December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Meya Dormohamed: Ondoeni wanaokwamisha mradi wa TACTIC

Na Esther Macha, TimesMajira Online, Mbeya

HALMASHAURI ya Jiji la Mbeya imezitaka kampuni ya ujenzi ya Cico inayojenga jengo na barabara za mradi wa Tactic na Kampuni ya Mhandisi ambayo ni mkandarasi mshauri kwenye miradi hiyo kuwaondoa wasimamizi wake kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Hayo yamesemwa Mei 22,2024 na Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya Mh.DorMohamed Issa baada ya kuhitimisha ziara ya kukagua ujenzi wa barabara za Kalobe-Itende, Machinjioni- Mapelele, Kabwe-Sido na Iziwa ili kuona hali halisi ya ujenzi .

“Sijaridhishwa na napata wasiwasi na kasi ya maendeleo ya mradi huu na sina uhakika kama mkandarasi atamaliza mradi kwa wakati uliopangwa kwa mujibu wa mkataba “amesema Mstahiki Meya.

Aidha Issa ameongeza kuwa tangu mkandarasi wa kampuni ya Cico alipokabidhiwa na kuanza kazi Novemba, 2023 hakuna alichokifanya kwenye barabara zote, hali ambayo inasababisha wananchi kuendelea kukabiliwa na changamoto ya barabara wakati Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan, imeshatoa fedha.

Hata hivyo Mstahiki Meya huyo amemtaka mkandarasi kumwondoa Meneja Mradi Mhandisi Bw.Penfeng Wang na Kampuni ya Mhandisi ambayo ni Mkandarasi Mshauri, Bw.Jofrey Kanjanja kwa kushindwa kusimamia kasi ya mradi kama ilivyopangwa.

“Mkandarasi mshauri urafiki wako na Mkandarasi unatia wasiwasi, kazi haiendi haiwezekani kila wakati mko pamoja, hapo kazi haiwezi kwenda utashindwa kusimamia vyema mradi huu, naomba kampuni zenu zitubadilishie wasimamizi haiwezekani hata kidogo”, amesema Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya.

Katika hatua nyingine Mstahiki Meya amemtaka Mhandisi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Bw.Leonard Mohosea kuhakikisha kila jumatatu anawasilisha taarifa za mwenendo wa mradi na kumsimamia ipavyo mkandarasi ili kufikia malengo ya mradi ambayo Serikali imejiwekea sambamba na kuwaondelea kadhia wananchini na kusiimua shughuli za maendeleo zitakazokuwa zikifanywa kupitia barabara hizo.

Mradi huo unaogharimu Shilingi Bilioni.21 ukijumuisha barabara tano yenye urefu wa kilometa 12.3(km12.3) mifereji ya maji ya mvua yenye jumla ya urefu wa kilometa 6.4(km6.4) na ujenzi wa jengo la maabara ya udhibiti ubora, ulioanza Novemba, 2023 unaotarajiwa kukamilika Februari 2025.

Mei 23, 2024 Mstahiki Meya anatarajia kuendelea na ziara kukagua utekelezaji wa miradi ya Tactic.