December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbunge alia na bajeti ya kilimo, soko la Chai

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dodoma

MBUNGE wa Njombe Mjini kwa tiketi ya CCM, Deodatus Mwanyika, amesema kutokana na kilimo kuwa ndicho kinabeba maisha ya Watanzania wengi, alitegemea bajeti ya Wizara ya Kilimo ingekuwa kubwa na ya kutosha, lakini kwa bajeti iliyopangwa hadhani kama itakidhi matarajio ya wengi.

Mbunge Mwanyika aliyasema hayo wakati akichangia mjadala wa Makadirio ya Bajeti ya Wizara Kilimo bungeni, jijini Dodoma.

Hata hivyo, amesema anawapongeza mawaziri na watendaji wa wizara hiyo kwa juhudi zao, kwani pamoja na bajeti kutokutosha, lakini wamejaribu kuweka maeneo ya mikakati ambayo yanaenda kushughulikia baadhi ya matatizo.

Mwanyika amesema itategemeana sana kama hizo fedha ndogo zilizopangwa kama zitapatikana. “Kama zisipopatikana, tutakuwa tunatwanga maji kwenye kinu, na sidhani kama kuna mafanikio ambayo yatapatikana ikilinganishwa na matarajio,” alisema Mwanyika.

Kwenye mchango wake, Mwanyika aliongelea mazao mawili ambayo yapo kwenye Jimbo la Njombe Mjini na katika Ukanda Mzima wa Nyanda za Juu Kusini.
Akianza na chai, alisema ni zao ambalo wana uhakika kwa sasa hivi katika soko la dunia bei yake inasikitisha.

Amesema pamoja na hayo, hapa nchini uzalishaji wa chai umeshuka kwa maana ya majani mabichi ya zao hilo. Pamoja na hayo, alisema anampongeza Waziri Mkuu na waziri wa wizara yenye dhamana ya kilimo walienda Njombe Machi 10,mwaka huu na kukutana na wadau wa chai.

“Tuliwaeleza matatizo yote ya chai, tukayajenga na kuweka mikakati, jambo kubwa ambalo wanalielewa ni kuhusiana na umwagiliaji. Tunahitaji kuwa na bajeti kubwa ya umwagiliaji, katika bajeti ya leo umwagiliaji umepewa bajeti kidogo,”amesema na kuongeza;

“Nina matumaini makubwa kwa sababu mheshimiwa waziri amekuja Njombe akayasikia, hivyo katika pesa hizo atahakikisha wakulima wa chai wa Njombe wanahudumiwa.”

Ametaja jambo lingine ambalo ni la umuhimu ni miundombinu wezeshi katika zao la chai. Alisema kama hawataainisha suala la miundombinu wezeshi katika suala la chai, hawatapata mafanikio wala malengo ya kuongeza uzalishaji wa chai kutoka tani 37 kwenda kule ambako wanataka, hawatafanikiwa.

Aidha, ametaja eneo jingine kuwa ni la ugani, akisema ni jambo la muhimu sana, lakini hawapo vizuri kwenye suala la ugani. Alisema inatakiwa waajiriwe maofisa ugani wa kutosha, kwani kuna wakulima wadogo wadogo ambao wanahitaji msaada mkubwa wa maofisa ugani.

Mbunge wa Njombe Mjini, Deodatus Mwanyika akichangia mjadala wa Makadirio ya Bajeti ya Kilimo bungeni Dodoma, ambapo ameiomba Serikali kuingilia Kati suala la wakulima wa chai Njombe Kukosa soko la zao hilo kwa kuzuiwa kuuza kwenye kiwanda chenye uwezo wa kuwalipa kisa Kilimo mkataba na viwanja visivyowalipa.

Ameomba hilo waendelee kuliangalia na amefurahi bajeti yao imeongezwa. “Lakini soko ni tatizo kubwa sana, Njombe na zao la chai soko letu sisi ni viwanda, viwanda vikifanyakazi maana yake tuna soko.

Kinachojitokeza Njombe tuna viwanda vinne vya Chai, hatuna uhakika wa hilo soko, lakini kwa bahati mbaya katika uemdeshaji wa viwanda vya chai katika eneo la Njombe ni mwekezaji mmoja ambaye anaendesha ofisi na anaweza kuwalipa wakulima.

Waendeshaji wengine wa viwanda vya chai mheshimiwa Spika ni jambo la kusikitisha, havijalipa wakulima wa chai, waziri mkuu ameliingilia, mheshimiwa Waziri amelisikia,lakini linaendelea,” alisisitiza Mwanyika .

Amesema kiwanda kilichobaki kimoja chenye uwezo wa kununua chai kina matatizo bado hakikipati majani ya chai ya kutosha.

Amesema mfumo wa kiwanda hicho ilikuwa ni kupata majani ya chai kutoka kwa wakulima wadogo wadogo, majani ya chai hayatoshi.

“Lakini ni kweli kwamba maeneo mengine yanayozalisha majani ya chai yanaweza yakauza kwenye kiwanda kile, lakini kwa sababu ya mikataba ambayo imesainiwa wakulima wale wanatakiwa wapeleke chai kwenye viwanda vya yule mtu ambaye hawezi kuwalipa.

Hili ni jambo ambalo wana Njombe hatulikubali, kwa nini wana-Njombe wasipeleke chai kwa yule mwenye kiwanda ambaye analipa?”