Na Ester Macha,TimesmajiraOnline,Chunya
MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Lupa, Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya,Masache Kasaka, ameomba Serikali kuharakisha zoezi la kupeleka nishati ya umeme katika maeneo ya wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu, hasa katika Kata ya Kiwanja, ili kuongeza tija katika shughuli za uzalishaji.
Hayo yamesemwa Oktoba 22, 2025, wakati Mbunge Masache akitoa salamu kwa wananchi kwa Mgombea mwenza wa Urais wa CCM, Emmanuel Nchimbi, huku akielezea mafanikio yaliyopatikana kupitia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020–2025.
Nchimbi alifanya mkutano huo wa hadhara akiwa katika ziara ya kampeni, ambapo alitumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi kumpigia kura Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na mgombea ubunge wa jimbo hilo, Masache Kasaka.

Masache amebainisha kuwa licha ya mafanikio makubwa yaliyopatikana chini ya Serikali ya Awamu ya Sita, bado kuna haja ya Serikali kuangalia upya maeneo ya uchimbaji ambayo hayajaendelezwa na kuyarejesha ili yatolewe kwa wachimbaji wadogo kwa utaratibu maalumu.
Amesisitiza kuwa kukosekana kwa nishati ya umeme katika maeneo ya uchimbaji kunapunguza ufanisi wa uzalishaji na kipato cha wachimbaji wadogo, ambao wengi wao wanategemea shughuli hizo kujikimu kimaisha.
Aidha, Masache amepongeza Serikali kwa juhudi zake katika kukuza sekta ya madini, hatua ambayo imechangia kupanda kwa bei ya dhahabu kufikia Sh300,000 kwa gramu moja, jambo alilosema limeongeza mapato ya Serikali na kuboresha maisha ya wananchi.


More Stories
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi
Waziri Mkuu kuanza ziara mkoani Rukwa Marchi 8 Hadi 10
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani