Na Joyce Kasiki,timesmajira online,Dodoma
OFISI ya Taifa ya Takwimu (NBS) imesema mfumko wa bei wa Taifa wa Agosti, mwaka huu, umesalia kuwa asilimia 3.3 kama ilivyokuwa mwezi Julai mwaka huu.
Akizungumza leo na waandishi wa habari katika ofisi za NBS Kaimu Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii Ruth Minja amesema,hiyo inamaanisha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia Agosti mwaka huu kuwa sawa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia mwezi Julai mwaka huu.
Aidha amesema,hali hiyo imechangiwa na kupungua na kuongezeka kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula kwa kipindi kilichoishia Agosti, mwaka huu, zikilinganishwa na bei za mwezi Agosti mwaka jana.
“Mfano baadhi ya bidhaa hizo za vyakula zilizopungua bei Agosti ikilinganisha na Agosti mwaka jana ni pamoja na mahindi kwa asilimia 5.8 unga wa ngano kwa asilimia 1.1 ,mihogo 16.3 na viazi vitamu kwa asilimia 11.9” amesema Minja.
Aidha Minja amesema kwa upande mwingine baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula zilizoongezeka bei Kwa Agosti mwaka huu zikilinganishwa na Agosti mwaka jana ni pamoja na mavazi kwa asilimia 2.2 ada za shule za msingi na sekondari za binafsi kwa asilimia 2.4 na huduma za malazi kwenye nyumba za wageni kwa asilimia 2.8.
Kwa mujibu wa Minja mfumko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioishia Agosti mwaka huu umepungua kwa asilimia 3.7 kutoka asilimia 3.8 kwa mwaka ulioishia Julai mwaka huu.
Kwa upande wa nchi za Afrika Mashariki amesema,nchini Kenya mfumko wa bei katika kipindi hicho pia umebaki kuwa asilimia 4.36 kama ilivyokuwa kwa mwaka ulioishia mwezi Julai mwaka huu.
Kwa upande wa nchi ya Uganda mfumko wa bei katika kipindi hicho umepungua hadi asilimia 4.6 kutoka 4.7 kwa mwaka ulioishia Julai mwaka huu.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua