Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Bumbuli
BAADHI ya wanawake wa Halmashauri ya Bumbuli wamesema wameanza kunufaika baada ya mbegu za nyanya na mahindi walizopewa na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga Mhandisi Mwanaisha Ulenge kuanza kutoa mazao.
Wamesema mbegu ya mahindi aina ya Stuka imekuwa ni bora kwenye ukanda wa milima, na imekuwa ni bora kwa kuweza kuzalisha mbegu nyingine baada ya kuvuna, kwani aina nyingine za mahindi, huwezi kuvuna halafu ukahifadhi kama mbegu kwa msimu mwingine.
Waliyasema hayo Julai 23, 2024 mbele ya Mhandisi Ulenge kwenye kikao cha Baraza la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Lushoto waliopo Jimbo la Bumbuli.
“Tunashukuru kwa kupata mbegu ya mahindi ya stuka,Mbegu hii ni nzuri kwa kuzalisha mazao mazuri,Lakini wataalamu wanasema mbegu za aina nyingine za mahindi ukivuna, huwezi kuhifadhi kama mbegu, lakini mbegu ya stuka, unaweza kuitumia hata miaka 100 unaweza kuvuna na kuhifadhi mbegu” amesema Beatrice Hizza Katibu wa UWT Kata ya Mayo.
Naye Ziada Kanju,Katibu UWT Kata ya Usambara amesema baada ya kupewa mbegu za nyanya na Mhandisi Ulenge, yeye na wanawake wa kata hiyo wanajishughulisha na kilimo cha vitivo (mashamba madogo), na wamefanikiwa kupanda nyanya hizo, na wanakaribia kuvuna.
“Tunashukuru kwa Mbunge Ulenge kuweza kutupatia mbegu za nyanya, mimi na wanawake wenzangu Kata ya Usambara tumepanda nyanya, na wakati wowote tutaanza kuvuna” amesema Kanju.
Akizungumza kwenye kikao hicho, Mhandisi Ulenge amewataka wanawake hao kuchangamkia fursa za mikopo inayotolewa na Serikali kupitia benki, lakini pia Benki ya CRDB ina program ya kukopesha wanawake bila riba kupitia Imbeju.
“Changamkieni fursa ya mikopo ili muweze kuendeleza shughuli zenu ikiwemo kilimo, ufugaji wa ng’ombe wa kisasa, ujasiriamali, biashara na kubuni bidhaa mbalimbali. Na sasa hivi kuna mikopo ya Serikali kupitia benki, lakini kupitia Benki ya CRDB kuna mikopo inatolewa kupitia Imbeju, hivyo msije mkaacha hizi pesa” amesema Mhandisi Ulenge.
Mhandisi Ulenge ili kujiridhisha na mbegu alizotoa ikiwemo mpunga, ngano, maharage, nyanya, na mahindi, alikwenda Kijiji cha Kwanguruwe, Kata ya Bumbuli alikwenda kuona kitivo cha nyanya kutoka kwa wakulima wanawake wa kijiji hicho.
More Stories
Kiswaga:Magu imepokea bilioni 143, utekelezaji miradi
Zaidi ya milioni 600 kupeleka umeme Kisiwa cha Ijinga
Kamishna Hifadhi ya Ngorongoro atakiwa kupanua wigo wa Utalii nchini