November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbunge aahidi kufikisha sakata la tembo serikalini

Na Esther Macha,Timesmajira Online. Mbarali

MBUNGE wa Jimbo la Mbarali, Francis Mtega amefika katika vijiji vitano vya Kata ya Igava vilivyovamiwa na tembo 100 na kuharibu mashamba ya mazao ya mahindi na kusema tatizo hilo ni kubwa atalifikisha serikalini.

Mtega amesema kuna uwezekano wanyama hao wamekuwa wengi kwenye Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, kiasi kwamba maeneo yao yamekuwa hayatoshelezi mahitaji yao hali inayowafanya waingie kwenye mashamba ya wananchi.

Mbunge huyo amesema kutokana na ongezeko la wananchi katika wilaya hiyo, waliamua kuiomba serikali isogeze mipaka ya hifadhi hiyo ili wananchi wapate maeneo kwa ajili ya kilimo na shughuli nyingine za kiuchumi.

“Katika hali ya kawaida mtu unaweza ukachanganyikiwa, umetumia gharama kubwa kutunza mazao ukitegemea utavuna halafu mazao yanapotea, inauma sana, mimi kama mwakilishi wenu isingeweza kuingia akilini niendelee na vikao vya Bunge, wakati wananchi mnakufa njaa,” amesema.

Hata hivyo amesema, atawaomba wataalamu wawashauri wananchi hao namna ya kufanya ili kukabiliana na wanyama hao, ambao wamekuwa wakisababisha hasara kubwa kwa wananchi na kwamba uharibifu uliofanywa ni ushahidi tosha kwamba maeneo hayatoshi.

Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Kata, Gaitan Madindo amesema tembo hao wanadaiwa kutoroka katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na kuharibu mashamba ya mahindi, mpunga na viazi vitamu ambayo ndiyo mazao yanayotegemewa na wananchi hao kwa chakula na biashara.

Madindo amesema, tembo hao wameharibu ekari zaidi ya 400 za mazao hayo huku akidai hakuna madhara yaliyotokea kwa binadamu na makazi yao.

Amesema Maofisa wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), walifika katika maeneo hayo kwa ajili ya kufanya tathmini ya uharibifu uliofanywa na wanyama hao pamoja na kuwaondoa ili kuokoa mazao.

Ofisa huyo amesema, tatizo lilotokea ni kiwango cha fidia ambacho wataalamu hao waliwaambia wananchi kuwa watalipwa kwa maelezo kuwa kiwango hicho, kilizua mgogoro mwingine kutokana na kutoendana na uhalisia.

“Maofisa hao walisema, serikali itawalipa fidia wananchi hao kila ekari moja sh. 20,000 lakini hawajaridhishwa na kiwango hicho kwa sababu wanadai hakiendani na gharama walizotumia kwenye kilimo,” amesema.

Naye Diwani wa Kata hiyo, Nasoro Udes amemuomba Mbunge Mtega, kuwasaidiwa wananchi hao walipwe fidia haraka ili wanunue chakula kwa wakulima wa maeneo mengine ambayo hayajaathirika.

Amesema mara nyingi wakulima, huwa wanapata shida na serikali kutakiwa kuwalipa fidia lakini fidia hizo hazitolewi kwa muda mwafaka na hivyo, kuwafanya wananchi waendelee kupata shida.

Akizungumzia hali hiyo Ofisa Maliasili kutoka TANAPA, Helen Mchati ambaye anaongoza kikosi kazi kilichotumwa na Wizara ya Maliasili na Utalii wilayani humo kuwaondoa tembo hao, amewataka wananchi hao kuwa watulivu wakati kikosi hicho kikiendelea kufanya kazi.

Amewataka wananchi kutumia pilipili kwa ajili ya kuwafukuza tembo hao kwenye mashamba kama ambavyo wanapatiwa elimu na wataalamu.

Amesema mpaka sasa wameshatimiza siku tano kwenye mashamba, hayo wakilinda usiku na mchana huku akiwataka wananchi kuepuka kupita mashambani nyakati za usiku kwa maelezo kuwa maofisa hao, wanatumia silaha za moto.