November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Matamasha Simba, Yanga Day yamkosha Waziri Ndumbaro

*Rais Samia azipongeza, Dalali afunguka kuanzisha Tamasha

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Dar

WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Damas Ndumbaro amefurahishwa ma Matamasha ya Simba Day na Siku ya Mwananchi yaliofanyika kwenye Dimba la Benjamini Mkapa jijini Dar es Salaam, Agosti 3 na 4 mwaka huu.

Matamasha hayo yamedhirisha ukubwa wa timu za Simba na Yanga hapa nchini, kutokana na kufurika na umati wa mashabiki wanaopenda mpira pamoja na timu hizo

Akizungumzia hilo mara baada ya kuhudhuria matamasha hayo yeye kama Waziri mwenye dhamana ya michezo amezipa kongole timu hizo kwani zimetuma salamu kwa nchi nyingine Barani Afrika kuwa Tanzania katika upande wa soka wapo vizuri.

“Mimi kama Waziri mwenye dhamana ya Michezo, siangalii Simba wala Yanga tu, naiangalia Tanzania, amekuja kiongozi wa Soka kutoka Uganda ameshanga ule umati wa Watu katika Simba Day.

“Nikamwambia ukija na kesho (jana) atakutana na umati mkubwa mwengine, hii ndio Tanzania. Simba na Yanga ndio alama za mpira wa Taifa hili.

“Mimi kama Waziri nimefurahi hicho kinachondelea kufanyika na vilabu vyetu, Mafanikio kwenye klabu ndio chanzo cha kufanya vizuri na ninachofurahi zaidi pia kwa sasa Simba na Yanga wanashindania mambo ya maana.

“Simba anashindania Sana michuano ya Afrika, halikadhalika na Yanga nae hivyo hivyo ,Simba walianzisha Simba Day na Yanga nae yumo kwenye Yanga Day,hayo ndio mafanikio utani wao sasa umekwenda kwenye mafanikio,” alisema Dkt. Ndumbaro.

Katika hatua nyingine Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amezipongeza klabu za Simba na Yanga kwa kufanikisha kuandaa Matamasha ya Simba Day, na Yanga Day. Agosti 3 na 4 yaliofanyika kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa.

Tamasha la Simba Day ni la 15 tangu kuanzishwa kwake na Field Marshall Mzee Hassan Dalali ambaye alikuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo.

Rais Samia alituma salamu zake na pongeza kwa klabu hiyo huku akiwa ujumbe wa yaliyopita sio ndwele, wagange yajayo.

“Hongera Simba na Wanasimba lakini pia Yanga SC kwa kufanikisha matamasha ya Simba Day na Yanga Day 2024. Nawatakia kila la kheri katika msimu mpya wa Ligi Kuu.

“Kwa upande wa Simba, Waswahili wanasema, yaliyopita si ndwele, lakini kwa Yanga ongezeni juhudi mufanye tena vizuri na msimu huu, ” alisema Rais Samia Suluhu Hassan.

Katika Tamasha la Simba Day, mashabiki wa timu hiyo waliongelea kiwango cha timu yao, baada ya kuiona kwa mara ya kwanza ikicheza dhidi ya APR ya Rwanda na kushinda mabao 2-0.

Magoli ya Simba SC, yalitiwa kimiani na kiungo fundi “Disconnector” Debora Fernandes Mavambo na Edwin Balua yote katika kipindi cha pili.