January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Marufuku kuagiza vikombe (Insulators) kutoka nje ya nchi -Dkt.Kalemani

Na Teresia Mhagama,TimesMajira online,Dar

WAZIRI wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani amepiga marufuku uagizaji wa vikombe (insulators) kutoka nje ya nchi baada ya uzalishaji wa vikombe hivyo sasa kufanyika nchini.

Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani akiwa ameshika moja ya vikombe (insulators) vinavyozalishwa katika kiwanda cha Inhemeter jijini Dar es Salaam.Kulia kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Amos Maganga na wengine ni watendaji kutoka Wizara ya Nishati, TANESCO na kiwanda cha Inhemeter.

Dkt.Kalemani ametoa agizo hilo jana baada ya kukagua shughuli za uzalishaji wa vikombe hivyo katika Kiwanda cha Inhemeter kilichopo wilayani Kinondoni mkoani Dar es Salaam.

“Nilikuja hapa mwezi Novemba mwaka jana kukagua uzalishaji wa mita za umeme na nikatoa agizo kuwa vikombe navyo visiagizwe nje ya nchi na viwanda vya uzalishaji wa vikombe vijengwe ndani ya nchi, hivyo nimekuja kufuatilia agizo hilo na kujiridhisha kama vikombe vinazalishwa au havizalishwi,” amesema Dkt.Kalemani.

Mashine Tatu kati ya Nne zilizopo katika kiwanda cha Inhemeter ambazo hutengeneza vikombe (insulators) zinazotumika kwenye miundombinu ya usafirishaji na usambazaji umeme.

Baada ya kufanya ukaguzi katika kiwanda hicho, Dkt. Kalemani amesema kuwa, amejiridhisha kuwa kiwanda kinazalisha vikombe takriban milioni 1.5 kwa mwaka na pia kiwanda kingine cha Africab kinazalisha vikombe Milioni Moja kwa mwaka huku mahitaji kwa sasa yakiwa ni vikombe Milioni M1.8.

Kutokana na uzalishaji huo, Dkt.Kalemani ameeleza kuwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Wakala wa Nishati Vijijini (REA) pamoja na wakandarasi wa umeme wanunue vikombe na vifaa vingine vya umeme vinavyozalishwa ndani ya nchi, hali itakayopelekea wananchi kuunganishiwa umeme kwa kasi.

Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani akiwa ameshika moja ya vikombe (insulators) vinavyozalishwa katika kiwanda cha Inhemeter jijini Dar es Salaam.Kulia kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Amos Maganga na wengine ni watendaji kutoka Wizara ya Nishati, TANESCO na kiwanda cha Inhemeter

Ameeleza kuwa, kuna faida mbalimbali za kuzalisha vifaa hivyo ndani ya nchi ikiwemo vifaa husika kupatikana kwa bei nafuu kulinganisha na vifaa vinavyoagizwa kutoka nje ya nchi, vifaa hivyo kutengenezwa kwa ubora na kuongeza ajira ndani ya nchi.

Aidha, ameipongeza kampuni hiyo kwa kuzalisha vifaa hivyo na kutoa ajira kwa vijana wa kitanzania takriban 150.

Ametoa wito kwa watendaji wa kiwanda hicho kuongeza uzalishaji wa vikombe hivyo ambavyo hufungwa katika miundombinu ya usafirishaji na usambazaji umeme ya uwezo tofauti ikiwemo 11kV, 33kV na 400kV.

Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani akiangalia baadhi ya vifaa katika kiwanda cha Inhemeter ambacho hutengeneza vikombe (insulators) zinazotumika kwenye miundombinu ya usafirishaji na usambazaji umeme. Wa pili kushoto ni Kaimu Kamishna wa Petroli na Gesi, Sebastian Shana na Kulia kwa Waziri ni Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Amos Maganga na wengine ni watendaji kutoka Wizara ya Nishati, TANESCO na kiwanda cha Inhemeter.

Insulators (vikombe) hufungwa kati ya nguzo na nyaya za umeme kwa lengo la kuzuia umeme huo kusafiri kupitia kwenye nguzo na baadaye kuleta madhara mbalimbali ikiwemo ya moto.

Katika ziara yake jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nishati aliambatana na watendaji mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati, Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).