November 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mene ashauri nchi za Afrika kuwa na soko la pamoja

Na Penina Malundo, timesmajira, online

KATIBU Mtendaji wa Eneo huru la  biashara Afrika, Wamkele Mene, amesema Afrika haitafanikiwa kufikia Ukombozi wa kibiashara endapo nchi hizo zake hazitakubali kuungana na kuwa na soko la pamoja ambalo lila nchi itafanya biashara na kupeleka bidhaa bila vikwazo.

Mene alitoa kauli hiyo jana wakati akifungua rasmi Maonyesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (DITF) katika viwanja vya sabasaba. 

Amesema bado kunahitajika nguvu kubwa ya kuleta mapinduzi ya kibiashara kwenye nchi hizo ili zizalishe bidhaa bora na kuwa huru kufanya kwenye soko la ushindani kimataifa. 

“Nchi za Afrika tunahitaji kukubaliana kuwa na soko la pamoja. Si Tanzania, Kenya wala nchi yoyote itafanikiwa kupata uhuru huu kama hazitakubalina kuwa na soko la pamoja,”mesema Mene

Ametolea mfano kwamba hata ulipoingia mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19 pamoja na vita vya Ukraine, uchumi wa nchi nyingi za Afrika uliyumba kwa kuwa baadhi ya bidhaa hutegemea kutoka kwenye nchi hizo. 

“Na ndio maana nasema hivi hakuna mtu yeyote atakayetoka duniani huko kuja kututafutia ukombozi kwenye eneo hili, tunahitaji kushirikiana kupambana wenyewe, “amesema Mene.

Kwa Upande wa Waziri wa Viwanda na Biashara, Ashatu Kijaji, amesema wamemhakikishia kiongozi huyo wa soko huru la biashara Afrika kuwa wanatumia soko hilo kuuza bidhaa zenye ubora.

“Kiongozi huyu baada ya kutembelea mabanda yetu, amesema amegundua tunatengeneza bidhaa nzuri na bora, lakini shida kubwa iliyopo ni kwamba bado hatujafahamu namna ya kuchangamkia soko nje ya Tanzania na ametushauri tuzioongezee thamani na tukashindane,”amesema Kijaji.