November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Matumizi ya FEFO yanavyozuia athari kwa mtoto tumboni na baada ya kuzaliwa

Joyce Kasiki

Lishe bora kwa mama mjamzito ni muhimu kwa kumpatia mama virutubishi muhimu ambavyo vitamsaidia yeye pamoja na mtoto na hivyo kumsaidia mtoto kukua vizuri kimwili na kiakili.

Ukosefu wa lishe bora wakati wa ujauzito huweza kusababisha matatizo ya kiafya kama vile mama kutoongezeka uzito kama inavyotakiwa na hivyo kukosa nguvu kipindi cha ujauzito na wakati wa kujifungua jambo ambalo ni hatari kwa mama na mtoto aliye tumboni.

Athari zinazoweza kujitokeza ni pamoja na mtoto kuzaliwa na udumavu,kuzaliwa mtoto njiti au mwenye uzito pungufu,mimba kutoka ,uwezekano wa kuzaliwa mtoto mwenye tatizo la kichwa kikubwa ,mdomo sungura na mgongo wazi ambazo ni hatari kwa malezi,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto na hivyo kuhatarisha ukuaji wake kwa ujumla.

Kwa kuona changamoto za malezi ,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto ,Serikali kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali ilizindua Programu Jumuishi ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto  iliyomlenga mtoto mwenye umri wa kuanzia miaka  0-8 ili kuhakikisha watoto wanafikia ukuaji timilifu na kuwa na tija katika Taifa.

Programu hiyo inahimiza wananchi kuangazia mambo muhimu matano katika malezi,makuzi ambayo ni afya bora tangu mama mjamzito mpaka mtoto anapofikisha umri wa miaka minane .

Hivyo, suala afya bora ya mama mjamzito na mtoto aliyepo tumboni na kuzaliwa kwa mtoto aliyekamilika,linachangiwa kwa kiasi kikubwa na matumizi ya dawa za kuongeza damu aina ya FEFO yenye mchanganyiko wa madini ya chuma na folic acid ‘foliki asidi ‘.

Hivyo mama mjamzito anaweza kuzuia hatari zinazoweza kujitokeza kwake na kwa mtoto kwa kuzingatia mambo mbalimbali ambapo pamoja na mambo mengine ni pamoja na kumeza  vidonge vya FEFO kila siku kwa kipindi chote cha ujauzito.

Licha ya kupungua kwa vifo vya akinamama wajawazito na watoto wa umri wa chini ya miaka mitano ,lakini bado serikali inaendelea kufanya jitihada  mbalimbali za kupunguza vifo hivyo kwa kutekeleza afua mbalimbali.

Mkurugenzi Msaidizi huduma za Lishe Wizara ya Afya Neema Joshua anasema mjamzito anatakiwa awe na folic ya kutosha kabla ya ujauzito huku akisema hiyo inamaanisha , wanawake wote wenye umri wa kuzaa wanatakiwa watumie fefo ambayo ni muunganiko wa madini ya chuma na vitamini ya folic acid.

Anasema mama mjamzito anatakiwa aanze kutumia FEFO ambayo itamsaidia kuongeza damu ,kufanya uumbaji wa mtoto hasa katika miezi mitatu ya kwanza .

Kuhusu athari za kutotumia dawa hizo anasema inaweza kusababisha upungufu wa damu kwa mama mjamzito ambao utaathiri hata uwezo wakati wa kujifungua kwa kukosa nguvu ,anakuwa katika hatari ya kifo kwa kutokuwa na damu ya kutosha.

Athari nyingine ni  kujifungua mtoto njiti au uzito pungufu,mimba kutoka ,uwezekano wa kujifungua mtoto mwenye tatizo la kichwa kikubwa mdomo sungura na mgongo wazi.

Kwa mujibu wa Joshua,pia kunakuwa na athari kwa mtoto ambapo anaweza kuzaliwa na udumavu kwani hatokua vizuri .

Daktari Bingwa Mwandamizi ,Magonjwa ya akina mama na Uzazi ,Idara ya Afya ya Uzazi ,Mama na Mtoto ,Wizara ya Afya Sunday Dominico anasema ,bado elimu ya afya ya uzazi inahitajika ili kuunga mkono jitihada za serikali za kukabiliana na changamoto za afya ya uzazi na vifo vya akina mama wajawazito na watoto.

Anasema wanawake na wasichana wanapaswa kuwahi kliniki mara wanapohisi ni wajawazito ili waweze kupata huduma stahiki na kumnusuru mtoto .

Vile vile anawataka wajawazito kutotumia dawa bila kushauriwa na daktari kwani inaweza kuhatarisha usalama wa mtoto aliye tumboni.

Doris Mollel ni Mkurugenzi wa Doris Mollel Foundation,taasisi isiyo ya kiserikali  inayoangazia masuala ya watoto hususan watoto njiti anasema katika eneo la malezi na makuzi kuna mijadala mikubwa inaendelea duniani hasa wanaozaliwa kabla ya wakati kwamba wanasaidiwa watoke salama hospitali tu ,lakini hakuna anayefuatilia maisha yao baada ya kutoka hospitali.

“Kwa hiyo Shiria la Afya Duniani (WHO) limeanza kuandaa vifaa vya kuwasaidia nchi wanachama kufuatilia malezi na makuzi ya hawa watoto wanaozaliwa na changamoto,maana kwa sasa hakuna anayejua katika watoto 10 wanaoruhusiwa kwenda nyumbani ni wangapi wanaendelea kuishi au wanakua kama watoto wengine,

“Kuna ‘study’ inaendelea kufanyika mkoani Mbeya… ,katika watoto 10 wanaoruhusiwa kwenda nyumbani,watoto wawili hadi wanne ndiyo wanabaki hai wengine sita wanapoteza maisha,

“Lakini kuna study nyingine imefanyika nchini Uganda,katika hawa watoto 10 wanaoruhusiwa tisa wanapoteza maisha ,lakini pia bado hatujawekeza kujua wangapi wanapata changamoto ya ulemavu na ni ulemavu wa aina gani ambao unaongoza zaidi hasa wa hawa wanaozaliwa na uzito pungufu na kuzaliwa kabla ya wakati.”

Anasema nchi ikiweza kusaidia kila mama mjamzito akaweza kutumia ina maana tutaweza pia kupunguza idadi ya watu wenye ulemavu nchini.

Maria Joseph mkazi wa Dodoma mjini anasema yeye anazifahamu FEFO uwa ni dawa za kuongeza damu na wala hajui kama kutokuzitumia ndizo zinazosababisha kuzaliwa wa mtoto wmenye changamoto.

“Kwa hiyo kutokana na maelekezo amabyo huwa tunapewa kliniki ,mimi nilipokuwa mjamzito wa watoto wangu wote watatu sijawahi kutumia vidonge hivyo wa sababu huwa zinaipa kichefuchefu .”anasema Maria

Anaiomba Serikali kuhaikisha kila kituo cha klini kinatoa elimu sahihi juu ya matumizi ya FEFO ili kupunguza kuzaliwa kwa watoto wenye changamoto mbalimbali .

Kwa mujibu wa Waziri wa Afya Ummy Mwalimu  wakati akisoma hotuba ya bajeti bungeni kwa mwaka wa fedha wa 2024/2025,Wizara hiyo imeendelea kuimarisha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini ili kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030  ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kufikia chini ya 70 kwa kila vizazi hai 100,000, vifo vya watoto walio chini ya miaka mitano kufikia 25 kwa kila vizazi hai 1,000 na vifo vya watoto wachanga kufikia 12 kwa kila vizazi hai 1,000 ifikapo mwaka 2030.

Anasema  katika kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024,kumekuwa na mafanikio kwa  wajawazito waliohudhuria mahudhurio manne au zaidi huku akisema pamoja na mafanikio hayo lakini  bado mahudhurio ya kliniki ya wajawazito wenye umri wa mimba chini ya wiki 12 yameendelea kuwa katika kiwango cha chini kwa asilimia 44.4, sawa na wajawazito 822,194 ikilinganishwa na asilimia 40.7 katika kipindi kama hicho mwaka 2022/23.

 ‘Nitumie fursa hii kuwahimiza akinamama wajawazito kuanza kliniki mapema ili wataalam waweze kuwa na muda muafaka wa kutambua changamoto zinazohusiana na ujauzito na kujifungua na kuchukua hatua stahiki kwa wakati’.anasema Ummy

Anasema ,katika kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024, wajawazito waliopata dawa ya kuzuia upungufu wa damu (FEFO) walikuwa ni asilimia 96 ikilinganishwa na asilimia 92.5 katika kipindi kama hicho mwaka 2022/23.

 Aidha anasema , wajawazito 1,721,734 sawa na asilimia 88 walipimwa wingi wa damu ikilinganisha na wajawazito 1,419,137 sawa na asilimia 74.95 waliopimwa wingi wa damu kipindi kama hicho mwaka 2022/23 ambapo asilimia 1.8 ya waliopimwa walikutwa na upungufu mkubwa wa damu na kupatiwa matibabu.