December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbaroni kwa tuhuma za kumuua mpenzi wa binti yake kwa sumu

Na Moses Ng’wat,Timesmajiraonline, Songwe.

JESHI la Polisi Mkoa wa Songwe linamshikilia baba kwa tuhuma za kumuua mpenzi wa mtoto wake kwa kumnywesa sumu inayodhaniwa kuwa ni ya kuulia panya.

Mtuhumiwa huyo, Mitedi Mwambughi (63), anadaiwa kumnywesa sumu, Christopher Mwamengo (23), ambaye inadaiwa kuwa alikuwa ni mpenzi wa mtoto wake,Faustina Mitedi (19), aliyemaliza kidato cha sita na alikuwa akisubiria kujiunga na chuo.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Rashid Ngonyani, amesema tukio hilo lilitokea Septemba 13, 2023 katika kijiji cha Ikonya, Kata ya Bara, Wilaya ya Mbozi, Mkoani hapa.

Kaimu kamanda Ngonyani amesema mtuhumiwa huyo alichukua uamuzi wa kumywesha sumu marehemu ili kulipiza kisasi baada ya kumtuhumu marehemu kumtorosha binti yake na kuishi nae kinyumba kwa zaidi ya siku mbili bila ridhaa yake.

“Mbinu aliyotumika mtuhumiwa kutekeleza mauaji hayo ni kumtumia binti yake kumuita marehemu nyumbani kwake kwa lengo la kumuuliza kwanini alimchukua binti yake bila ridhaa yake ndipo alipompatia sumu,”amefafanua.

Kaimu Kamanda Ngonyani amesema kuwa baada ya marehemu kupatiwa sumu alianza kujisikia vibaya na baadae kukimbizwa hospitali kabla ambapo wakati anaendelea na matibabu alifariki.

“Tumefanya uchunguzi wa awali kwa kushirikiana na madaktari wa Hospitali ya Wilaya na sampuli zimepelekwa kwa mkemia mkuu wa serikali ili kubaini ni sumu ya aina gani ambayo marehemu alilishwa,” amefafanua Ngonyani.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Mbozi, Dkt. Kelvin Masea, amethibitisha marehemu kupokelewa katika Hospitali hiyo na kwamba alifikishwa hospitalini hapo Septemba 13, 2023 majira ya saa 3:00 usiku na alinza kupatiwa na ndani ya saa mbili alikuwa amepoteza maisha.

“Marehemu alipokelewa hapa (Hospitali ya Wilaya ya Mbozi) akiwa mahututi hajitambui na daktari wa zamu alimuhudumia kwa saa mbili tuu kabla hajapoteza uhai wake” amesema Mganga Mfawidhi Masea.

Amesema timu ya madaktari katika hospitali hiyo wakishirikiana na jeshi la polisi walifanya uchunguzi wa awali kwa kuchukua sampuli ambazo zimepelekwa kwa mkemia mkuu wa serikali.