Na Heri Shaaban, TimesMajira Online
Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Omary Kumbilamoto, ameipongeza Taasisi ya Fahari Tuamke Maendeleo kwa jitihada zake za kupambana na vitendo vya ukatili kwa watoto na kuwataka wadau wengine kuiunga mkono.
Kumbilamoto aliyasema hayo katika wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyoandaliwa na taasisi ya Fahari na kufanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Ulongoni.
Alisema ukatili unatokea kwa sababu watu wengi hawana hofu ya Mungu na kuwataka wazazi na walezi kumrudia Mungu.
“Kama ingekuwa waislam wanafuata maandiko, wakristo wanafuata maandiko ukatili usingetokea katika taifa letu kwa sababu maelekezo ya dini zote yanakataa kuwafanyia watoto ukatili,” alisema Kumbilamoto.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Fahari Tuamke Maendeleo, Neema Mchau, alisema katika kuadhimisha siku hiyo waliguswa pia kutoa msaada kwa watoto 100 wanaoishi kwenye mazingira magumu wanaosoma katika Shule za Msingi Ushindi na Ulongoni.
“Vitu hivi tumevinunua kwa kushirikiana na wazazi wa watoto wanaosoma katika shule yetu ya Fahari, wameguswa kuwafariji watoto hawa ili na wao wasijione wanyonge, wasome kwa bidii na kutimiza ndoto zao,” alisema Neema.
Neema aliutaja msaada huo kuwa ni pamoja na sukari, sabuni, madaftari, mafuta ya kupakaa na dawa za meno.
Pia aliwataka wananchi na wadau mbalimbali kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan katika mapambano ya kupinga ukatili ili kuwanusuru watoto ambao ndiyo waathirika wakubwa wa vitendo hivyo.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake, Asnath Sadala, alisema migogoro ya kifamilia imesababisha baadhi ya watoto kukosa misingi ya malezi na kuzurura ovyo mitaani.
More Stories
Jokate awapa tano vijana UVCCM maandalizi Mkutano Mkuu wa CCM
Watakaokwamisha mapato Kaliua kukiona cha moto
Dkt.Gwajima aagiza kuundwa kamati za ulinzi wa watoto