
s Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),Mohamed Mchengerwa, ametoa maagizo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Geofretly Mkinga, kuhakikisha kuwa ifikapo Oktoba 2025, mradi wa ujenzi wa barabara ya Banana hadi Msongola yenye urefu wa kilomita zaidi ya 12, pamoja na uwekaji wa taa za barabarani, uwe umefika kiwango walichokubaliana na mkandarasi Oktoba mwaka huu na hadi April, mwakani kuwa imekamilika kwa kiwango cha lami.
Mchengerwa ametoa maagizo hayo mwishoni mwa wiki, wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo, ambao tayari umeanza kutekelezwa, akiwa ameambatana na Mbunge wa Jimbo la Ukonga, Jerry Silaa, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, Meneja wa TARURA Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandishi Geoffrey Mkinga na viongozi wengine wa Serikali.
Amesema, Serikali imetoa kiasi cha Sh bilioni 30.8 kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa kiwango cha lami na kuweka taa katika barabara ya kutoka Banana hadi Kata ya Msongola, huku akisitiza kwamba hatua stahiki zitachukuliwa endapo kutakuwa na ucheleweshaji usio na sababu za msingi katika utekelezaji wa mradi huo muhimu kwa wananchi wa maeneo husika.
“Wananchi wa maeneo haya wamekuwa wakikumbwa na changamoto ya muda mrefu ya barabara mbovu, yenye mashimo na vumbi. Tunataka kuona kuwa ifikapo mwezi wa 10 kazi hii imekamilika kwa kiwango kinachokubalika. Ucheleweshaji wa makusudi hautavumiliwa,” alisisitiza Mhe. Mchengerwa.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mbunge wa Jimbo la Ukonga, Jerry Silaa, amesema, utekelezaji wa barabara hiyo ulianza awamu za nyuma, huku akidai kuwa akiwa kama mbunge wa jimbo hilo, alihakikisha barabara hiyo inaingia katika ilani ya CCM mwaka 2020 kwa ujenzi wa kilometa 10.5 za awali huku akimshukuru Mwenyekiti wa CCM pia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia kilometa zaidi ya 18 badala ya kilometa 11.5.
Silaa amesema, mgawanyo wa ujenzi wa barabara hiyo ni kilometa 3.95 kuanzia Banana hadi relini, kilometa 11.9 kuanzia kipande cha Kivule hadi Msongola na kilometa 2.78 kuanzia njia panda ya hospitali ya Wilaya hadi njia panda Ngongole.
Aidha, katikati ya ziara hiyo, Silaa alitumia nafasi hiyo kuwaaga wananchi wa Kivule, ambao wapo katika Jimbo jipya la Kivule akisema kuwa, pamoja na Jiografia ya mipaka kuwagawa lakini bado ana ‘mapenzi ya dhati’ na wananchi hao.
“Yapo mengi tuliyofanya wote na nipende tu kuwashukuru sana kwa ushirikiano wenu ambao mmenionesha kwa kipindi chote cha uongozi wangu katika Jimbo hili na wengine wanasema kuwa Mh Jerry amechukua fomu ya kuomba ridhaa kugombea Ukonga kwahiyo sisi Wana-Kivule hatupendi niseme ukweli kutoka moyoni mwangu kuwa Kivule ipo katika sakafi ya moyo wangu! Alisema Silaa.
Kwa upande wake, Meneja wa TARURA Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Geofrey Mkinga, amesema mradi huo una thamani ya shilingi bilioni 30 na utekelezaji wake umeanza rasmi.
Ameeleza kuwa hadi sasa utekelezaji wa mradi huo umepaswa kufikia asilimia 32, lakini kumekuwa na kuchelewa kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo mvua kubwa zilizonyesha jijini Dar es Salaam pamoja na mchakato wa ulipaji fidia kwa wananchi waliotakiwa kupisha mradi huo.
Mhandisi Mkinga amebainisha kuwa hatua za kushughulikia changamoto hizo zinaendelea kuchukuliwa, ili kuhakikisha utekelezaji wa mradi huo unarudi katika mstari na kukamilika kwa wakati kama ilivyopangwa.
Mradi wa barabara ya Banana hadi Msongolo ni miongoni mwa miradi mikubwa ya kuboresha miundombinu jijini Dar es Salaam, ukiwa na lengo la kurahisisha usafiri na kuboresha maisha ya wakazi wa maeneo ya Ilala na viunga vyake.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, aliahidi Kusimamia utekelezaji wa mradi huo kuhakikisha dhamira ya Serikali kwa wananchi wake inaenda kusimamiwa na kutekelezwa kwa kiwango stahiki na kusema kuwa Wilaya hiyo imepewa heshima kubwa.

More Stories
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi
Waziri Mkuu kuanza ziara mkoani Rukwa Marchi 8 Hadi 10
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani