June 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mataifa 16 ulimwenguni kuiombea Tanzania amani kuelekea chaguzi zijazo

Na Lubango Mleka, TimesMajira Online, Igunga

MKUU wa Wilaya ya Igunga, Mkoani Tabora Sauda Mtondoo amefungua kongamano la siku Tatu linalofanyika katika kanisa la International Pentecostal Assembly’s of Good Igunga lenye lengo la kutoa mafunzo ya Uongozi yanayokwenda sambamba na maombezi ya kuiombea Tanzania kufanya uchaguzi ujao wa Serikali za mitaa kwa mwaka 2024 na 2025 kuwa wa amani na utulivu.

Kongamano hilo ambalo limehusisha Viongozi mbalimbali wa kanisa hilo walioungana kutoka mataifa 16 na kuunda umoja wa Viongozi ujulikanao kama Leadership Empowerment International Network (LEIN), Waumini wa kikristu kutoka maeneo ya Tanzania na nje ya Tanzania na Viongozi mbalimbali wa Serikali na Taasisi zisizo za Kiserikali.

DC Mtondoo ametumia nafasi hiyo kuwataka viongozi wa dini kuendelea kuhubiri amani, kwani lengo kuu la Serikali ni kuilinda amani. kufundisha maadili mema kwa watoto.

“hakuna namna tunavyoweza kushiriki katika shughuli zetu za Ibaada na shughuli zingine za kijamii kama hakuna amani, kwa hiyo jukumu la Serikali yoyote ni kuhakikisha kwamba amani inakuwa kipaumbele katika kuendesha mambo yake yote na mambo mengine yaende vizuri, nasisi Serikali ya Tanzania tunamshukuru Mungu na nyinyi viongozi wa dini kuendelea kutuombea na kuwa na amani, na kama inavyojulikana Tanzania ni kisiwa cha amani,”

” lakini pia nimeambiwa mtakuwa na mada mbalimbali zitakazo fundishwa, ikiwa na kuliombea Taifa na chaguzi zetu zijazo, nikianza na suala la uchaguzi kiongozi hapa amesema uongozi unatoka kwa Mungu, kama kanisa, kama LEIN mmeona kuweka hili mikononi mwa Mungu katika chaguzi zijazo ambazo tunaenda kuzifanya kama nchi kupitia maombi haya tunakwenda kupata viongozi bora kuanzia ngazi ya vitongoji mpaka vijiji na 2025 kuanzia ngazi ya kata, wabunge mpaka kumpata Mh. Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema DC Mtondoo.

Kwa upande wake Rais wa LEIN Bishop Dr. David Makimei kutoka nchini Kenya amesema kuwa LEIN ilianzishwa mwaka 2012 baada ya kufanyika kwa kongamono la kidini nchini DRC ambapo baadhi ya waandishi kutoka Kenya walifanya uchunguzi wa mambo mbalimbali nchini humo na mwaka 2013 wakafanya nchini Kenya, 2014 Tanzania, mwaka 2015 kongamano likafanyika Kampala Uganda, 2016 likafanyika tena nchini Tanzania, mwaka 2017 walikwenda Rwanda, mwaka 2018 makamu wa Rais wa sasa Reverend Bertin Binunu alijiunga na LEIN.

“Mwaka 2019, 2020 na 2021 hatukuweza kufanya kwa sababu ya janga la ugonjwa wa COVID – 19, tunamshukuru Mungu mwaka 2022 tukaanza tena safari yetu Congo ikatupokea na wawakirishi wao tunao leo hapa, mwaka 2023 tulianza vikao vya kuja tena Tanzania na leo 2024 tupo hapa wilaya ya Igunga mkoani Tabora nchini Tanzania, matarajio yetu mwakani 2025 kwenda Sudani Kusini nakama hatutafanikiwa basi tutafanya kongamano nchini Kenya, na kila mmoja wenu anakaribishwa kuwa mwanachama, ” akisema Dr. Makimei.

Huku Bishop Eusto Chanangula kutokea Songea Tanzania, akisema kuwa Matarajio yao baada ya kongamano, viongozi wengi watakuwa wamewezeshwa katika kuongoza na kutumika katika hali ya usahihi ya neno la Mungu, maana viongozi wanahitaji maarifa na ufahamu katika uongozi.

Naye Mchungaji mwenyeji wa kanisa la International Pentecostal Assembly’s of Good Igunga, Salome Shimba amesema kuwa, Ameweza kuandaa mkutano huu kwa maana ya kuombea Taifa la Tanzania kutokana na hali halisi tunayoelekea kwenye uchaguzi, wameona vyema kukaa makanisa ya Pentecostal Ulimwenguni na nchi 16 zimeshiriki, hapa Igunga yapo mataifa mbalimbali ya afrika kuiombea afrika amani hasa nchi ya Tanzania.

” Sisi Wachungaji hatushughulikii mambo ya kiroho pekee, lakini pia mambo ya kijamii zaidi, kwa mfano kesho tuna zoezi la kuchangia damu kwa ajili ya kuokoa maisha ya mama na mtoto waathirika wa ajali hii ikiwa na maana kanisa kurudisha shukrani kwa jamii, kongamano hili linatarajiwa kuisha siku ya jumamosi na jumapili tutakaa pamoja na kupanga nini mwakani tunakwenda kufanya,” akisema Mchungaji Shimba

Rais wa LEIN Bishop Dr. David Makimei (katikati) akiwa na baadhi ya Maskofu na wachungaji kutoka nchi 16 waliohudhuria ufunguzi wa kongamano la mafunzo ya Uongozi na kuombea chaguzi zijazo nchini Tanzania kufanyika kwa amani.
Maaskofu, Wachungaji na wawakirishi kutoka baadhi ya nchi 16 Ulimwenguni wakiwa mbele ya Kanisa la International Pentecostal Assembly’s of Good Igunga mjini wakiombea Taifa la Tanzania kuelekea katika chaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni na uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka 2025.
Waumini wa kanisa la International Pentecostal Assembly’s Of Good wakifuatilia kwa umakini somo la Uongozi kutoka kwa Rev. Omusolo Fred Sande kutoka nchini Uganda.
Rev. Omusolo Fred kutoka kanisa la Covenant Reformed Church kutoka Soroti nchini Uganda akifundisha somo la Uongozi katika kongamano lililoandaliwa na LEIN katika kanisa la International Pentecostal Assembly’s of Good mjini Igunga.