WANYAMAPORI ni urithi wa asili wa mazingira pekee na raslimali yenye umuhimu mkubwa kitaifa na kimataifa kutokana na thamani yake ya kiuchumi na uwezo wake katika kuchangia kwenye maendeleo endelevu.
Tanzania ina idadi kubwa ya anuwai za wanyama na mimea, ikiwa ni pamoja na spishi ndogo na spishi kuu ambazo hupatikana kwa nadra sana ikiwemo mbwa mwitu; faru weusi, duma, tembo wa Afrika, nyumbu, pundamilia, twiga, nyati, chui, na simba ambao ni muhimu katika muktadha wa kimataifa.
Mtandao wa maeneo yaliyohifadhiwa kwa ajili ya uhifadhi wa wanyamapori ndiyo msingi wa tasnia ya matumizi endelevu ya wanyamapori inayojumuisha kutazama wanyama, uwindaji wa kitalii, uwindaji wa wakazi, pamoja na ufugaji wa wanyamapori.
Pamoja na tasnia kuwa hiyo na mchango mkubwa katika uchumi kwa taifa, inaelezwa kuwa sekta ya wanyamapori nchini haijaweza kuendelezwa nchini kufikia na uwezo wake kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo Kupotea au kutoweka kwa makazi ya wanyamapori kutokana na makazi ya watu, kilimo, malisho ya mifugo, uchimbaji migodi na ukataji miti.
Aidha inaelezwa kuwa kuongezeka kwa ujangili kwa kasi kubwa na biashara isiyo halali, kutokuwepo na uwezo wa kutosha wa kuwadhibiti wanyama wakali na waharibifu pamoja na upungufu wa watendaji wa kuendesha shughuli za kuhifadhi wanyamapori, ni miongoni mwa sababu nyingine zinazosababisha kudumaa kwa sekta ya wanyamampori nchini.
Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali imeweka sera, mikakati na mipango mbalimbali ili kuweka udhibiti na uendeshaji wa shughuli za wanyamapori na usimamizi wa rasilimali zake nchini.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Hamisi Kigwangalla anasema Serikali kupitia Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania inatekeleza jukumu la kusimamia, na kuratibu utafiti na uhifadhi endelevu wa wanyamapori kwa kutumia matokeo ya utafiti wa kisayansi.
Anasema taasisi hiyo imeendelea kutekeleza miradi ikiwemo ya utafiti wa mbwa mwitu, na utafiti wa magonjwa ya kimeta, homa ya vipindi na kifua kikuu pamoja na utafiti wa mfumo wa ikolojia katika hifadhi ya Serengeti unavyofanya kazi na manufaa yake kwa jamii, pamoja na utafiti wa mahusiano ya nyuki na mimea na sensa za wanyamapori.
“Mbwa mwitu wapo katika tishio la kutoweka hapa nchini, ambapo utafiti katika mfumo ikolojia ya Serengeti umeendelea kwa kufuatilia makundi 24 yenye jumla ya mbwa mwitu 277, makundi hayo yanatumia maeneo ya Hifadhi za Serengeti, Ngorongoro, Mapori ya Akiba Maswa na Ikorongo/Grumeti, Mapori Tengefu Loliondo na Ziwa Natron, na maeneo ya Selela na Engaruka” anasema Dkt. Kigwangalla.
Kwa mujibu wa Dkt.Kigwangalla anasema malengo ya utafiti huo ni kurejesha uwiano wa kiikolojia unaotokana na mchango wa wanyama hao ambao miaka ya 1990 walitoweka katika Mfumo wa Ikolojia ya hifadhi ya Serengeti, kutokana na ugonjwa wa kifafa cha kanivora na hivyo Serikali imeendelea kuelimisha jamii za wafugaji kuhusu jinsi ya kujilinda dhidi ya mbwa mwitu.
Aidha Waziri Kigwangalla anasema wizara yake pia imefanya utafiti kuhusu kuhusu mfumo ikolojia wa hifadhi ya Serengeti katika kuhimili ongezeko la tembo katika kipindi cha miaka 50 ijayo, ambapo matokeo ya utafiti huo yanatarajia kutolewa katika mwaka wa fedha 2018/2019 na yanatarajia kusaidia kubaini aina ya mifugo ambayo haiendani na malisho katika eneo hilo.
Akifafanua zaidi, Dkt.Kigwangalla anasema kutokana na na kuwepo kwa taarifa za vifo vya mifugo 236,437 ikiwemo ng’ombe 77,889, Kondoo 78,490, Mbuzi 72,881 na Punda 7,177 katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, taasisi ya utafiti wa wanyamapori imefanya uchunguzi na kubaini kuwa vifo vya mifugo hiyo vilisababishwa na ukame, magonjwa na wingi wa mifugo kuliko uwezo wa eneo.
Anaongeza kuwa mbali na madhara kwa mifugo, pia ugonjwa wa kimeta kwa mifugo umesababisha madhara makubwa kwa jamii ya wafugaji waliokula nyama ya mifugo hiyo, ambapo kati ya watu 240 240 waliougua kimeta 18 kati yao walifariki, ambapo Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imechukua hatua ya kutoa chanjo kwa mifugo yote na kuwaelimisha wafugaji.
Kigwangalla anasema Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori imeendelea na utafiti wa mimea na nyuki wanaouma na wasiouma katika Wilaya 120 na taarifa ya awali ya utafiti huo yametumika kuchora ramani ya kiikolojia inayoonesha kanda muhimu za ufugaji nyuki nchini.
Ili kulinda na kusimamia sekta ya wanyamapori nchini, Serikali imeendelea kuchukua hatua kadhaa ikiwemo kuandaa mpango madhubuti wa kusimamia na kudhibiti uendeshaji wa biashara ya wanyamapori hai lengo la kuongeza uratibu na usimamizi kwa karibu kazi ya ukamataji wa wanyamapori hai.
Aidha Serikali imeendelea kusimamia Sheria ili kudhibiti uingizaji wa mifugo ndani ya maeneo ya hifadhi za wanyamapori na misitu kinyume cha sharia, hatua iliyokusudia kurejesha uoto wa asili katika maeneo mbalimbali na kuimarisha ustawi wa wanyamapori.
Ushirikiano baina ya Serikali, sekta binafsi na wanachi ni kiungo muhimu katika kufanikisha azma ya kuwa na mikakati ya pamoja katika kukabiliana na uvunaji na usafirishaji haramu wa wanyamapori waliopo hatarini kutoweka.
More Stories
Boost ilivyoboresha miundombinu ya elimu Ilemela
Samia apongeza walimu 5,000 kupatiwa mitungi ya gesi, majiko kutoka Oryx
Uwekezaji kwenye kilimo utatimiza ndoto ya Samia ya nchi kuwa ghala la chakula Afrika