Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
TUME ya Madini imesema mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 7.2 Mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 9.0 Mwaka 2023.
Hayo yamesemwa jijini hapa leo,Machi 4,2025 na Katibu Mtendaji wa Tume hiyo Mhandisi Ramadhani Lwamo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na utekelezaji wa tume hiyo kwa kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya sita.
Mha.Lwamo amesema kuwa hiyo ni kutokana na kuimarika kwa usimamizi wa shughuli mbalimbali za Madini.
Vilevile amesema ukuaji wa Sekta ya Madini umeongezeka kutoka asilimia 9.4 Mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 11.3 Mwaka 2023.
“Hii ni Kutokana na kuendelea kuimarika kwa Sekta ya Madini, mwenendo wa Mchango wa Sekta ya Madini na ukuaji wake unatarajiwa kufikia asilimia 10 na zaidi ifikapo Mwaka 2025,”amesema.
Aidha Mha.Lwamo amesema kuwa kiwango cha makusanyo ya maduhuli ya Serikali kimepanda kutoka shilingi bilioni 624.61 zilizokusanywa mwaka wa fedha 2021/2022 hadi kufikia shilingi bilioni 753.82 mwaka wa fedha 2023/2024
“Kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022 mauzo ya madini katika masoko na vituo vya ununuzi wa madini yameendelea kuongezeka kutoka shilingi bilioni 2.361.80 hadi shilingi bilioni 2,597.18 kwa mwaka 2023/2024,”amesema.
Pamoja na hayo Mha.Lwamo amesema kuwa Tume ya madini imeendelea kusimamia kikamilifu upatikanaji wa ajira kwa Watanzania kwenye kampuni mbalimbali za uchimbaji wa madini.
Ambapo Ajira 19,874 zimezalishwa na makampuni ya uchimbaji wa madini ambapo kati ya hizo, 19,371 ni Watanzania.
Ameeleza kuwa Tume imeweka mazingira rafiki kwa ajili ya wachimbaji wadogo wa madini kupata leseni za uchimbaji pamoja na kuwaunganisha na taasisi za kifedha ili wapate mikopo kwa ajili ya uendelezaji wa shughuli za uchimbaji.
“Tume imefanikiwa kutoa jumla ya leseni 41,424 kati ya 37,318 zilizopangwa kutolewa katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita ambayo ni sawa na asilimia 111. Leseni hizo zilijumuisha leseni za uchimbaji mkubwa, uchimbaji wa kati na uchimbaji mdogo,”amesema


More Stories
TMDA yajivunia kuanzisha mfumo thabiti wa udhibiti wa vifaa tiba na vitendanishi
Kikwete kuungana na marais watatu kushiriki Kongamano la nane la viongozi Afrika
Katavi yazindua kampeni kukabiliana na udumavu