananchi wa Kijiji cha Vyadigwa, Kata ya Kimbe, Wilaya ya Kilindi wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Tanga Omar Mgumba (hayupo pichani) alipofika kijijini hapo Oktoba 28, 2022 kukagua miradi ya maendeleo na kuzungumza na wananchi. (Picha na Yusuph Mussa).
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Omar Mgumba (wa pili kulia) akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kwaluguru, Kata ya Negero, Wilaya ya Kilindi mara baada ya kuwasili wilayani humo Oktoba 28, 2022 kufanya ziara ya siku mbili. (Picha na Yusuph Mussa).