January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mgogoro wa ardhi kati ya ASA na wananchi wamalizika

Na Moses Ng’wat,Timesmajiraonline,Mbozi.

MKUU wa Mkoa wa Songwe, Dkt. Francis Michael, amefanya mkutano wa hadhara na wakazi wa vijiji vinne vya Tarafa za Igamba na Itaka, Wilayani Mbozi na kumaliza mgogoro wa ardhi kati ya wakazi hao na Wakala wa mbegu za kilimo (ASA) kwa kuagiza wananchi hao kupatiwa ekari 500 kwa ajili ya shughuli za kilimo.

Ametoa uamuzi huo Novemba 16, 2023 katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo la mgogoro katika kijiji cha Magamba, Wilayani Mbozi, ambapo wananchi kutoka vijiji vinne walifika kumsikiliza Mkuu huyo wa Mkoa.

Hata hivyo, baada ya kufanya uamuzi huo, Mkuu wa Mkoa amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mbozi, Abdalla Nandonde kwa kushirikiana na maofisa ardhi kwenda kulihakiki eneo hilo na kulipima ukubwa wake na kisha kuligawa katika vijiji hivyo vinne.

“Wenyeviti wa serikali za vijiji maeneo haya si yakukodisha Kwani baada ya kupimwa na kuingizwa kwenye kijiji wananchi wanapaswa kuendelea kuayatumia kama walivyokuwa wakiyatumia hapo awali”.

Dkt. Michael amesema baada ya wataalam wa ardhi kumaliza kulihakiki na kulipima eneo hilo, kila kijiji kitapatiwa ekari 125 ambazo zitajumuishwa kwenye eneo la kijiji ili waananchi waendelee kulitumia kwa ajili ya shughuli za kilimo bila kubughudhiwa.

“Mkurugenzi Mtendaji hakilisha kesho unaleta watu wako kwa kushirikiana na maofisa ardhi mje mlipime eneo lote kwa kushirikiana na viongozi wa serikali za vijiji ili kupata suluhisho la kudumu na tutoe nafasi kwa wananchi kuendelea na shughuli za kilimo Kwani tayari mvua zimeshaanza,”amesema Dkt.Michael.

Wananchi hao wanadaiwa kuvamia eneo hilo na kujimegea kipande cha ekari 250 kati ya ekari 1586.5 na kuanza kulitumia kwa ajili ya shughuli za kilimo.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa Dkt. Michael amemuagiza Kaimu ofisa Tarafa ya Itaka, Emmanuel Hankungwe kwa kushirikiana na wenyeviti wa vijiji vinne vya Hangomba, Magamba, Itewe na Iporoto kuhakikisha wanawaondoa watu wote waliovamia hifadhi ya msitu wa Ludewa unaomilikiwa na Wakala wa mbegu za kilimo (ASA) na kufanya uharifu mkubwa kwa kukata miti hovyo, ikiwemo kuanzisha makazi ya kudumu.