Na Iddy Lugendo, Timesmajira Online
TUME ya Ushindani (FCC) imepongezwa kwa jitihada kubwa wanazoendelea kufanya kwa kutoa Elimu kwa wadau na wananchi mbalimbali ambao wamekuwa wakitembelea banda lao katika Maonesho ya Sita ya Madini kwa lengo kujua namna ya kutambua na kupambana kudhibiti bidhaa bandia sokoni.
Akizungumza na waandishi wa habari Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini, Costantine Kanyasu mara baada ya kutembelea kliniki ya biashara inayojumuisha taasisi mbalimbali za Serikali ikiwemo FCC katika Maonesho ya Sita ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika viwanja vya EPZA Bombambili mkoani Geita.
“Mnafanya kazi nzuri na kila mtu anaona, naomba muendelee kutoa elimu katika jamii ili iweze kuelewa shughuli mnazozifanya kama za masuala ya ushindani na bidhaa bandia kwa sababu bado watu wengi hawana uelewa wa kutosha,” amesema Kanyasu.
Ofisa Uhusiano Mkuu wa FCC, Nsajigwa Wilfred, amesema wamekuwa wakishiriki kwenye maonesho hayo na mengine ili kutoa elimu kwa umma uweze kukitambua chombo hicho na shughuli wanazozifanya za kulinda ushindani katika kibiashara na kumlinda mlaji.
“Tunakuhakikisha majukumu tuliyonayo kisheria yanatekelezwa kwa ufanisi, tunahakikisha kwamba mlaji na mtumiaji wa bidhaa analindwa na kudhibiti uwepo wa bidhaa bandia katika soko la nchi yetu.
“Tunajua mheshimiwa unashiriki vikao vya kamati ya ushauri ngazi ya mkoa na halmashauri yako na wabunge wengine pia watusaidie kutupatia nafasi ya kuja kutoa elimu,” amesema Nsajigwa.
Ofisa Mkaguzi na Mfuatiliaji wa Bidhaa Bandia Kanda ya Ziwa, Mgasi Kalindimya, amesema wanatumia maonesho hayo kuwaelimisha Watanzania kuhusu masuala mbalimbali yakiwemo ya bidhaa bandia, ushindani sokoni na namna ya kupata mitaji na teknolojia mpya.
“Tunatoa elimu tunawaasa wasikimbilie kwenye taasisi za mitaani wa sababu kuna kitu kinaitwa kausha damu wengi wanakuja bandani wanalalamika sana, wamekopa wananyang’anywa mali zao, sisi tunawashauri waende kwenye taasisi zinazotambulika kisheria,” amesema Kalindimya.
Aidha amewataka wazalishaji kufanya kazi kwa karibu na tume hiyo ili kuhakikisha bidhaa bandia haziingii sokoni na kusisitiza kuzalisha bidhaa ambazo hazitaigwa na wengine.
Katika maonesho hayo tume hiyo inatoa elimu kwa umma jinsi ya kutambua bidhaa bandia na kuwataka Watanzania kuchukua hatua kujiepusha nazo kwa sababu zina athari kwa afya, zinahatarisha usalama wa mali na maisha na zinaongeza umaskini kwa kulazimu kuzinunua mara kwa mara kutokana na kuharibika haraka.
More Stories
Gavu aanika miradi iliyotekelezwa na Serikali ya awamu ya sita Geita
RC Makongoro: Samia aungwe mkono nishati safi ya kupikia
TAKUKURU,rafiki yanufaisha wananchi Mwanza