Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Serikali imesema kuwa, Tanzania itazalisha umeme wa kiasi cha megawati 200 zinazotokana na Jotoardhi kabla ya mwaka 2025.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, alisema hayo wakati wa ziara yake ya kukagua vyanzo vya nishati ya Jotoardhi vya Kiejo-Mbaka na Ngozi mkoani Mbeya.
Alisema kuwa, Tanzania kuna jumla ya maeneo 52 yanayoweza kutoa nishati ya Jotoardhi ambayo tayari yameshatambuliwa.
Alieleza kuwa, kwa ujumla, Serikali ina mpango wa kuongeza megawati 1100 zinazotokana na Nishati Jadidifu kabla ya mwaka 2025 na hizo megawati zitatokana na vyanzo mbalimbali kama vile Jotoardhi, Jua na Upepo.
Aliongeza kuwa, Wizara ya Nishati inaweka nguvu kubwa katika kuendeleza vyanzo vya nishati ya Jotoardhi kwa sababu vyanzo hivyo haviishi na hivyo ukaguzi alioufanya katika maeneo hayo ya Jaothemo utasaidia Serikali kuona hatua stahiki za kuchukua ili kuendeleza vyanzo hivyo.
“Kipindi cha ukame maji yanaweza kupungua, lakini Jotoardhi katika kipindi cha ukame au mvua, mvuke unaotoka chini ya ardhi uko palepale.” Alisema Katibu Mkuu
Alisema kuwa, nchi ya Kenya ina zaidi ya megawati 1100 zinazotokana na Jotoardhi na Tanzania kutokana na eneo lake kubwa kupitiwa na Bonde la Ufa kuna uwezekano wa kupata umeme mwingi zaidi unaotokana na nishati hiyo.
“Mfano hapa mkoani Mbeya katika eneo hili la Rungwe kumeonekana kuna uwezekano mkubwa wa kutoa nishati ya Jotoardhi kwa sababu tawi moja la Bonde la Ufa limeingia katika eneo hili na Tawi jingine limeelekea upande wa Malawi.” Alieleza Mhandisi Mramba
Kwa upande wake, Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania (TGDC), Mhandisi Mathew Mwangomba alisema kuwa, eneo la Kiejo-Mbaka linaweza kuzalisha megawati 60 zinazotokana na Jotoardhi.
Alisema kuwa, Serikali imetoa takribani shilingi Bilioni 20 kwa ajili ya uendelezaji wa eneo hilo na sasa wamenunua mtambo wa kuchoronga eneo hilo, na kwamba, Wataalam wa TGDC na Wahisani wameshirikiana katika kufanya tafiti zote zinazotakiwa.
Aliongeza kuwa katika eneo la Ngozi, inategemewa kuwa litazalisha megawati 70 zinazotokana na Jotoardhi na kwamba TGDC imejipanga vizuri katika kuhakikisha kuwa Tanzania inapata umeme kutoka kwenye nishati hiyo Jadidifu.
More Stories
CPA.Makalla :CCM kutumia 4R za Rais Samia katika uchaguzi Serikali za Mitaa
CCM kutumia 4R za Samia Uchaguzi Serikali za Mitaa
Dkt. Mpango awasilisha salam za Rais Samia mazisha Baba yake mzazi, Gavana Tutuba