Moses Ng’wat,Timesmajiraonline,Songwe.
SERIKALI Mkoa wa Songwe imewanasa watu watano, wakiwemo viongozi vyama vya msingi vya Ushirika wa Kilimo na Masoko (AMCOS) wakihusishwa na tuhuma za kujipatia mbolea ya ruzuku kwa njia ya udanganyifu mifuko 8,738 na kuiuza kwa wakulima kwa bei ya kulangua kinyume na mpango wa serikali.
Taarifa ya kukamatwa kwa watuhumiwa hao imetolewa leo ,Januari 12, 2024 na Mkuu wa mkoa wa Songwe, Dkt. Francis Michael, ikiwa ni muendelezo wa operesheni ya kikosi kazi kilichoundwa na Mkuu huyo wa mkoa kwa lengo la kufuatilia mwenendo wa utoaji ruzuku ya mbolea kupitia mfumo wa kidijitali na kuisambaza kwa wakulima kwa bei elekezi ya serikali.
Alimtaja mtuhumiwa wa kwanza kuwa ni Omary Hashimu ambaye anahusishwa na watuhumiwa wengine watatu ambao ni wafanyabiashara waliokamatwa awali na baadhi yao kufikishwa mahakamani kwa kujipatia mifuko 74,000 ya mbolea kinyume cha utaratibu na kuiuza nje ya mfumo wa serikali.
Mtuhumiwa wa pili aliyetajwa na Mkuu wa Mkoa ni Rashid Msyaliha, ambaye ni Mwenyekiti wa chama cha ushirika wa Kilimi na Masoko (AMCOS) cha Ilomba, Wilayani Mbozi, ambapo alikutwa na mifuko 2,907.
“Mwenyekiti huyu wa Amcos ya Ilomba ambaye tunaendelea kumshikilia na yupo chini ya ulinzi na wenzake , amebainika na makossa kadhaa, ikiwemo kununua au kutoa mifuko 624 ya mbolea ya ruzuku kwa kutumia namba ya ruzuku bila ridhaa ya bodi na wanachama wa Amcos na kuiuza kwa bei ya juu”.
Akifafanua Zaidi, Mkuu wa Mkoa Dkt. Michael alisema mtuhumiwa huyo pia alitumia udanganyifu na kujiandikisha kama mkulima wa kijiji cha Ilomba na kusajili shamba lenye ukubwa wa ekari 1000 na kujipatia mbolea ya ruzuku mifuko 2096 na kuiuza nje ya mfumo.
“Kama haitoshi Mwenyekiti huyu wa Amcos pia alitoa taarifa za uongo kuwa ana shamba lingine la ekari 100 katika kijiji hicho cha Ilomba na kujinufaisha na mifuko mingine ya ziada 187 ya mbolea ya ruzuku na kuiuza nje ya mfumo” alifafanua Mkuu wa Mkoa Dkt. Michael.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa aliwataja watuhumiwa wengine waliokamatwa kuwa ni viongozi watatu wa Idunda Amcos iliyopo Wilayani Mbozi ambapo wamekutwa na makosa mbalimbali ikiwemo makossa ya jinai.
Aliwataja viongozi hao kuwa ni Mwenyekiti wa Amcos hiyo, Yisega Mwazembe, Bahati Mwazembe, pamoja na Sikuzan Mwashwa ambaye ni mhasibu wa kikundi.
“Viongozi hawa wa Idunda AMCOS tuhuma zao ni kununua na kutoa mifuko 5831 ya mbolea kwa kutumia namba ya ruzuku ya Amcos bila ridhaa ya bodi na wanachama na mifuko hiyo haikuwafikia wakulima haikujulikana ilipelekwa wapi” alisema Skt.Michael.
Alisema katika ufuatiliaji zaidi kikosi kasi hicho kilibaini kuwa namba hiyo ya usajili ya AMCOS ilitumia jina la Mwenyekiti wa AMCOS ambapo ni kosa la jinai, huku viongozi hao pia wakidaiwa kutoa taarifa za uongo na kusajili shamba hewa lenye ukubwa wa ekari 1000.
Mkuu wa mkoa Dkt. Michael amesema watuhumiwa wote watano wanaendelea kushikiliwa katika kituo cha polisi Vwawa, Wilayani Mbozi na upelelezi ukikamilika watafikishwa mahakamani.
Aidha, Mkuu wa Mkoa alibainisha kuwa, hadi kufikia sasa kikosi kazi hicho alichokiunda kimekamata mifuko ya mbolea ya ruzuku 100,019 na kwamba operesheni hiyo itakuwa endelevu.
More Stories
Mashirikisho yaunga mkono azimio mkutano mkuu CCM
Watumishi wa Mahakama waonywa
CCM ilivyotambua mchango wa wanahabari Mkutano Mkuu Maalum