January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mchikichini kuimarisha ulinzi kukabiliana na uhalifu

Na Agnes Alcardo, TimesMajira Online, Dar

UONGOZI wa Soko la Mchikichini maarufu kama Karume, lililopo Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, umedhihirisha kuchukua hatua za makusudi katika kuimarisha ulinzi wa soko hilo kwa kuajili walinzi kutoka katika kampuni zenye uzoefu na kufunga CCTV kamera, ili kuwabaini waharifu na baadhi ya wafanyabiashara wenye nia hovu.

Akizungumza na Mwandishi wa gazeti hili leo Jijini humo, Mwenyekiti wa Soko la Mchikichini, Geofrey Milonge, amesema, hatua hizo zimechukuliwa ili kukabiliana na matukio ya wizi na moto, ambayo yameendelea kutokea katika soko hilo.

Amesema, kumekuwa na matukio mengi ambayo yamekuwa yakifanyika katika soko hilo, Hali ambayo imekuwa ikihatarifa maisha na biashara za watu wengi katika soko hilo.

Aidha amesema, toka uongozi wa soko hilo uamue kuimarisha ulinzi wa soko, matukio mengi ya wizi na kuungua kwa soko yamepungua ” hapo mwanzo kulikuwa na matukio mengi sana yakiharifu katika soko letu lakini tangu tulipoimarisha ulinzi kwa kuweka walinzi kutoka kwenye kampuni zenye uzoefu mzuri na kufunga CCTV kamera matukio mengi yamepungua hata ya kuungua kwa moto kwani wakati mwingine inaweza kuwa ni uzembe wa mtu mmoja unaweza sabanisha hasara kwa soko zima”, amesema Milonge.

Pia, ameushukuru uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwajali na kuwawezesha wamachinga katika soko hilo, huku akielezea ushirikiano mzuri wanaoupata kutoka kwa viongozi wake wa chini akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo na Mbunge wa Ilala, Mussa Azan Zungu.

Nae, Mmachinga katika soko hilo, Assumpa Moshi, ameelezea Mabadiliko mazuri waliyopata katika soko hilo akitofautisha na ilivyokuwa awali, ambapo mali zao zilikuwa hatarini.

” kwakweli tunashukuru sana kwa huu uongozi wetu wa sasa kwani umekuja na Mabadiliko makubwa mno ya kuhakikisha hivi sasa mali zetu zinakuwa na usalama, hapo mwanzo ilikuwa ukifunga biashara yako jioni unapoondoka unamuachia Mungu lakini hivi sasa tuna amani kwani ulinzi umeimarishwa.Lakini pia tunaendelea kutoa shukrani zetu kwa Serikali kwani imeendelea kututhamini na kutufanya kupenda mazingira yetu ya kazi kutokana na kutujengea miundombinu mizuri katika soko letu”, ameongeza Assumpta.