Na Mwandishi wetu, Timesmajira
🔺· *Ni katika maduhuli ya Serikali*
· 🔺*Kahama yafikia 85% ya ukusanyaji maduhuli*
Na Mwandishi wetu, Timesmajira
MGODI wa Dhahabu wa Manda, unaomilikiwa na Wakinamama chini ya uenyekiti wa Asha Msangi umechangia Shilingi Milioni 800 katika maduhuli ya Serikali kwa mwaka huu wa fedha 2024/2025.
Mgodi huo ambao kwa kiasi kikubwa unaendeshwa na wakinamama upo Kahama Kijiji cha Mwime Kata ya Zongamela ambao una leseni ya uchimbaji mdogo wa madini na umeajiri zaidi ya vijana 200.
Akizungumza katika mahojiano mmiliki wa mgodi huo ambae pia ni Mwenyekiti wa wanawake wachimbaji mgodini hapo, Asha Msangi anasema “Kabla ya kuanza kwa shughuli za uchimbaji wa madini nilikuwa nafanya biashara ndogo ndogo, nilikuwa na kiduka kidogo tu, badae nikahamia kwenye mazao nikawa napeleka mchele Arusha hata hivyo biashara ilikuwa ngumu, nikahamia kwenye uchimbaji.
“Nilikuwa nachimba kwenye migodi ya watu, nikapata uzoefu nikaomba leseni nikapewa moja kama majaribio lakini nashukuru nilifanya vizuri na nikaaminika sasa hivi namiliki leseni 12, nimeunda na vikundi vya kinamama ambao nashirikiana nao kuchimba, ”amesema Asha.
Kwa upande wa Afisa Madini Mkazi wa Kahama, Leons Welengeile amesema mgodi huo wa Manda ni wadau muhimu na unatoa ajira kwa vijana na kinamama wengi kupitia shughuli zinazoendelea katika mgodi huo.

“Kwa mwaka huu wa fedha 2024/2025 kuanzia mwezi Julai 2024 hadi Februari 2025 mgodi huu wa Manda umechangia Shilingi Milioni 810 katika maduhuli ya Serikali na hiyo ni kupitia mrabaha na tozo ya ukaguzi ambazo zinakusanywa na Tume ya Madini Kahama, achilia mbali makusanyo mengine yaliyokusanywa na halmashauri na TRA,”amesema Leons na kuongeza,
“Kwa hiyo tuwaamini wakina mama, hivyo tunaendelea kufungua fursa kwao,”amesisitiza.
Aidha, Leons amesema maduhuli ya Serikali katika Mkoa wa Kimadini Kahama yameendelea kupanda mwaka hadi mwaka kutoka ukusanyaji wa Shilingi Bilioni 97 mwaka 2022/2023, Shilingi Bilioni 101 mwaka 2023/2024 na kwa mwaka 2024/2025 hadi mwezi Machi 2025 kiasi cha Shilingi Bilioni 88.08 kimekusanywa ikiwa ni sawa na asilimia 85 ya makusanyo ya Miezi 9,”amesema.

Amesema anaamini kwa mwelekeo unavyokwenda mpaka kufikia mwishoni mwa mwaka wataweza kutimiza lengo la makusanyo kama ilivyokusudiwa.
More Stories
COSOTA yasuluhisha migogoro 118 katika kipindi cha miaka minne
NMB yawapa tabasamu wanafunzi wa kike Sekondari ya Usongwe
MUWSA yatekeleza agizo la Rais Samia, yafunga mita za maji za ‘Prepaid’ 460