Na Mwandishi wetu, Timesmajira
Katika kuhakikisha elimu ya nishati safi ya kupikia inamfikia kila Mtanzania, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange ametumia sehemu ya ziara yake ya kukagua maendeleo ya miradi ya umeme katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupika kwa umeme kwa viongozi wa Serikali za Mikoa na Wilaya ili kuongeza uelewa zaidi kwa wananchi.
Bw. Twange ametumia nafasi hiyo kuelimisha na kutoa zawadi za majiko janja yenye teknolojia inayotumia umeme kidogo kwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Kenani Kihongosi, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ,Saidi Mtanda, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi Pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Wakili Julius Mtatiro ikiwa ni sehemu ya Kampeni ya TANESCO ya kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kutumia umeme.
Amesema licha ya Shirika hilo kujikitika katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya umeme wa uhakika bado wanajukumu la kutekeleza kwa vitendo Ajenda ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wananchi wanatumia nishati safi kwa ajili ya kupikia na ametoa majiko hayo kwa viongozi wa Serikali ili kupata picha halisi ya unafuu wa kutumia umeme kupikia ili kuwa mabalozi wazuri kwa wananchi.

‘’Vifaa hivi vinatumia umeme kidogo kwenye kupika na tumetoa majiko haya kwa ajili ya matumizi ya kupikia ili mtusaidie kuwahamasisha na kuongeza uelewa kwa wananchi kwa kuwa mtakuwa mashahidi na mabalozi wazuri wa kueleza faida za majiko hayo hatua itakayowavutia zaidi wananchi kisha kubadili mitazamo’’ amesisitiza Twange
Naye Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Wakili Julius Mtatiro ameipongeza TANESCO kwa mkakati huo ambao unadhamira ya dhati ya kufanya mageuzi ya elimu ya matumizi ya nishati safi ili kuwafanya wananchi kuachana na matumizi ya nishati isiyo salama zenye athari kiafya kwa watumiaji na chanzo cha uharibifu wa mazingira.
‘’Tumepokea zawadi ya jiko hili tunashukuru, tutaitumia mikutano yetu na wananchi kutoa elimu ya matumizi ya nishati safi na wananchi wetu ni waaminifu ninaamini wataelewa na kwa sasa tutawaelimisha kwa vitendo,’’ amefafanua Mtatiro.
Ziara ya Mkurugenzi wa TANESCO,Lazaro Twange katika Mikoa ya kanda ya ziwa imelenga kukagua miradi mbalimbali ya uzalishaji umeme lakini pia ametumia nafasi hiyo kuongeza msisitizo wa matumizi ya nishati safi ya kupikia ya umeme ikiwa ni muendelezo wa kampeni inayofanywa na TANESCO ya kuhakikisha ajenda ya Serikali inafanikiwa.
More Stories
Kiongozi wa Mwenge aifagilia RUWASA Tanga
Rais Samia kuanza ziara ya siku saba Simiyu na Mwanza
Msigwa awataka wazazi kuzungumza na watoto wao matumizi mabaya ya mtandao