Na Heri Shaaban, TimesMajira Online, Ilala
Mbunge wa Jimbo la Segerea, Bonnah Ladslaus Kamoli, amesema Daraja la Majoka katika Kata ya Kinyerezi likijengwa chini ya kiwango wananchi walikatae kutokana na Mkandarasi wa Kampuni ya Mabibo Construction kulalamikiwa kwa kudaiwa kukosa vifaa vya ujenzi.
Mbunge Bonnah alipokea malalamiko ya wananchi wake katika ziara jimboni Segerea kuangalia miradi ya maendeleo ambapo alitembea Kata ya Kinyerezi, Kisukuru na Bonyokwa kuangalia miundombinu ya barabara.
“Nakuagiza Mhandisi wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) ndio wasimamizi wa barabara hizi, malalamiko ya wananchi mmeyasikia daraja hili likijengwa chini ya kiwango wananchi walikatae,” alisema Bonnah.
Mbunge Bonnah alisema Sh milioni 650 za serikali sio fedha ndogo hivyo ametaka vigezo vizingatiwe daraja lijengwe kwa viwango vya kisasa.
Awali James Kihiyo alitoa malalamiko kuhusiana na mkandarasi huyo akidai ujenzi huo unafanyika bila kuleta mchanga wala mawe yenye ubora na kuishauri Serikali kumuangalia mkandarasi huyo kwa karibu.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Kibaga, Hashim Gulana, amempongeza Mbunge Bonnah Ladslaus Kamoli kwa utekekezaji wa Ilani ya chama na kusimamia miradi ya maendeleo.
Mwenyekiti Gulana ameomba mkandarasi huyo achepue mto huo ambao umefauta makazi ya watu na kero nyingine ni barabara ya Msitu wa Nyuki kuelekea kwa masista ambapo amemuomba mbunge asikie kilio cha barabara hiyo.
Mhandisi wa TARURA Ilala, Injinia Legnard Mashanda, alisema Daraja la Majoka linajengwa na Mkandarasi Mabibo Construction Company Ltd kwa fedha ambazo ni mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji.
Alisema mradi ulianza Juni 2023 na kwamba utamalizika kwa muda wa miezi sita.Mhandisi Mashanda alisema kwa sasa mradi umefikia asilimia 8.12 na gharama za mradi ni Sh milioni 650.
Alisema litajengwa daraja la midomo mitatu yenye uwazi wa mitaa nne kwa tatu hivyo kufanya urefu wa daraja kuwa mita 13.2.
Aidha alisema kazi zingine zilizofanyika ni kusafisha mto urefu wa mita 200, kuchonga barabara na kuweka vifusi urefu wa kilomita moja.
More Stories
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa