Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya
WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Adolf Ndunguru kuziandikia barua Halmashauri ambazo mapato yake ya ndani yanazidi sh.bilioni tano kutenga fedha Kwa ajili ya ukarabati wa barabara za ndani.
Mchengerwa amesema hayo Julai 28,2024 mkoani Mbeya wakati akizindua bodi ya ushauri ya Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini(TARURA)ambapo amesisitiza kila idara kufanya Kazi Kwa ubunifu ili kuleta ufanisi na sio kukaa kusubiri bajeti ya serikali Kuu.
Aidha Mchengerwa ameeleza kuwa tangu kuanzishwa Kwa TARURA mwaka 2017, Halmashauri zimejisahau kutenga fedha za ukarabati wakati sheria inazitaka kufanya hivyo zile zenye mapato ya ndani yanayozidi sh.bilioni tano.
Hata hivyo Mchengerwa amesema kwamba Halmashauri ya Jiji la Mbeya imekuwa ya mfano Kwa kutenga fedha za ukarabati wa barabara akitaka Halmashauri nyingine ziige mfano huo, kwani kusubiri fedha kutoka serikali Kuu wakati zina mapato yake ni kuchelewesha maendeleo ya wananachi.
Akielezea kuhusu bodi Waziri Mchengerwa amesema ina wajibu wa kumshauri Waziri na Katibu Mkuu ili kuhakikisha wananchi wanaunganishwa na mawasiliano ya barabara lakini akatahadhari kuepuka kujiingiza kwenye utendaji kwani jukumu hilo ni la katibu mkuu na Mtendaji wa TARURA.
Aidha, ameitahadharisha bodi hiyo kutoingilia majukumu ya utendaji badala yake ijielekeze kwenye mambo ya sera na ushauri ili kuleta ufanisi kwenye sekta hiyo.
“Nimpongeze Sana mtendaji Mkuu wa TARURA kwa Kazi nzuri hasa kipindi hiki cha serikali awamu ya sita na wasaidizi kazi mnayofanya ni kubwa nchi nzima mnafanya kazi vizuri naomba msilewe sifa bado
mna kazi kubwa kwani taifa bado linawahitaji Sana ,tupo katika wakati mgumu ambapo barabara nyingi zimeharibiwa na mvua na mvua ikaja na kuharibu ovyo “amesema Waziri Mchengerwa.
Kwa upande wake Mtendaji mkuu wa wakala wa barabara Vijijini na Mijini,Mhandisi Victor Seif amesema kuwa wajumbe wapya wa bodi ya ushauri ya TARURA wafanye kazi na kutimiza wajibu wao na kutimiza matakwa ya Rais Dkt.Samia .
Katibu Mkuu wa TAMISEMI Adolf Ndunguru amesema bodi hiyo itaongeza ufanisi, akieleza kuwa wakati ilipomaliza muda wake majukumu ya bodi alikuwa akiyafanya yeye na kusema bodi ina jukumu la kumshauri Waziri kuhusu malengo, vipaumbele,mipango,tathmnini,mikakati ya TARURA,posho na mishahara ya watumishi.
Ndunguru amesema kuwa bodi hiyo ya ushauri inamajukumu ya kisera na kusema huko nyuma mahudhurio hayakuwa mazuri ya wajumbe,hivyo inatakiwa wajumbe wote wahudhurie katika vikao vyao sio kutuma wawakilishi.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakaniÂ
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best