Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Sikonge
WAKAZI wa kata ya Ipole Wilayani Sikonge Mkoani Tabora wamepata ahueni ya kero ya maji baada ya Waziri wa Maji Jumaa Awesu kutuma ujumbe mfupi kupitia simu ya Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Halima Mamuya akiahidi kushughulisha kero hiyo haraka iwezekanavyo.
Waziri ametuma ujumbe huo katika mkutano wa hadhara uliofanyika jana katika kata hiyo baada ya Mamuya kupokea kilio chao kuhusiana na mradi huo kutofanya kazi kwa zaidi ya mwaka sasa na kuwa kero kubwa kwa wananchi.
Baada ya kupokea kilio hicho na kuelezwa kuwa chanzo hicho ndio tegemeo pekee la wakazi wa kata za Chabutwa, Ipole na Ngoywa lakini tangu kiharibike hawana msaada mwingine wowote ule wanaopata, baada ya kuelezwa Waziri akatuma meseji hii, ‘Waambie nimesikia kilio chao nitalishughulikia haraka iwezekanavyo’.
Ujumbe huo uliamsha shangwe na furaha katika mkutano huo baada ya Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa kuusoma hadharani na kuwaeleza kuwa kilio chao kimefika kwa Waziri mwenye dhamana hivyo wasiwe na wasiwasi tena.
Mamuya amewahakikishia kuwa serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ni sikivu, haipendi na haiko tayari kuona wananchi wake wakiteseka, ndiyo maana wamekuja kuona utekelezaji ilani ya uchaguzi katika wilaya zote za Mkoa huo, kusikiliza kero na kuzitafutia ufumbuzi.
Awali akimkaribisha kuhutubia mkutano huo, Diwani wa kata hiyo John Mbogo amesema kero ya maji katika kata hiyo ni kubwa sana kutokana na kuharibika kwa chanzo hicho pekee cha maji kilichowekewa jiwe la msingi na Rais wa kwanza Hayati Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1977 na maji yake hayakauki.
Amebainisha kuwa licha ya serikali kutoa kiasi cha sh milioni 349 kwa ajili ya ukarabati wa chanzo hicho lakini hakuna kilichofanyika huku wakiwatupia lawama Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira (RUWASA) Wilayani humo.
Mbogo ameongeza kuwa haoni sababu chanzo hicho chenye maji ya uhakika kutofanyiwa matengenezo wakati serikali ya Rais Samia inajali sana wananchi wake, na imeendelea kuleta mabilioni ya fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Aidha ameomba Mradi wa serikali wa kupeleka maji katika Miji 28 ambao umeanza kutekelezwa Mkoani humo (Sikonge, Urambo na Kaliua) kufikishwa katika kata hiyo ili kumaliza kabisa kero hiyo kwa wakazi wa kata hiyo na kata jirani.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu