May 27, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbunge Kasalali atoa ushauri mzito maboresho Jeshi la Polisi

Na Joyce Kasiki, Timesmajira online,Dodoma

MBUNGE  wa Sumve, Kasalali Mageni, ameibua hoja nzito kuhusu changamoto zinazowakabili askari wa Jeshi la Polisi nchini na umuhimu wa Serikali kuchukua hatua madhubuti katika kuimarisha mazingira yao ya kazi.

Kasalali  ametoa kauli hiyo Bungeni jijini Dodoma , Leo Mei 26 ,2025 Wakati akichangia bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Aidha aliwataka viongozi waandamizi wa Wizara, hususan Waziri na Mkurugenzi mpya wa vitambulisho, kuongeza kasi na kuonyesha dhamira ya kweli ya kufanya mageuzi makubwa.

 “Wahusika wa vitambulisho wanatakiwa kuamshwa zaidi, bado wanaiangusha Serikali,” amesema kwa msisitizo.

Katika mchango wake, Mbunge huyo amewapongeza askari wa Jeshi la Polisi kwa kazi nzuri wanayoifanya huku  akisisitiza kuwa ,wanahitaji kupewa mazingira bora ya kazi ili waendelee kutoa huduma kwa weledi.

 “Askari anatoka chuoni akiwa mzalendo halisi, tayari kulitumikia Taifa lake. Lakini je, tunampa mazingira bora ya kutekeleza jukumu hilo?” alihoji  Kasalali.

Ameeleza kuwa licha ya utii wa sheria na taaluma waliyonayo, askari wamekuwa wakikumbwa na changamoto nyingi ambazo wakati mwingine hukosa sehemu ya kuzizungumza. 

Amesema Bunge ndilo jukwaa sahihi la kutetea maslahi ya askari ili waweze kuishi maisha yenye staha na kufanya kazi kwa morali ya juu.

“Kama Bunge na Serikali, tujiulize: Askari anapohamishwa, je, analipwa fedha za uhamisho kwa wakati? Akipatwa na matatizo, fidia inatolewa kwa haraka? Akistaafu au kwenda likizo, malipo yake yanatolewa kwa staha? Kama haya hayafanyiki, tusishangae kuona baadhi yao wakitafuta njia mbadala za kukidhi mahitaji yao,” ameongeza.

Mbunge huyo pia aligusia uhaba wa sare za kazi, akiitaka Serikali kuhakikisha kuwa Jeshi la Polisi linakuwa na sare nyingi za ziada zinazozidi idadi ya askari waliopo, badala ya askari kuanza “kujipendekeza” ili kupata uniform mpya.

“Kuna wakati gari la polisi halina mafuta, au tairi limeisha , wanakwenda kudoea matairi kwenye magari ya Halmashauri. Hili halikubaliki. Jeshi letu haliwezi kuhudumiwa kwa kubahatisha wakati wao wanatuhudumia kwa uaminifu na ujasiri,” amesema 

Amehitimisha kwa kusema kuwa kazi nzuri ya polisi ndiyo inayolifanya Taifa kuwa salama, na kwamba Serikali ina jukumu la kuwapa motisha na huduma stahiki kama ishara ya kuthamini mchango wao. 

“Tunapojivuna kuwa mitambo yetu imepimwa na kukutwa imara, ni kwa sababu ya askari wetu, tuwatendee haki.”