January 12, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Matinyi awataka wakurugenzi kushirikisha waandishi wa habari kuisemea miradi ya Serikali

Na Esther Macha, TimesmajiraOnline,Mbeya

MSEMAJI mkuu wa serikali,Mobhare Matinyi amewataka wakurugenzi wote nchini kushirikisha waandishi wa habari na maafisa habari katika kutembelea miradi ya maendeleo pamoja na kuandaa mikutano ya hadhara na kuitolea taarifa.

Matinyi amesema hayo leo wakati wa mkutano na wakurugenzi wa halmashauri saba za mkoa wa Mbeya pamoja na waandishi wa habari ambapo lengo kuu la mkutano huo ni kueleza mafanikio katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Amesema kuwa kwa kazi kubwa inayofanywa na wakurugenzi wa halmashauri nchini ni muda muafaka kwao kuwa pamoja na waandishi wa habari na maafisa habari ili taarifa za kazi ziweze kufika kwa wananchi .

“Katika ngazi ya Mkoa taarifa huwa zinafika kwasababu ni Mkoa ambao upo katika Mji mkubwa na moja miji katika nchi yetu kuna vyombo vya habari vya kutosha hivyo”amesema.

Ameongeza kuwa ” Hakikisheni mnakuwa karibu na vyombo vya habari andaeni mikutano na kutoa taarifa za miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na serikali na kufanya ziara maalum kutembelea miradi na hiyo ndo itakuwa njia bora ya watanzania kujua nini serikali ya awamu ya sita inafanya “amesema Msemaji mkuu wa serikali.

Hata hivyo Matinyi amesema Mkoa wa Mbeya wa kimkakati katika nchi umekuwa ukipokea wafanyabiashara wa nchi nne ambazo ni , Malawi,Zambia,Congo pamoja na Zimbabwe huku alisema Mkoa wa Mbeya umefanya vizuri katika mazao ya biashara na upatikanaji wa madini ya dhahabu kutoka kilo 20 mpaka 300.

Awali akizungumzia kuhusu wanafunzi walioripoti Shule,Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Homera amesemampaka sasa wanafunzi walioripoti shule kuanza kidato cha kwanza ni asilimia 80,huku waliokatisha masomo zaidi ya 500 wamerudi shule kuendelea na masomo ili waweze kutimiza ndoto zao.

Aidha mkuu huyo wa mkoa amezungumzia kuhusu mapato ya mkoa na kusema kuwa wamekusanya zaidi ya Bil.36.7 kati ya Bil .49 ambazo wilaya za Chunya,Busokelo na Rungwe zinaongoza kwa makusanyo ya mapato.

Missana Kwangura ni mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Wilaya Mbarali amesema kuwa kwa miaka mitatu wamepokea zaidi ya Bil.90 .

Kwangura amesema kuwa sekta ya elimu msingi walipokea Bl.3.4 na kuwa shule za Msingi 139 na kuwa ndani ya miaka mitatu wameweza kuongeza shule 13 na hivyo kufikia shule 142 za msingi.