Na.WAMJW,timesmajira,Morogoro
WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima amepiga marufuku utaratibu wa kuwauzia kadi za kliniki akina mama wajawazito pamoja na zile za watoto baada ya kuzaliwa wanapopelekwa kliniki za chanjo kwani ni kinyume na mwongozo wa serikali.
Dkt. Gwajima Ameyasema hayo jana mjini Morogoro alipokuwa akiongea na timu ya wataalamu wa afya halmashauri na mkoa huo kwenye kikao cha kujadili changamoto za afya ya uzazi, mama na mtoto.
“Nimekua nikipokea malalamiko mengi toka sehemu mbalimbali ya nchi kwamba mama mjamzito au mama akijifungua kadi ya kiliniki wanauziwa kutoka vituo vyetu vya kutolea huduma za afya, hii hapana”. Amesema
Hata hivyo Waziri huyo amesema amebaini ni kweli kadi hizo zinauzwa Jambo ambalo siyo maelekezo ya serikali bali ni utaratibu binafsi wa baadhi ya viongozi wa afya na watumishi wasio na mapenzi mema kwa serikali na wananchi.
Aidha, amesema kufanya hivyo ni kukosa ubunifu na uwezo katika kukabiliana na changamoto za kawaida kabisa mahala pa kazi na hivyo kuwataka watumishi hao kutatua changamoto hiyo kwani gharama za kupata kadi hizo ziko ndani ya uwezo wa halmashauri kitu ambacho wanaweza kuondoa uhaba huo katika maeneo yao bila kusubiri .
Amezitaka pia halmashauri zote nchini kuanzia leo kupata ufumbuzi wa ukosefu wa kadi hizo na asisikie tena malalamiko kutoka kwa akina mama wanaofika kliniki kwani Serikali haitaki kuwaona akina mama wajawazito na Watoto chini ya miaka mitano wanapata shida hizo.
More Stories
Wizara ya madini yakusanya bil.521 nusu ya kwanza mwaka wa fedha 2024/25
Meya awafunda wenyeviti Serikali za Mitaa
Mgeja aipongeza CCM kwa uteuzi Wagombea Urais