January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mfanyabiashara asaidia wenye ulemavu, aahidi neema zaidi

Na Agnes Alcardo, TimesMajira Online, Dar Es Salaam

MKURUGENZI Mtendaji wa Kampuni ya KC, Chris Lukosi, maarufu kama “Madungu Jeshi”, Jana alitoa msaada wa Viti Mwendo 18, kwa watu wenye ulemavu, ikiwa kama sehemu ya shukrani na kurudisha kwa Jamii.

Akikabidhi msaada huo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, kwa walemavu 18, katika Mtaa wa SalaSala, Kata ya Wazo jijini Dar es Salaam jana,  Chalamila alimpongeza Lukosi kwa kutambua umuhimu wa watu wenye ulemavu na uhitaji.

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari, Chalamila alisema, “Lukosi ni mtu mwenye moyo wa upendo na ni vyema na wengine wakaiga nyendo zake na kuikumbuka Jamii yenye uhitaji”.

Aidha Chalamila ameeleza kuwa alifuatwa na walemavu watano ofisini kwake wakieleza mahitaji yao ili kuendesha maiasha yao na kutimiza majukumu yao ya kila siku

“Kati ya mahitaji muhimu waliyoorodhesha ni pamoja na wheel chair ndipo niliona kwa kuwa sina uwezo huo nikamtafuta kaka yangu Lukosi na kumuomba msaada wa wheel chair tano, alisema Mkuu wa Mkoa.

Chalamila alisema baada ya kumuomba, Lukosi msaada wa viti mwendo hivyo, alimweleza kuwa akitoa viti vitano havitatosha, hivyo ananza na hizi chache zilizopo hapa.

“Alinieleza kuwa jumamosi anasafiri ataongeza vingine  atakaporudi na kuanzia sasa huo utakuwa muendelezo wake kwa wote wenye ulemavu jijini Dar es Salaam” alisema Chalamila.

Kwa upande wake Mfanyabiashara huyo anayemilika kampuni inayojihusisha na uuzaji magari alieleza nia yake ya kuendelea kuwasaidia watu wenye ulemavu pamoja na misaada mbalimbali kwa wenye mahitaji,

“Pamoja na kutoa viti mwendo hiivi, naahidi kuwa saidia watu wote wanaishi na ulemavu pamoja na wale wenye mahitaji maalumu katika Mkoa wa Dar es Salaam” alisema Lukosi

Aidha, Chalamila aliwataka wakina mama wote wenye watoto wenye ulemavu kutokata tamaa na kuwasisitizia kuwa, Serikali haijawasahau na kudai kuwa itaangalia cha kufanya kwa ajili ya kuwasaidia watu wote wenye ulemavu.