December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mch.Msigwa aikosoa CHADEMA mbele ya Mwenezi wa CCM taifa

Na Agnes Alcardo,TimesmajiraOnline,Dar

ALIYEKUWA Mbunge wa Jimbo la Iringa na Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa na Mjumbe wa Kamati Kuu kwa takribani miaka 10, kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),Mch.Peter Msigwa,amewasihi wananchi kutopoteza muda kuiunga mkono CHADEMA akidai kuwa, chama hicho kimekosa maono na kitawapeleka kusikojulikana chini ya Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe.

Mch.Msigwa, amesema hayo leo,Julai 16,2024 Jijini hapa kwenye Mkutano wa Hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Panga, maeneo ya Wazo katika Jimbo la Kawe Jijini Dar es Salaam, ikiwa ni muendelezo wa Ziara ya siku 10 ya Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, CPA Amos Makalla, yenye lengo la kukagua uhai wa Chama cha CCM, kukagua Miradi ya Maendeleo na utekelezaji wa Ilani ya Chama 2020/2025.

Amesema ameamua kuhama CHADEMA na kuhamia CCM, kutokana na chama hicho kupoteza muelekeo wa maono na kuwa Chama chenye kujali maslahi ya watu wachache na kuongeza kuwa suala la Demokrasia, Uhuru na Haki limekuwa ni suala linaloongelewa midomoni na si kufanya kwa vitendo.

Pia amesema kuwa, kati ya sababu zilizofanya kukiacha chama hicho na kuhamia CCM ni pamoja na kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha anawaletea maendeleo wananchi wake na kutumia mfumo wa maridhiano (R4), kitu ambacho kimeonekana kuwa kizuri na kinachochea amani nchini.

“Leo nimeona nije hapa kuelezea furaha yangu niliyonayo hivi sasa kwani hivi karibuni nilikaribishwa CCM kwa kupokelewa na Mwenyekiti wa Chama cha CCM na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan na kukataa kuendelea kuwa mjinga CHADEMA.

Pia niwasihi vijana wote na wananchi kwa ujumla wenye mpango wa kuunga mkono CHADEMA wasiwe na mawazo hayo kwani huko watapoteza muda wao kwa kutumika mwishoni kupelekwa kusikojulikana”, amesema Mch. Msigwa.

Aidha ameeleza kuwa CHADEMA ni chama ambacho kimekuwa kikijiongoza bila ya kufuata Demokrasia, Haki na Uhuru, tofauti na waliokuwa ndani ya chama hicho ambavyo wamekuwa wakihaminishwa kuwa ni chama kinachopigania haki za wananchi.

“Wakati najiunga na CHADEMA yule Nkurunzinza na viongozi wenzake walituhaminisha kuwa CCM inakosea na tuliwaamini kweli kweli huku wakiongelea kuwa CHADEMA ndiyo chama kinachostahiri kushika madaraka, kwani kinafuata misingi ya Demokrasia, Haki na Uhuru kumbe si kweli hivyo wanavyosema vinatoka tu midomoni na katika mioyo yao hivyo ndugu zangu tusipoteze muda katika chama kile”, ameeleza Mch. Msigwa.

Pia ameongeza kuwa, CHADEMA ni chama ambacho kimekuwa hakijali maslahi ya Wanachama wake hususani viongozi wa Chama, kwani ni chama ambacho kimekuwa kikiwataka Wanachama wake kufanya shughuli za kichama kwa kutumia gharama zao binafsi.

“Ninayowaeleza haya ni ya kweli, kwani nimekuwa katika Chama kile kwa muda mrefu sana, chama kile hakina hata hela ya kujiendesha wakati kimekuwa kikichukua pesa za ruzuku, alafu ukiuliza Mwenyekiti sasa hapa natakiwa kwenda sehemu fulani kwa ajili ya shughuli ya kichama anakwambia komaa Kamanda! Yani sisi tukomae wakati yeye anatumia Chopa ( Helicopter )”, ameendelea kufafanua Mch. Msigwa.

Mch. Msigwa ameendelea kusema kuwa, katika nyakati tofauti baadhi ya viongozi katika chama hicho, walipoamua kutoa ushauri juu ya kufuata misingi ya chama, Mwenyekiti huyo amekuwa akiwaambia wafuate Katiba na si matendo ya mtu, huku akieleza kuwa hivi sasa hata viongozi ambao wamekuwa wakipatikana katika chama hicho si kwa kufuata Katiba bali ni uchaguzi wa mtu mmoja.

” Kwa kuwa ni chama ambacho tuliaminishwa kuwa ni chama kizuri na kinachofuata katiba yake, kuna wakati tulikuwa tukitoa ushauri kwa viongozi wenzetu lakiniajibu yaliyokuwa yanatoleea na yule Nkurunzinza ni kuwa fuateni Katiba na si maneno ya mtu hii imekaaje? Wakati moja ya sifa ya kiongozi ni pamoja na kuyaishi Yale unayoyahutubia”, amesema Mch. Msigwa.