January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Sensa 2022, kusaidia kuimarisha usalama

Na Penina Malundo, timesmajira

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Hamad Masauni amesema kupatikana kwa takwimu za sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 zitasaidia kwa kiasi kikubwa uimarishaji wa usalama nchini huku kurahisisha waharifu kubainika kwa urahisi.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika mafunzo ya uwasilishaji ,usambazaji na uhamasishaji wa matumizi ya matokeo ya sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 kwa viongozi wa dini,amesema sensa ya mwaka 2022 ni ya kipekee kutokana na kuhusisha maeneo mengi ikiwemo Makazi ya watu tofauti na zilizopita za kuhesabu watu.

Amesema matokeo hayo ya sensa yataweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kupanga shughuli mbalimbali za nchi katika kuleta Maendele mradi o yake ikiwemo kwenye masuala ya kiusalama.

“Jambo la upekee katika sensa ya mwaka huu haikuhusisha tu kuhesabu watu bali imehusisha hadi Makazi ya Watu na Majengo ,ni jambo ambalo limetupa faraja kubwa kutokana na matokeo ya kusaidia kuhusisha usalama wa nchi yetu,”amesema na kuongeza

“Serikali ilikuwa katika hatua ya utekelezaji wa mambo mbalimbali ya kuimarisha usalama nchini hivyo basi matokeo haya ya sensa yalitokana na umuhimu wa kuhusisha maeneo matatu ikiwemo kuimarisha usalama nchini ili yawezw kufanikisha kwa urahisi,”amesema.

Aidha amesema dhamira ya dhati ya serikali ni kuhakikisha inakamilisha mchakato wake wa miradi ya kiusalama katika miji minne mikubwa ambapo inaanza na Mkoa wa Dar es Salaam, Dodoma,Mwanza na Arusha ambapo katika mradi huo utahusisha matumizi ya teknolojia ya kisasa katika kubaini uhalifu na wahalifu na kuweza kuwakabili kwa haraka.

Waziri Masauni amesema kwa namna hiyo nchi itaenda kufaidi matumizi ya takwimu ipasavyo kwa sababu itawezesha kufahamu kwa urahisi watu wale watakaofabya uhalifu kupatikana kiurahisi.

Kwa Upande wake Kamisaa wa Sensa 2022, Anne Makinda amesema kunaumuhimu wa sensa katika kufanya Maendeleo ya nchi na kutambua maeneo gani ambayo hayajapata kipaumbele yapewe kipaumbele.

Amesema mafunzo hayo wanayoyatoa kwa Makundi mbalimbali yamekuwa na msaada mkubwa kwa watu kwani wamekuwa wakielimisha juu ya uwepo wa ramani ya maeneo yao na kuonyesha kila kitu ambapo inasaidia sasa wananchi kuwajibika kimaendeleo katika maeneo yao.

“Sensa ya mwaka 2022 imemalizika,Sasa nchi inajiandaa na nyingine ambapo hii inatusaidia kuonyesha kwa uhalisia maeneo gani ambayo hayajapata kipaumbele katika maendeleo kwani kuna baadhi ya vijiji viliomba kujengewa shule lakini unakuta watoto ni wachache ,unakuta Kiongozi mmoja alikuwa na sauti hivyo Kila kitu kinaenda kwake,”amesema na kuongeza.

“Hivyo sasa maeneo ambayo hayajapata kipaumbele ndo yatapewa kipaumbele na hapo tutauliza sensa inasemaje katika kupeleka Maendeleo katika eneo hilo,”amesema.

Naye Mratibu wa Sensa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Kapala amesema mafunzo hayo yanafanyika kwa mujibu wa mwongozo wa kitaifa wa matumizi ya matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022.

“Mwongozo huo umeeleza mafunzo haya yafanyike kuanzia ngazi ya taifa hadi ya chini kabisa za utawala kwa makundi mbalimbali, ” amesema.

Aidha amesema mafunzo hayo yanamalengo matatu ambayo ni kuwaelimisha viongozi wa dini juu ya umuhimu wa matokeo ya sensa, kuwajulisha namna ya kupata na kusambaza matokeo ya sensa pamoja na kuwajengea uwezo kuhusu jinsi ya kutumia matokeo hayo katika kutekeleza mipango na shughuli mbalimbali za maendeleo.