December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbunge Fyandomo kuwatembelea mabinti wenye ulemavu kubaini uhitaji wa taulo za kike


Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya

KATIKA kutambua umuhimu wasichana wenye ulemavu waliopo mashuleni jamii imeombwa kujitoa kuwasaidia kuwapatia taulo za kike kutokana na baadhi yao kutoka kwenye familia duni .

Akizungumza na gazeti hili jana kuhusu uhitaji wa taulo za kike kwa wasichana wenye ulemavu Mbunge wa Vitimaalum mkoa wa Mbeya ,Suma Fyandomno amesema kuwa mabinti walio wengi wenye ulemavu wanakuwa katika kipindi kigumu kutokana na familia zao kutojiweza.

Aidha Mbunge huyo amesema kuwa ameweka mikakati ya kupita wilaya zote za mkoa wa Mbeya   ili kubaini  uhitaji  wa taulo kwa mabinti wenye ulemavu.

“Ndugu yangu hili suala nimepanga kufanya ziara baada ya Bunge la bajeti kuisha ,nitafanya hivyo kuona uhitaji wa watoto hawa maana nao ni sehemu ya jamii , nitaanza kupita mashuleni kasha kwenye kata kwa kushirikiana na maafisa maendeleo ya jamii wilaya na kata maana hawa ndugu zetu ndo wanashinda kwenye maeneo ya wananchi na mashuleni  na wanajua ukubwa wa tatizo”amesema Mbunge huyo .

Hata hivyo Fyandomo amesema kuwa katika kuhakikisha kuwa anatembelea wananchi alifanya ziara ya kutembelea hospitali na kupeleka taulo za kike ,sabuni ,Pampers kwenye wodi za wanawake katika hospitali za wilaya ya Kyela na Rungwe .

Akielezea zaidi Mbunge Fyandomo amesema kwamba kwenye shule za watoto wenye ulemavu Katumba(2) iliyopo Rungwe hajaweza kupita kufanya tathimini hiyo sababu hao ni watoto si mabinti .

“Nitapita upya kufanya tathimini ili kujua endapo pana uhitaji  ili niweze kusaidia kundi hili la mabinti wenye ulemavu ili waweze kupata elimu bora na hata waliopo majumbani waweze kujisikia kuwa na amani na kuona jamii inawajali “amesema.

Hawa Kihwele ni Diwani wa Kata ya Igurusi ,amesema kuwa ni muhimu kuzingatia upungufu wa viungo  vya watu wenye ulemavu na kwamba halmashauri zote ni pana na zina taasisi ambazo zinazalisha taulo za kike hivyo ni kuzifuatilia na kuhakikisha  wasichana  na hasa watu wenye ulemavu  wanapata  muda wote na kuwa na akiba pamoja na kuwatembelea na kuwaachia taulo .

Kwa upande Mkurugenzi wa shirika la Sauti ya Mama ,Thabita Bughali amesema kuwa shirika hilo limekuwa likiwatembelea mabinti wenye ulemavu mashuleni na majumbani kuwapa elimu namna ya kujistiri kutokana na kila binti alivyo na ulemavu wake pamoja na na kuwapatia taulo za kike.