Na Penina Malundo, Timesmajira
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mohamed Mchengerwa amewataka wagombea wote ambao hawajaridhishwa na uteuzi wa wagombea wa nafasi mbalimbali kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa waweke pingamizi ndani ya siku 2 kuanzia leo tarehe 08 – 09/11/2024.
Amesema hayo leo tarehe 8 .11.2024 wakati akiongea na vyombo vya habari kuhusu uteuzi wa wagombea katika Ofisi za Wizara jijini Dodoma
“Kama mnavyojua, leo ni siku muhimu ya uteuzi wa wagombea kwaajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa mujibu wa Kanuni ya 18 ya Tangazo la Serikali Na. 571, 573, 574, pamoja na Kanuni ya 17 ya Tangazo la Serikali Na. 572 yote ya tarehe 12 Julai 2024.”
“Kanuni hizi zinamtaka Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi kufanya uteuzi wa wagombea leo tarehe 8 Novemba, 2024, kuanzia saa mbili kamili asubuhi hadi saa kumi kamili jioni. Mara baada ya uteuzi kukamilika, majina ya wagombea wenye sifa na wale ambao hawajakidhi vigezo vya kugombea yatabandikwa hadharani ili umma uweze kuyapata wakiwemo wagombea wenyewe”.Amesema Mchengerwa.
Ameendelea kueleza kuwa kwa mujibu wa Kanuni hizo mtu yeyote aliyeomba kuteuliwa kuwa mgombea au mgombea ambaye hakuridhika na uamuzi uliotolewa na Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi, anaweza kuwasilisha pingamizi na kumuomba Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi kupitia upya uamuzi uliofanyika ili amteue kuwa mgombea au atengue uteuzi anaoupinga.
Amesema kwamba pingamizi hili linaweza kuwasilishwa kwa maandishi ndani ya siku mbili tangu uamuzi au uteuzi ulipofanyika. Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi atalishughulikia pingamizi hilo na kutoa uamuzi ndani ya siku mbili tangu alipolipokea.
“Hivyo, kwa mujibu ya kanuni hizi, kuanzia leo tarehe 8 na kesho tarehe 9 Novemba 2024, kwa mgombea yeyote ambaye hatoridhika na uamuzi wa Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi kuhusu uteuzi, anapaswa kutumia nafasi ya siku hizi mbili ili malalamiko yake yaweze kufanyiwa kazi kwa mujibu wa Kanuni’.Alisisitiza
Amesema kwamba Uchaguzi huu unaongozwa na kanuni hivyo wagombea wasioridhika wanapaswa kuweka pingamizi na sio kuzungumza mitandaoni kwa sababu endapo utazungumza mitandaoni na hujawaweka pingamizi atakuwa hujafuata Kanuni hivyo wote wenye changamoto wahakikishe wanaweka pingamizi kwenye maeneo yao.
Aliongeza kuwa iwapo mgombea hatoridhika na uamuzi wa Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi juu ya pingamizi lake, ana haki ya kukata rufaa kwenye Kamati ya Rufaa ndani ya muda usiozidi siku nne baada ya uamuzi huo kutolewa. Maana yake Rufaa ziwasilishwe kuanzia tarehe 10 hadi 13 Novemba, 2024 kwa kamati ya Rufaa.
Aidha, amesema ni muhimu wagombea wote wafuate taratibu za kisheria na kuhakikisha malalamiko yao yanawasilishwa katika sehemu sahihi ndani ya muda uliowekwa kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi. Hii itasaidia kuimarisha utulivu na uwazi katika mchakato mzima wa uchaguzi.
More Stories
DC Korogwe awataka viongozi wa vijiji kuwatumikia wananchi kwa uadilifu
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam