December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

MCB kukutana Iringa Mkutano Mkuu wa Mwaka 2024

Mkutano Mkuu wa mwaka wa wenyehisa wa Benki ya Biashara ya Mwalimu (MCB) 2024 umepangwa kufanyika tarehe 27 Juni 2024 Mkoani Iringa, huku benki hiyo ikionesha azma yake thabiti katika uwazi na ushirikiano na wadau.

“Mkutano huu wa Mwaka unathibitisha umuhimu wa muundo imara wa utawala wa MCB, ukiwapa wanahisa jukwaa muhimu la mazungumzo yenye tija kuhusu mwelekeo na mafanikio ya benki,” amesema Bi. Anna Mgaya kutoka Idara ya Masoko ya MCB katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana.

Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2016, MCB imejipambanua kama taasisi madhubuti katika sekta ya benki nchini Tanzania, ikipata mafanikio makubwa ambayo yatajadiliwa kwa kina katika mkutano huo.

Washiriki wanatarajiwa kufanya mapitio kamili ya utendaji wa MCB kwa mwaka uliopita, pamoja na majadiliano kuhusu mikakati muhimu na fursa za kuongoza mwelekeo wa benki huko mbeleni, alisema Anna kupitia taarifa hiyo.

“Mkutano huu wa kila mwaka ni zaidi ya majukumu yakawaida kwetu, hili ni jukwaa muhimu la kuunganisha shughuli zetu na matarajio ya wadau wetu,” aliongeza Bi. Mgaya.

Mbali na mafanikio ya kifedha, Benki ya Biashara ya Mwalimu inaendelea kujizatiti kwa miradi yake ya kijamii(CSR) kama elimu, afya, na utunzaji wa mazingira, Hatua hizi zinaonesha azma ya MCB katika kuleta mabadiliko chanya katika jamii.

Mkutano Mkuu wa Mwaka unatarajia kuwezesha majadiliano yatakayojenga uelewa wa kina na kwamba unahimiza ushiriki wa wanahisa kushirikiana na bodi katika kukuza ufanisi kwenye mazingira yenye ushindani mkubwa.

Tutatumia fursa hii kujengeana ufahamu zaidi kuhusu maono ya kimkakati na misingi ya kisasa katika uendeshaji wa benki, Kama taasisi ya kifedha inayoaminika, Mwalimu Commercial Bank inaendeleza ubunifu katika kutimiza mahitaji mbalimbali ya wateja wake, huku  ikiheshimu misingi ya uadilifu, weledi, na kujikita katika huduma bora kwa wateja.