December 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbunge akabidhi Mil.6 kwa vikundi vya wanawake Uyui

Na Allan Vicent, TimesMajira Online,Tabora

MBUNGE wa viti maalumu kupitia Jumuiya ya Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Mkoa wa Tabora Bi.Jackline Kainja leo amekabidhi mitaji ya biashara kiasi cha sh mil 6 kwa vikundi vya wanawake wa UWT vya wilaya ya Uyui.

Jumla ya vikundi 30 kutoka katika kata zote 30 za wilaya hiyo vimenufaika na fedha hizo ambazo zimelenga kuwawezesha kuanzisha miradi ya kiuchumi.

Akizungumza katika mkutano wa Baraza la UWT la wilaya hiyo Mbunge Kainja amesema ametoa kiasi cha sh 200,000 kwa kila kata kwa ajili ya kuanzisha miradi yao ya kiuchumi.

Amebainisha kuwa huu sio wakati wa kampeni bali ni wakati wa kujenga chama na kutekekeza ahadi alizotoa kwa wanawake wenzake wa CCM wa Mkoa huo.

Bi.Jackline ameomba vikundi vyote kutumia fedha hizo kwa lengo lililokusudiwa ili kuinua Jumuiya hiyo ikiwemo kujiongeza kipato na hatimaye kujikwamua kiuchumi.

Amesisitiza kuwa huo ni mwanzo tu, anajiandaa kufanya ziara maalumu ya kutembelea kata zote katika wilaya hiyo ili kujionea maendeleo ya miradi yao.

Aidha amewataka wanawake wote wa CCM kumsemea vizuri Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ili aendelee kutekekeza ilani kwa nguvu zake zote na kuwaletea maendeleo.

Mbunge Jackline Kainja (kulia) akikabidhi kitita cha sh mil 6 kwa Mwenyekiti wa UWT wilaya ya Uyui Hamida Maarifa kwa ajili ya kuanzisha miradi yao ya kiuchumi.